9 Dei, Siku ya Mwamko na Kushikamana na Wilaya
https://parstoday.ir/sw/radio/iran-i22354-9_dei_siku_ya_mwamko_na_kushikamana_na_wilaya
Ni jambo linalojulikana na wanadamu wote kwamba, hakuna mtu anayeweza kuainisha jinsi ya kuzaliwa au kufariki kwake dunia. Hata hivyo jamii ambayo kama alivyo mwanadamu, inazaliwa na kufa, huwa na taathira katika kubakia hai na katika kufa kwake.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 29, 2016 07:54 UTC
  • 9 Dei, Siku ya Mwamko na Kushikamana na Wilaya

Ni jambo linalojulikana na wanadamu wote kwamba, hakuna mtu anayeweza kuainisha jinsi ya kuzaliwa au kufariki kwake dunia. Hata hivyo jamii ambayo kama alivyo mwanadamu, inazaliwa na kufa, huwa na taathira katika kubakia hai na katika kufa kwake.

Kufa kwa jamii hutokana na kukosa kitu kinachoitwa katika istilahi ya kidini kuwa ni  basira (بَصِیرَةِ), kwa maana ya ung'amuzi, uelewa na uwezo wa kumaizi baina ya vitu na katika hali na mazingira tofauti (intuition). Ung'amuzi na uwezo huo wa kumaizi ndiyo chemchemi ya uhai wa jamii. Kwa msingi huo, jamii yoyote ile inayotaka kulinda uzima na uhai wake na kuepuka mauti ya hatua kwa hatua, inapaswa kulinda hali na uelewa, ung'amuzi na uwezo wake wa kupambanuai baina ya vitu na hali tofauti. Uwezo huo ni kito chenye thamani kubwa kinachoondoa giza la ujinga, kuongeza uwezo wa kuchambua matukio mbalimbali na kumuwezesha mtu au jamii kutabiri kwa njia sahihi matukio ya siku zijazo. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: "Ni rahisi sana kwa mtu kutokuwa na macho kuliko kukosa uwezo wa kung'amua na kumaizi". "فَقْدُ الْبَصَرِ أَهْوَنُ مِنْ فِقْدَانِ الْبَصِیرَةِ"

Jamii yenye ung'amuzi, uelewa, muono wa mbali na umakini ni jamii inayoweza kuainisha njia sahihi katika zama za fitina, matukuio mbalimbali na kwenye tufauni, mawimbi na misukosuko. Katika aya za Qur'ani tukufu Mwenyezi Mungu SW anajitaja Yeye mwenyewe kuwa ni Basiir (بَصیر) na kuna aya kadhaa zinazomtaja SW kwa sifa hiyo ya ung'amuzi, umaizi, uelewa wa kina na kuona mbali. Vilevile Mtume Muhammad (saw) na Qur'ani tukufu ni sababu ya kuwa na sifa na hali hiyo umaizi, ung'amuzi, kuona mbali na kumpa mja uelewa na umakini. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Qur'ani inawataja baadhi ya wanadamu kuwa wanataza kwa macho lakini hawaoni kwa sababu hawana sifa hii ya basiir ambayo ni zaidi ya mtu kuona kwa jicho kiungo. 

Miongoni mwa ujumbe muhimu sana za Qur'ani tukufu ni kuwataka wanadamu kuwa na sifa ya "بَصیر" na kung'amua, kumaizi, kuona mbali na kuwa na uelewa wa kutosha kwa ajili ya kupata ibra na mafunzo na uwezo wa kumaizi njia sahihi na hatima njema. Mitume wa Mwenyezi Mungu SW walikuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba, wafuasi wao wa kweli wanapata sifa hii ya ung'amuzi, uwezo wa kumaizi na kupambania na uelewa wa kina na kufanya harakati zao kwa mujibu wa sifa hiyo. Aya ya 108 ya Suratu Yusuf inasema: Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua (umaizi na ung'amuzi)- mimi na wanaonifuata. Masahaba na wafuasi wa kweli wa mtukufu huyo pia walikuwa na sifa hiyo na walifanya harakati zao kwa kutumia nguvu na sifa ya kumg'amua, kumaizi, uelewa na kuona mbali. Sifa hii pia ndiyo siri ya kubakia hai Uislamu licha ya mashaka, misukosuko na mateso makubwa waliyokabiliana nayo Waislamu wa awali. Ni sifa hii ya uelewa mkubwa, uwezo wa kumaizi na kuona mbali pia ndiyo iliyowafanya wafuasi wa Imam Ali bin Abi Twalib na maimamu wengine katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) kusimama kidete na kustahamili machungu mengi kama kuteswa, kufungwa jela, kupelekwa uhamishoni maeneo ya mbali, kusulubiwa juu ya miji na kuuawa katika njia ya kutetea haki na kushikamana na wasia wa Mtukufu Mtume.

