Mar 28, 2023 07:17 UTC
  • Watu 6, wakiwemo watoto 3 wauawa kwa kupigwa risasi shuleni Marekani

Watu sita wakiwemo wanafunzi watatu wameuawa kwa kupigwa risasi wakiwa shuleni katika mji wa Nashville, jimbo la Tennessee kusini mwa Marekani.

Mkuu wa Polisi katika jimbo hilo, John Drake amesema aliyetekeleza ukatili huo dhidi ya shule binafsi ya Kikristo ya The Covenant ni mwanamke kwa jina Audrey Elizabeth Hale.

Hale anasemaka kuwa wanafunzi wa zamani wa shule hiyo, na kwamba alikuwa amebadilisha jinsia yake na kujiarifisha kama mwanaume.

Mkazi huyo wa mji wa Nashville aliyekuwa na umri wa miaka 28 ameuawa pia na maafisa usalama katika tukio hilo la jana Jumatatu. Polisi ya US imesema inachunguza lengo la mwanamke huyo aliyebadilisha jinsia kufanya unyama huo huku akiwa amejizaiti kwa silaha nzito na bastola. 

Duru za habari zinaarifu kuwa, Hale ameacha nyuma 'manifesto' inayoonesha kuwa alikuwa amedhamiria kufanya wimbi la mashambulizi katika maeneo kadhaa ya mji huo.

Hali ya mshike-mshike katika shule binafsi ya Kikristo ya The Covenant

Mwishoni mwa Januari mwaka huu, watu kumi waliuawa kwa kupigwa risasi kwa umati huko Monterey Park, California nchini Marekani wakati wa sherehe za Mwaka Mpya wa Kichina.

Ufyatulianaji wa risasi kiholela ni jambo linaloonekana kuwa la kawaida nchini Marekani, huku jitihada za kupasisha sheria ya kudhibiti umiliki wa silaha hizo zikikwamishwa na lobi za wazalishaji na wamiliki wa bunduki.

Mwaka uliopita 2022, Marekani ilikumbwa na visa zaidi ya 600 vya ufyatulianaji risasi , karibu mara mbili ya idadi iliyorekodiwa miaka minne iliyopita wakati kulikuwa na visa 336. Kiwango cha vifo vinavyosababishwa na silaha za moto kinazidi kuongezeka nchini Marekani. Aidha ununuzi wa bunduki ulipanda hadi viwango vya rekodi mnamo 2021 na 2022.

Tags