Jumatatu, 04 Novemba, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe Pili Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 4 Novemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1055 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia malenga wa Kiirani, Abu Is'haq Kesa-i Marvazi.
Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasamani na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (SAW) na kizazi chake hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Kesa-i Marvazi mbali na kusifika kwa utunzi wa mashairi, lakini pia alitoa waadhi na hekima kupitia mashairi yake ya Kifarsi. Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameandika ya mashairi.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, wakati wa harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala dhalimu wa Shah, serikali ya Sharif Emami ililazimika kujiuzulu.
Jafar Sharif Emami alikuwa kibaraka wa ukoloni wakati wa kupamba moto harakati za wananchi Waislamu na alikuwa akitoa ahadi za uongo kwa lengo la kupotosha mwelekeo wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Baada ya Sharif Imami, Jenerali Azhari aliunda serikali ya kijeshi. Hata hivyo Imam Khomeini aling'amua njama na hila za kiongozi huyo na kutangaza kwamba, mawaziri wakuu wanaobadilishwa ni vibaraka wa Shah na ubeberu na akawataka wananchi wasihadaike na hila za viongozi hao bali waendeleze harakati za mapambano za kutaka kuangusha utawala dhalimu wa Shah.
Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita kulifunguliwa maonyesho ya kwanza ya kimataifa ya vitabu mjini Tehran.
Maonyesho hayo yalishirikisha makampuni na taasisi 196 za uchapishaji vitabu za kigeni kutoka nchi 32 duniani yaliyokuwa na vitabu zaidi ya elfu 16. Vilevile taasisi 215 za uchapishaji za ndani ya Iran zilishiriki katika maonyesho hayo.
Tangu mwaka huo Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran yamekuwa yakifanyika kila mwaka hapa nchini.
Na miaka 29 iliyopita katika siku kama hii ya leo Yitzhak Rabin, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel aliuawa na Mzayuni mwenye misimamo ya kufurutu ada.
Rabin alikuwa Waziri Mkuu wa Israel kuanzia mwaka 1974 hadi 1977 kwa tiketi ya Chama cha Leba. Hata hivyo aliuzuliwa wadhifa huo kwa tuhuma za ubadhirifu.
Ni muhimu kukumbusha kuwa, Yitzhak Rabin alikuwa miongoni mwa makamanda wa makundi ya kigaidi ya Kizayuni.