Iran yahimiza kukomeshwa ghasia katika mji mkuu wa Libya, Tripoli
(last modified Thu, 15 May 2025 11:44:14 GMT )
May 15, 2025 11:44 UTC
  • Iran yahimiza kukomeshwa ghasia katika mji mkuu wa Libya, Tripoli

Iran imeelezea wasiwasi wake kuhusu mapigano makali yanayoendelea kati ya makundi yenye silaha katika mji mkuu wa Libya Tripoli, ikitaka kusitishwa mara moja ghasia na umwagaji damu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei ameyasema hayo leo Alkhamisi huku kukiwa na ripoti za mapigano kati ya kundi la waasi la Radaa na Brigedi ya 444, linalomuunga mkono Waziri Mkuu wa Libya, Abdulhamid al-Dbeibeh, mjini Tripoli.

Esmaeil Baghaei amezitaka pande zote zinazohusika katika makabiliano hayo kusaidia juhudi za kurejesha utulivu nchini Libya na kufuata njia ya mazungumzo ili kutatua tofauti zao, na vilevile kutoruhusu uingiliaji haribifu wa kigeni katika masuala ya ndani ya Libya.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ametuma salamu za rambirambi na kueleleza masikitiko yake kwa familia za waliouawa na kujeruhiwa katika ghasia hizo.

Mapigano hayo yalizuka kwa mara ya kwanza Jumatatu iliyopita kufuatia kuuawa kwa kiongozi wa kundi moja la wanamgambo, Abdelghani al-Kikli na kushindwa ghafla kwa kundi lake la Stabilization Support Apparatus (SSA) na makundi yenye mfungamano na Dbeibeh.

Ingawa siku iliyofuata, serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa ilisema imedhibiti hali ya mambo, lakini mashahidi na vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuanzishwa tena kwa mapigano hayo mjini Tripoli.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) pia umetoa wito wa kuwepo utulivu, na kuonya kwamba hali ya sasa inaweza "kutoka nje ya udhibiti".