Mwanadiplomasia Shahidi Hossein Amir abdollahian
(last modified Wed, 29 May 2024 07:04:25 GMT )
May 29, 2024 07:04 UTC
  • Mwanadiplomasia Shahidi Hossein Amir abdollahian

Tumeawandalia makala hii ya wiki ambayo itatupia jicho shakhsia ya Shahidi Hossein Amir Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran. Hossein, kama alivyokuwa akisema; ni mtu wa kijijini aliyekuwa akipenda tini, na Mwenyezi Mungu anaapa kwa tini na zeituni katika Qur'ani kwamba wale walioamini na wakatenda mema watapata malipo makubwa Kwake.

Alizaliwa katika mji wa Damghan, mkoani Semnan ambao ni maarufu kwa pistachio zake za kupendeza.   

Hossein alizaliwa tarehe 4 mwezi Ordibehesht mwaka 1343 Hijria Shamsiya sawa na Aprili 1964. Alikuwa na umri wa karibu miaka sita alipofiwa na babake na kuwa yatima. Katika miaka hiyo, aliishi maisha rahisi na ya kawaida kabisa na familia yake. Baada ya kuaga dunia baba yake, matatizo ya maisha yalizidi lakini Abdollahian siku zote alikuwa na matumaini na mustakbali. 

Alikuwa na umri wa miaka 14 Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi; na alikuwa na shauku maalumu ya kushiriki katika maswala ya kijamii sawa kabisa na mabarobaro na vijana wengine wanamapinduzi. Alipoamua kwenda chuo kikuu, alikubaliwa kwanza kujiunga na masomo ya maabara, lakini haikuwa vile alivyotarajia. Alitaka kufanya mambo muhimu zaidi kwa ajili ya Iran ya Kiislamu; hivyo aliamua kuacha masomo hayo, na mwaka uliofuata kwa mara nyingine akafanya mtihani wa kujiunga na chuo kikuu na safari hii alikubaliwa kusomea taaluma ya uhusiano wa kidiplomasia katika chuo cha Wizara ya Mambo ya Nje. Baada ya hapo aliendelea na masomo ya uhusiano wa kimataifa katika ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu katika Chuo Kikuu cha Tehran na hivyo kuhudumu katika uga wa siasa za nje za Iran. 

Kazi ya kwanza ya kisiasa ya Hossein Amir Abdollahian ilikuwa ni kuhudumu katika ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Baghdad mji mkuu wa Iraq kama mtaalamu wa Naibu Balozi. Baada ya hapo mnamo mwaka 2002 Abdollahian alikuwa Naibu Mwakilishi Maalumu wa Waziri wa Mambo ya Nje katika Masuala ya Iraq. Miaka mitano baadaye wakati utawala wa Baath ulipoanguka kulifanyika kikao kufuatia ombi la Marekani kwa ajili ya kudhamini usalama wa Iraq. Amir Abdollahian alikuwa mkuu wa timu ya mazungumzo ya Iran kwenye kikao hicho.

Katika mwaka huo, Amir Abdollahian alianza kazi kama Balozi wa Iran nchini Bahrain, na miaka miwili iliyofuata sambamba na kuanza kazi serikali ya kumi hapa nchini mwaka 2009 Abdollahian aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya nchi za Kiarabu na Kiafrika. Aliendelea kuhudumu katika nafasi hiyo pia hadi mwanzoni wa uongozi wa serikali ya 12.

Kazi muhimu ya mwanadiplomasia Hossein Amir Abdollahian katika miaka yote hiyo ilikuwa ni kukabiliana na kuenea kwa makundi ya kigaidi hata hivyo majukumu yake yaliongezeka baada ya kujiimarisha kundi la Daesh katika eneo. Abdollahian alikuwa bega kwa bega na shahidi Haj Qassim Suleimani Kamanda wa kikosi cha Quds cha jeshi la walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mapambano dhidi ya Daesh na taratibiu nafasi na mchango wake ukaanza kujulikana miongoni mwa nchi za ukanda wa muqawama na Asia Magharibi. Luteni Jenerali Qassim Suleimani mara kadhaa alikuwa akielekea Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran bila ya taarifa kwa ajili ya mashauriano na Abdollahian kuhusu masuala mbalimbali ya eneo. Baadhi ya waandishi wa habari wa upande wa sera za nje walikuwa wakimwita Abdollahian kwa jina la Qassim Suleimani wa uga wa diplomasia. Walikuwa wakikutana na kufanya mazungumzo bila ya hafla yoyote; na  nikatika mazingira hayo ya kawaida kabisa na pasina na kujiona na ghururi yaliyopelekea shakhsia wawili hao kuwa karibu sana.  

