Grossi: Tumekubaliana na Iran kuendelea na mchakato wa uhakiki
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amekaribisha makubaliano yaliyofikiwa baina ya wakala huo na Iran juu ya suala la usimamizi na kuendelea mchakato wa kuthibitisha kwamba miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika kwa malengo ya amani.
Rafael Grossi amesema hayo katika kikao cha Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Ameongeza kuwa: "Tumekubaliana na Iran kwamba IAEA iruhusiwe kuendelea na usimamizi na uhakiki na kwamba: anakaribisha maamuzi ya Iran wa kudhamini kutekeleza hatua zaidi za mchakato wa kuthibitisha kwamba miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika kwa malengo ya amani.
Katika mkutano huo wa Bodi ya Magavana ya IAEA, Rafael Grossi ameashiria pia ziara yake ya karibuni mjini Tehran na mazungumzo aliyofanya na viongozi mbalimbali wa ngazi ya juu wa Iran akiwemo Rais Ebrahim Raisi.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) amesema: Pande zote mbili zinakiri kuwa ushirikiano chanya unaweza kuandaa njia ya kufikiwa makubaliano makubwa zaidi kati ya nchi wanachama na kwamba siku kadhaa zijazo maelezo zaidi yatatolewa kwa nchi wanachama wa Bodi ya Magavana kuhusu mazingira yanayohusiana na majukumu ya Iran katika fremu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na makubaliano ya NPT.
Tarehe 4 Machi na mwishoni mwa ziara ya siku mbili ya Rafael Grossi mjini Tehran, kulitolewa taarifa ya pamoja kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki iliyosisitzia kwamba Iran na kwa hiari yake inaruhusu shirika hilo kufanya shughuli zaidi za uhakiki na ufuatiliaji ikiwa italazimu.
Mbinu ya utekelezaji wake itaafikiwa baina ya pande hizo mbili katika mkutano wa kiufundi utakaofanyika hivi karibuni mjini Tehran.