Dalili za kufifia kundi la G7 katika uchumi wa dunia
Mkutano wa mawaziri wa fedha na wakuu wa benki kuu za kundi la G7 la nchi zilizoendelea kiviwanda ulifanyika Niigata, Japan; na kama ilivyokuwa katika mikutano mingine ya nchi za Magharibi na washirika wao, mkutano huo pia umeathiriwa na maswala ya kisiasa na usalama, ikiwa ni pamoja na vita vya Ukraine, suala la nyuklia la Korea Kaskazini, na hatimaye Uchina.
Waziri wa Fedha wa Marekani, Janet Yellen, na Waziri wa Fedha wa Japan Shun'ichi Suzuki, walikutana pembezoni mwa mkutano wa G7 kujadili vikwazo dhidi ya Russia.
Hii ina maana kwamba, nchi wanachama wa G7 (Ujerumani, Ufaransa, Italia, Japan, Uingereza, Marekani na Canada), hasa Marekani, zinahisi kikamilifu mabadiliko ya nguvu ya kimataifa kutoka Magharibi hadi Mashariki; na kwa kuwa hazina uwezo wa kushindana na kudhibiti mabadiliko hayo, zinafanya mikakati ya kuzusha na kuibua matatizo na mikingamo ili kuzusha migogoro ya kimataifa, na mfano wa wazi wa jambo hilo ni mgogoro wa Ukraine, ambapo Marekani inajaribu kuitumbukiza dunia katika hali ya machafuko kwa kutumia njama hiyo inayotekelezwa kwa mahesabu makubwa.
Rajya Singh Yadav, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: "Inaonekana kuwa Kundi la G7 limefika mwisho wa mstari, na sasa kunadhihiri makundi mapya na yenye ushawishi mkubwa duniani kama Jumuiya ya Ushirikiano ya BRICS ambayo kwa namna fulani ni kielelezo cha maendeleo na nguvu ya Mashariki dhidi ya Magharibi. Katika hali hii, nchi kama Japan zitajitengenezea matatizo ya kikanda kwa kufuata kibubusa sera za Marekani."
Tunapotazama mwenendo wa maendeleo ya kundi la BRICS tunaona kuwa, ni mshindani mkubwa wa G7 katika eneo la Mashariki mwa dunia. Mchango wa nchi wanachama wa kundi la BRICS katika uchumi wa dunia umeongezeka kwa zaidi ya asilimia nane tangu kuanzishwa kwa kundi hili mwaka 2009 hadi 2020. Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, mwaka 2009, wakati kundi la nchi zinazoibukia kiuchumi linalojulikana kwa jina la BRICS lilipoundwa, likiwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, sehemu ya nchi hizo tano katika Pato la Taifa la dunia ilikuwa asilimia 15.9. Mwaka 2009, jumla ya pato la taifa la Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini lilikuwa dola bilioni 9,662, na mwaka 2020 lilifikia dola bilioni 20,646. Kwa hivyo, kwa ushirikiano wa nchi hizi tano, sehemu yao katika uchumi wa dunia imeongezeka polepole na kufikia asilimia 24.4 mnamo 2020. Sambamba na kupata ustawi wa kiuchumi, nchi hizo pia zimeamua kutumia sarafu zao za kitaifa badala ya dola ya Marekani, jambo ambalo ni pigo kubwa kwa hadhi ya uchumi ya Marekani duniani.
Matokeo ya utafiti wa Taasisi ya Acorn Macro ya Uingereza yanaonyesha kuwa, jumla ya pato la taifa la nchi za BRICS ni zaidi ya jumla ya pato la taifa la nchi za G7. Kwa msingi huo inaonekana wazi kuwa, nguvu ya masuala mbalimbali za kisiasa na kiuchumi inahama kutoka Magharibi na kuelekea Mashariki. Kwa sababu hiyo, Marekani, ambayo imetanguliza mbele sera ya kuanzisha vita baridi na nchi za Mashariki, ikiwamo China, na kuziunganisha nchi kama Japan katika vita dhidi ya Russia, inajaribu kupindua meza kwa maslahi yake kwa na kuonesha kuwa ulimwengu wa Magharibi umeungana.
Mtaalamu wa masuala ya kimataifa, Li Miadong pia anasema: "Lengo la Marekani ni kuibua migogoro ya kiusalama katika maeneo mbalimbali ili kuathiri ukuaji na ustawi wa uchumi wa nchi za Mashariki. Kwa hivyo, Washington inajaribu kudumisha hadhi ya Magharibi kwa kutumia migogoro ya kiusalama, lakini unaonekana kuwa, hali ya mambo inakwenda kinyume na matakwa ya Marekani kutokana na kuimarika miungano kama ule wa BRICS."
Kwa vyovyote vile, kutokana na hamu ya nchi kama vile Argentina, Iran, Indonesia, Misri, Mexico, Pakistan, Saudi Arabia na baadhi ya nchi nyingine kujiunga na kundi la BRICS, tunaweza kusema kuwa kundi hili linaelekea kuwa muungano muhimu zaidi wa kiuchumi duniani, ambao utazuia njama na majaribio ya nchi za Magharibi ya kutaka kuathiri vibaya ustawi wa uchumi wa Mashariki.
Kwa kutilia maanani hayo yote inaonekana kuwa, kundi la G7 haliwezi tena kutumia ubabe wake wa kiuchumi kwa ajili ya kutwisha na kulazimisha maoni na matakwa yake kwa uchumi wa dunia, na hii ina maana ya kufifia kwa nguvu ya Magharibi na tawi lake la kiuchumi, yaani kundi la G7.