Kwa msingi huo ni jambo la dharura kwa watu kuwa na sifa na uwezo huu wa kumaizi, kung'amua, uelewa mkubwa na muono wa mbali katika malengo, katika kuchaua nyezo, katika kumjua vyema adui na katika kufanya harakati kwa shabaha ya kuibakisha hai jamii na kulinda uzima na usalama wake. Watu wengi wa jamii kama hiyo huwa na uwezo wa kutambua, kung'amua na kumaizi baina ya haki na batili wakati wa misukosuko ya kisiasa na kijamii na huzifanya panga na nyembe za adui kuwa butu na kuondoa vumbi na kiwingu cha fitina katika anga na macho ya watu wa jamii husika.   

Tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia ambayo ilisadifiana na tarehe 30 Disemba mwaka 2009 kulifanyika maandamano ya aina yake hapa nchini Iran ambayo yalikuwa tukio muhimu sana katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu. Tukio hilo kwa hakika linatambuliwa kuwa ni ukurasa wa dhahabu wa kitabu kikubwa cha fahari za taifa la Iran. Tarehe 9 Dei hapa nchini ni nembo ya utukufu, kujitawala na kuwa na sifa ya ung'amuzi na uwezo wa kumaizi baina ya haki na batili wa taifa mbalo liko tayari kusabilia nafsi, mali na kila lililoghali kwa ajili ya kulinda misingi ya Uislamu, itikadi na maadili yake mbele ya hujuma na njama za maadui. 

Siku ya tarehe 9 Dei (30 Disemba 2009) ilikuwa siku ya kudhihirika uadui na uhasama wa wazi na wa nyuma ya pazia wa maadui wa ndani na nje ya nchi mkabala wa utawala wa Kiislamu hapa nchini ambapo maadui wa ndani na nje walilenga shabaha Uislamu, itikadi za kidini, maadili, uongozi wa Iran na mengine mengi ya thamani. Mpambano huo wa haki na batili ulianza tarehe 4 Dei (25 Disemba 2009) baada ya makundi ya watu mamluki na vibaraka wasiojielewa kuanzisha machafuko ya mitaani na kuchanachana picha ya mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Khomeini na baadaye wakachezea shere na kuhujumu shughuli na marasimu ya kidini ya Siku ya Ashuraa yaani shughuli za kidini za kukumbuka tukio chungu la kuuliwa shahidi mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali (as). Ghasia hizo zilizushwa baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Iran. Siku chache tu baada ya tukio hilo la kusikitisha wananchi kote nchini Iran walitengeneza hamasa ya aina yake na kushiriki katika maandamano ya tarehe 9 Dei kulinda na kutetea Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu. Tukio hilo kwa hakika liliwashangaza wachambuzi wengi wa mambo na kuwaacha bumbuazi viongozi wa nchi za Magharibi. Wachambuzi wa mambo na viongozi wa nchi za kibeberu kamwe hawakutasawari wala kuamini kwamba, katika kipindi hicho cha mgogoro waliouchochea dhidi ya mfumo wa utawala nchini Iran na hujuma kubwa ya kisiasa na kijamii na vilevile anga chafu ya kisiasa iliyoandamana na kuzidishwa vikwazo na mbinyo, wananchi wa Iran wangeweza- katika kipindi kifupi- kumaizi na kung'amua baina ya haki na batili na kuthibitisha tena kwamba, licha ya kupita kipindi cha zaidi ya robo karne tangu wafanye Mapinduzi ya Kiislamu nchini, wako tayari kusabilia roho na nafsi zao kwa ajili ya kulinda maadili, dini, itikadi na mapinduzi yao na wanalitambua suala hilo kuwa ni jukumu lao la kidini, kitaifa na kibinadamu. Mwamko na kuwa macho wananchi wa Iran katika hamasa hiyo kulikuwa kukubwa kiasi kwamba Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alisema: Tutakuwa bado hatujatekeleza wajibu wetu iwapo tutasujudu mara mia kadhaa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema kubwa ya kuwa macho na umaizi wa wananchi katika tukio hili. Hii ni hamasa kubwa ambayo imevuruga mahesabu ya adui yaliyopangwa kwa ushirikiano wa baadhi ya watu wachache wenye chuki na vinyongo ndani ya nchi. Katika siku hii, hamasa kubwa Umma Kiislamu imefanya harakati kwa kutumia sifa ya ung'amuzi, umaizi na kuona wa mbali na kuwakatisha matumaini maadui", mwisho wa kunukuu.   

