China:Uhusiano wetu na Marekani uko katika kiwango cha chini kabisa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i98960-china_uhusiano_wetu_na_marekani_uko_katika_kiwango_cha_chini_kabisa
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa China amesema kuwa uhusiano wa nchi hiyo na Marekani umefika katika kiwango cha chini kuwahi kushuhudiwa katika historia na kutahadharisha kuwa hali hiyo haina maslahi kwa nchi yoyote ile.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 19, 2023 05:28 UTC
  • Qin Gang
    Qin Gang

Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa China amesema kuwa uhusiano wa nchi hiyo na Marekani umefika katika kiwango cha chini kuwahi kushuhudiwa katika historia na kutahadharisha kuwa hali hiyo haina maslahi kwa nchi yoyote ile.

Qin Gang, Waziri wa Mambo ya Nje wa China amenukuliwa na televisheni ya taifa ya nchi hiyo akibainisha hayo jana katika mazungumzo yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken aliyekuwa ziarani mjini Beijing. Gang amesema, China imekuwa ikifuatilia sera thabiti na kuwepo ushirikiano wa pande mbili kwa maslahi ya pande zote. Amesema, wanataraji kuwa upande wa Marekani utakuwa na msimamo wa mantiki kuhusiana na China.

Uhusiano wa China na Marekani umezorota kutokana na masuala mengi ikiwa ni pamoja na biashara, teknolojia na usalama wa kikanda. Mwezi uliopita Mao Ning msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema kuwa Beijing haioni umuhimu wa kuendelea na mazungumzo na Marekani, wakati Washington inaendelea kutekeleza sera mbovu mkabala wa Beijing ikiwa ni pamoja na hatua kandamizi za kiuchumi na uingiliaji wa kisiasa katika masuala ya China.