Aug 10, 2025 02:28 UTC
  • Jumapili, 10 Agosti 2025

Leo ni Jumapili 16 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria mwafaka 10 Agosti 2025.

Miaka 206 iliyopita katika sikuu kama ya leo, nchi ya Colombia ijipatia uhuruu baada ya Simon Bolivar mpigania ukombozi wa Amerika ya Kusini kupata ushindi dhidi ya jeshi la Uhispania. Nchi hiyo ilikuwa chini ya udhibiti na ukoloni wa Uhispania.

Simon Bolivar

 

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano yaliyojulikana kwa jina la The Treaty of Sèvres kati ya utawala wa Othmaniya uliokuwa umeshindwa katika Vita vya Kwanza vya dunia na waitifaki wake. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utawala wa dola ya Othmaniya ulipoteza karibu asilimia 80 ya ardhi yake iliyokuwa ikiitawala, na kupunguza eneo ililokuwa ikilitawala kutoka kilomita mraba milioni tatu hadi kilomita mraba laki sita tu. Makubaliano hayo yalitambua rasmi makubaliano ya awali ya Ufaransa na Uingereza juu ya kugawana ardhi iliyokuwa ikitawaliwa na dola ya Othmania, ambapo Uingereza ilizitawala Iraq, Jordan na Palestina na Ufaransa nayo ilizitwaa na kuzidhibiti Syria na Lebanon.

 

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita, vilianza vita vya miaka miwili kati ya Japan na China juu ya mzozo wa maeneo ya Yangtze na Canton ambayo yalikuwa maeneo ya kistratijia ya ardhi ya China. Canton ilikuwa bandari muhimu mno huko kusini mwa China ambayo Wachina walipigana vita vya miaka miwili kuilinda mbele ya uvamizi wa Wajapani. Hata hivyo na baada ya kupata hasara kubwa tarehe 25 Aprili 1939 bandari ya Canton ikatwaliwa na Japan. Utawala wa Japan uliendelea kujipanua katika ardhi ya China kwa kudhibiti maeneo mengine ya mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo Wajapani walilazimika kurudi nyuma kutokana na mapambano makali ya wananchi wa China.

 

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, kufuatia kushindwa kikamilifu Japan katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kwa mujibu wa maazimio ya Kongamano la Potsdam, maeneo ya kaskazini mwa Korea yalidhibitiwa na Jeshi Jekundu la Urusi ya Zamani. Kabla ya kushindwa Japan, maeneo hayo yalikuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo. Aidha baada ya siku chache maeneo ya kusini ambayo ni kisiwa  yakadhibitiwa na Marekani. Kudhibitiwa maeneo ya kaskazini na kusini ya Korea ulikuwa utangulizi wa kugawanywa ardhi hiyo katika nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini.