Kufa shahidi Rais wa watu na mchapakazi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/radio/iran-i112084
Kwaheri chimbuko la fahari ya taifa la Iran, kwaheri Kiongozi wa Mashahidi Wahudumu wa nchi hii kwa kazi uliyofanya, kwaheri shakhsia ambaye hukusita kutetea na kuupigania Uislamu, tulikupenda kuliko unavyofikiri; hatutakusahau wewe na marafiki zako. 
(last modified 2024-05-23T07:46:24+00:00 )
May 23, 2024 07:46 UTC
  •  Kufa shahidi Rais wa watu na mchapakazi wa Iran

Kwaheri chimbuko la fahari ya taifa la Iran, kwaheri Kiongozi wa Mashahidi Wahudumu wa nchi hii kwa kazi uliyofanya, kwaheri shakhsia ambaye hukusita kutetea na kuupigania Uislamu, tulikupenda kuliko unavyofikiri; hatutakusahau wewe na marafiki zako. 

Usiku wa ajabu na mgumu ulioje wa Jumapili iliyopita; mgumu kama ule wa kumpoteza baba, karibu sote tulijua kilichotokea lakini hatukutaka kuamini. Kwa kiasi gani tulikumbuka mwezi Juni mwaka 1989. Walisema, tumuombee afya Imam Khomeini Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu. Watu walinyanyua mikono juu kuomba dua na kuswali misikitini, vichochoroni na barabarani, na hata majumbani mwao, lakini ilipofika asubuhi, wote walikuwa wamevaa nguo nyeusi.

******              *****

Jumapili usiku iliyopita tulitamani kwamba mwisho wa usiku huo mweusi usiwe kama usiku ule wa mwaka 1989. Tulitaka kumuona Sayyid Ebrahim Raisi akiwa salama asubuhi mkabala wa televisheni akiwawafariji wananchi. Tulikuwa tukisema kuwa kwa kuwa yeye ni mnyenyekevu atawaomba radhi wananchi kwa masaa hayo kadhaa ambayo tulikuwa tumekumbwa na wasiwasi kuhusu hali yake, hata hivyo aliondoka akiomba radhi kwa ajili ya Siku ya Kiyama na kujikabidhi kwa Mola Mlezi.

Mwili wa shahidi Rais wa Iran ukipitishwa mbele ya wananchi 

Tulimpoteza mapema sana Imam na Mwasisi wa mapinduzi yetu. Kila mtu alifikiria kuwa baada yake pia tutapoteza mapinduzi yetu. Alipoaga dunia maadui zetu walifurahi lakini sisi tuliridhia kwa ridhaa yako (Mwenyezi Mungu). Tulifuata mafundisho ya Imam na kuandika mara nyingi kuhusu mifano hii ya dhahabu ili Iran ya Kiislamu iwe na nguvu na kusalia imara. Tuliikabidhi bendera kwa mikono iliyobarikiwa ya Imam Khamenei; mtu yule yule aliyenusurika kuuawa miaka kaadha iliyopita ambaye mpango wake umekuwa kuendelea kuwa mbeba bendera. Ni katika miaka hiyo ambapo Iran ya Kiislamu ilipoteza nguvu na mtaji mkubwa wa rasilimali watu.

Sayyid Ebrahim Raisi ni Rais wa pili wa Iran kufa shahidi. Muhammad Ali Rajai ni Rais wa kwanza shahidi wa Iran ambaye alifanya kazi usiku na mchana bila kusita kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Hapa tunashuhudia ni kwa kiasi gani mashahidi hawa wawili wanashabihiana. Uaminifu, ikhlasi, na Uchamungu ni  miongoni mwa sifa za kiutu za  viongozi hawa wawili, na zaidi ya hayo, viongozi hawa walifanya kila walichoweza kwa manufaa ya wananchi. Ingawa vipindi vya urais vya mashahidi hawa wawili havikumalizika, lakini wote wawili walifanya kazi kubwa na kuwahudumia vyema wananchi na kushughulia matatizo yao; na miongoni mwa huduma hizo ni kwamba walifanikiwa kujenga uhusiano mwema kati yao na wananchi.  

Shahidi Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran 

Raisi alizaliwa Mashhad na alifiwa na baba yake akiwa na umri wa miaka mitano. Tokea hapo  kichwani mwake alihisi kivuli cha baba mkarimu. Baba wa nuru, ambaye Wairani wote wamemwona kuwa mmiliki wa nchi yao na kumkimbilia ili apate kuwatatulia matatizo yao. Tangu wakati huo, shahidi Ebrahim Raisi alikuwa na mapenzi kifuani mwake kwa Imam Reza (AS)  hadi alipoteuliwa rasmi mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 55 kwenye nafasi ya Msimamizi wa Haramu Tukufu ya Imam Reza (A.S), Imam wa nane wa Waislamu wa Shia. Siku zote Raisi alikuwa karibu na Imam Reza (AS) katika muda wake wa faragha. Ilikuwa ni katika miaka hiyo ambapo alikuwa akifanya kila alichoweza kuwahudumia watu wa mji wa Mash'had na waumini wanaokwenda kufanya ziara katika mji huo, na hivyo akajulikana kama  Mhudumu wa Haram ya Imam Reza.

Hujattul Islam wal Muslimin Sayyid Ebrahim Raisi hakuwahi kukosa kumtumikia Imam Reza (AS) na waumini wanaofanya ziara licha ya majukumu yote aliyokuwa nayo; na alikuwa akishiriki katika zamu yake ya kutumikia Haram Tukufu na wafanya ziara huko Mash'had mpaka siku ambayo alipata ujira na zawadi ya kuhudumu kwa miaka mingi katika haramu ya Imam Reza (AS) baada ya kufa shahidi katika njia ya kuhudumia Uislamu na Waislamu. Alifanikiwa kufikia matarajio yake ya muda mrefu katika siku ya kumbukizi ya kuzaliwa Imam Reza AS. Aidha miaka sita iliyopita Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) alikuwa ameelekea katika mji wa Mash'had; na Ebrahim Raisi alikuwa amemwalika kwa ajili ya kufanya usafi katika eneo la  kaburi tukufu la  Imam. Sayyid Ebrahim alisema:" Hali ya Haj Qassim ilibadilika siku ile alipokuja kufanya usafi katika eneo la kaburi lenye kung'aa la Imam Reza (AS).   

Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi enzi za uhai wake akifanya usafi katika haram la Imam Reza (A.S)

Mtumishi huyo wa Imam Reza (A.S) alihudumu katika nafasi ya Rais hadi dakika ya mwisho na alisabilia maisha yake yote kuwatumikia wananchi khususan wananchi wanyonge na wa matabaka ya chini. Huyo ndiye Shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.