Jul 07, 2023 03:09 UTC
  • Trump: Rais Biden ni mraibu wa mihadarati ya cocaine

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump amedai kuwa Rais Joe Biden wa nchi hiyo ni mtumiaji wa mihadarati aina ya cocaine, na kwamba vyombo vya habari vya nchi hiyo vinajaribu kufifiliza kashfa ya kupatikana dawa hiyo ya kulevya ndani ya Ikulu ya White House.

Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa TruthSocial, Trump amehoji, "Je kuna mtu anadhani cocaine iliyopatikana katika eneo la West Wing ndani ya Ikulu ya White House inatumiwa na mtu mwingine ghairi ya Biden na (mtoto wake wa kiume) Hunter?"

Trump ameongeza kuwa, "Vyombo bandia vya habari hivi karibuni vitaanza kudai kuwa kiwango cha mihadarati hiyo kilichopatikana White House ni kidogo, na labda si cocaine, bali ni dawa tu kama asprini."

Ikulu ya White House ya Marekani karibuni ilikumbwa na sakata jingine baada ya kifurushi cha mihadarati aina ya cocaine kinachoripotiwa kuwa cha Hunter Biden, mtoto wa Rais wa Marekani, Joe Biden kupatikana ndani eneo la West Wing katika makazi hayo rasmi ya rais.

Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, maafisa wa Kitengo cha Ulinzi wa Rais wa Marekani maarufu kama Secret Service (USSS), Jumapili iliyopita walipata kifurushi hicho na kudai kuwa ni kitu kisichojulikana.

Cocaine ilipatikana katika ubavu wa kushoto wa White House

Hata hivyo duru za habari zimeliambia gazeti hilo kuwa, kifurushi hicho kilikuwa cha mihadarati aina ya cocaine inayomilikiwa na Hunter Biden, mtoto wa kiume wa Rais wa Marekani ambaye anakabiliwa na kashfa nyingi za kimaadili na rushwa.

Maafisa wa White House hata hivyo wanadai kuwa si Biden wala mwanawe Hunter walikuwa katika Ikulu ya White House wakati wa kupatikana mihadarati hiyo.

Tags