Shahidi Kamanda Suleimani 

Vita vya uharibifu vilianza huko Syria mwaka mmoja baada ya Hossein kukubali kuhudumu katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran. Wakati huo kundi la kitakfiri la Daesh lilikuwa tayari limeingia katika ardhi ya Syria na kutishia usalama wa eneo. Ushirikiano wa Hossein Amir Abdollahian na Kamanda Suleimani ulianza tangu huko nyuma kwani wawili hao hata walikuwa wakiwasiliana wakati wa mapambano huku wakifanya juhudi za kurejesha amani katika eneo. Mmoja katika uga wa diplomasia na mwingine katika uga wa kijeshi. Diplomasia yao ililenga kuleta uthabiti na usalama katika eneo na kuzuia kuenea Uzayuni kama sababu kuu ya hali ya mchafukoge katika eneo. 

Hossein Amir Abdollahian amehadithia kumbukumbu zake za vita vya Syria katika kitabu kwa jina la " Subh-e-Sham" ambacho ni moja ya chambuzi za awali na chache zaidi zilizopo kuhusu vita vya Syria. Shahidi mwanadiplomasia Hossein Amir Abdollahian ameeleza kumbukumbu zake nyingi katika kitabu hicho kuhusu ushirikiano wake na shahidi Suleimani na sifa maalumu za kamanda huyo. Amir Abdollahian ameandika katika sehemu moja ya kitabi hicho kwamba: "Nilikuwa nimeelekea Damascus wakati vita vilipopamba moto kwa lengo la kukutana na kuzungumza na Rais Bashar al Assad wa Syria. Nilialikwa na Luteni Jenerali Suleimani kuhudhuria mkutano huo. Njia ya kuelekea upande yalipo makao makuu ya kamandi ya jeshi la Syria ilikuwa ya kutisha sana utadhani nilikuwa nikisubiri kukutana na viongozi wa Daesh na si kwa ajili ya kukutana na Kamanda Suleimani. Miongoni mwa nyumba zilizokuwa zimebomolewa katika mji huo, Luteni Jenerali Suleimani alikuwa pamoja na maafisa kadhaa wa jeshi la Syria na wanamuqawama wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika kusimamia oparesheni ya kukomboa baadhi ya maeneo ya Syria yaliyokuwa yakishikiliwa na Daesh. Kamanda Suleimani alikuwa mtulivu sana katika mazingira hayo magumu na alikuwa akieneza utulivu huo pia kwa wenzake.  

Shahidi Kamanda Qaasim Suleimani enzi za uhai wake 

Hossein Amir Abdollahian aliaminiwa sana na Kamanda Suleimani na hii ilipelekea kuteuliwa katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran baada ya kushika hatamu za uongozi serikali ya Sayyid Ebrahim Raisi. Mwanadiplmasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran alitilia mkazo kukuza uhusiano na nchi jirani na za Asia katika wadhifa wake huo uliodumu kwa karibu miaka mitatu lakini hiyo haikuwa na maana ya kukata uhusiano na nchi za Ulaya. Pamoja na hayo, kwake yeye na wenzake, Ulaya haikuwa tu nchi tatu za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambazo zimekuwa zikidhihirisha mitazamo na kuchukua kikamilifu maamuzi dhidi ya Iran. Mwendazake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alichukua hatua kubwa ili kupunguza madhara na taathira za vikwazo dhidi ya Iran kwa kupanua uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na nchi za bara la Asia na Afrika na kuhuisha diplomasia ya Iran katika uwanja huo; na hivyo mazingira mapya kwa ajili ya kuanzisha mazungumzo kati ya Tehran na nchi za Ulaya. 

Shahidi Hossein Amir Abdollahian 

Si hayo tu bali Hossein Amiri Abdollahian alikuwa sauti ya muqawama mara baada ya kuanza vita na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza. Jitihada zake ndizo zilizopelekea nchi za Kiislamu kuitisha mikutano mingi ya kujadili suala la kusimamisha vita dhidi ya Gaza. Alipelekea kusikika duniani sauti na vilio vya wanawake na watoto wa Gaza. Abdollahian pia alikuwa mpambanaji wa mhimili wa muqawama katika uga wa sera za nje. 

Helikopta iliyokuwa imembeba Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,  Hossein Amir Abdollahian na ujumbe waliofuatana nao ilipata ajali Jumapili jioni Mei 19, 2024 ilipokuwa ikirejea kutoka kwenye ufunguzi wa bwawa la Qiz Qalasi kwenye mpaka wa pamoja wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.