Hapana shaka kuwa, kama si kuona mbali, uwezo wa kung'amua, uelewa mkubwa na sifa ya kumaizi baina ya haki na batili ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Iran, basi kungetokea moto mkubwa wa fitina na hitilafu ambao ingekuwa vigumu kuuzima kwa kipindi kifupi, na suala hilo lingekuwa na taathira mbaya na kubwa kwa jamii nzima. Tadbiri na uongozi makini wa Ayatullah Ali Khamenei katika kipindi hicho nyeti vilizuia jamii kuwa mateka wa hitilafu na fitina zilizozushwa na maadui. Tarehe 9 Dei hapa nchini imesajiliwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kama siku ya hamasa kubwa ya mamilioni ya wananchi waliojitokeza kulinda mapinduzi hayo na thamani na itikadi za Kiislamu na vilevile kutangaza tena utiifu wao kwa Mapinduzi na Kiongozi wake Mkuu baada ya wimbi kubwa la fitina na hitilafu zilizozushwa na maadau kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2009.

Ayatullah Ali Khameni anaizungumzia siku hiyo ya tarehe 9 Dei akisema: "Kimaumbile siku zote za mwaka ziko sawa lakini wanadamu, kwa irada zao na jihadi jitihada zao ndio wanaochagua siku maalumu kati ya siku zote za mwaka na kuifanya makhsusi na tofauti na siku nyingine. Huishika siku hiyo kama bendera ili iwe kinara na kiongozi wa siku nyingine. Siku ya Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram (siku ya mapambano ya mjukuu wa Mtume (sawa) Imam Hussein dhidi ya batili katika medani ya Karbala) kidhati haina tofauti ya siku nyingine za mwaka, lakini Imam Hussein (as) aliipa siku hiyo uhai mpya, aliipa maana mpya na akaipandisha juu na kuipa utukufu mkubwa. Ni jihadi ya wafuasi waaminifu wa Imam Hussein (as) ndiyo iliyoipa siku hiyo umuhimu mkubwa. Vivyo hivyo siku ya tarehe 9 Dei. Kidhati tarehe 9 Dei haina tofauti na tarehe 10 Dei, lakini wananchi, kwa harakati yao iliyotokana na basira yaani sifa ya kumaizi, kung'amua, utambuzi mkubwa, kumjua vyema adui na kutambua alama za nyakati, wameifanya siku hiyo iwe tofauti na siku nyingine za mwaka", msisho wa kunukuu.

Ayatullah Khameeni anasema katika sehemu nyingine kwamba: Kuweni na yakini ya kuwa siku ya tarehe 9 Dei (30 Disemba) itabakia hai katika historia. Hii ni siku tofauti ya nyingine kwa taifa la Iran. Siku hiyo, katika kipindi cha sasa kilichogubikwa na vumbi, ilikuwa na umuhimu mkubwa sana. Unapotazama mazingira ya yaliyotukia katika siku hii utauona mkono wa Mwenyezi Mungu, utaiona roho ya hamasa ya Imam Hussein na utaona roho ya imami ya watu kwa utawala wa Ahlibaiti wa Mtume (saw). Hii ni kazi ya Mwenyezi Mungu", mwisho wa kunukuu.   <<<<<   >>>>.