Rafsanjani, Mwanasiasa wa Aina Yake-3
https://parstoday.ir/sw/radio/iran-i23815-rafsanjani_mwanasiasa_wa_aina_yake_3
Sehemu ya leo ya makala hii itatupia jicho ukurasa wa tatu wa maisha Ayatullah Rafsanjani baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa hadi alipofariki dunia zaidi ya moja moja iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 18, 2017 05:08 UTC
  • Rafsanjani, Mwanasiasa wa Aina Yake-3

Sehemu ya leo ya makala hii itatupia jicho ukurasa wa tatu wa maisha Ayatullah Rafsanjani baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa hadi alipofariki dunia zaidi ya moja moja iliyopita.

Katika makala ya wiki iliyopita tulisema kuwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Hashemi Rafsanjani aliendelea kuwa na nafasi na mchango muhimu sana katika kuimaisha nguzo na misingi ya Jamhuri changa ya Kiislamu. Akiwa chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini, Rafsanjani na wanamapinduzi wenzake walikuwa na nafasi muhimu sana katika kukabiliana na migogoro na changamoto nyingi zilizojitokeza baada ya ushindi wa Mapinduzi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, ni harakati na mapinduzi machache sana duniani ambayo yalikabiliwa na misukosuko, njama na uadui mwingi baada ya kupata ushindi kama ilivyokuwa kwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Harakati za makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu na yaliyotaka kujitenga baadhi ya maeneo ya Iran ambayo yaliungwa mkono na kupewa misaada ya madola makubwa mawili ya dunia wakati huo, yaani Marekani na Russia, mauaji ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu, vikwazo vya kiuchumi na hatimaye vita vya kulazimishwa vlivyoanzishwa na Saddam Hussein na kuendelea kwa kipindi cha miaka 8 katika eneo lenye ukubwa wa kilomita 1200 kwenye mpaka wa nchi hizi mbili, yote yalitengeneza mazingira maalumu na ya aina yake. Kwa hakika kila moja kati ya migogoro hiyo ulitosha kuuangusha na kuusambaratisha mfumo na utawala wowote mchanga. Hata hivyo kusimama kidete kwa taifa la Iran likiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini na kuwepo kwa shakhsia wakubwa kama Rafsanjani kuliliwezesha taifa kuvuka salama kipindi hicho kigumu.

Ransanjani, Ayatullah Khamenei na Ahmad Khomeini

Tulisema katika makala iliyopita kwamba, moja kati ya majukumu ya Ayatullah Hashemi Rafsanjani baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kislamu ni ukamanda wa majeshi yote na kuongoza vita. Katika kipindi hicho Jamhuri ya Kiislamu na kutokana na ushujaa na ujasiri wa vijana wake, ifanikiwa kupata ushindi mkubwa katika medani mbalimbali za vita dhidi ya jeshi lililokuwa limejizatiti kwa silaha mpya na za kisasa kutoka kwa madola mawili makubwa ya Mashariki na Magharibi. Kushindwa kwa Saddam Hussein katika vita hivyo lilikuwa pigo kubwa mno kwa waungaji mkono wake na ushindi mkubwa kwa Iran ya Kiislamu. Kwa msingi huo katika mwaka wa mwisho wa vita hivyo vya kulazimishwa, yaani katika kipindi cha kati ya mwaka 1987 na 1988, Marekani iliamua kuingia rasmi na moja kwa moja katika vita dhidi ya Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Katika upande mwingine nchi za kifalme za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi zikiongozwa na Saudi Arabia, sambamba na kuzidisha misaada yao ya kifedha kwa Saddam zilifanya njama zaidi za kuzuia ushindi mkubwa na mpana zaidi wa Jamhuri ya Kiislamu kupitia njia mbalimbali ikiwemo ya kuzidisha uzalishaji wa mafuta ya petroli kwa shabaha ya kushusha chini bei ya bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa na kwa njia hiyo kutoa pigo kwa Iran ambayo ilikuwa ikitegemeza sana pato la mafuta.   

Mwaka 1987 vita vya kulazimishwa vya Saddam Hussein dhidi ya Iran vilizusha hali ngumu na kuonesha mustakbali wenye giza. Wakati huo Ayatullah Hashemi Rafsanjani akiwa Spika na Kamanda wa Majeshi ya Iran alisema kuwa: Jambo muhimu zaidi kwa dunia ni kwamba kushindwa kwa Iraq kusitambuliwe kuwa ni ushindi wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Mwaka huo huo wa 1987 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 598 ambalo lilikubaliwa na Jamhuri ya Kiislamu lakini kwa masharti. Matatizo makubwa ya kiuchumi, kuingia moja kwa moja Marekani katika vita kwa maslahi ya dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein misaada ya kijeshi na zana za kisasa za kivita ya nchi za Magharibi na Russia kwa utawala wa Baath wa Iraq, ukiukaji wa sheria za kimataifa na jinai kubwa za kivita kama mashambulizi ya silaha za kemikali ya Saddam Hussein dhidi ya raia wa eneo la Halbcha viliwafanya viongozi wa Iran hususan Imam Khomeini kuelewa kwamba, kuendeleza vita hakutakua na maslahi. Kipindi hicho Ayatullah Rafsanjani alikuwa na mchango mkubwa katika kukubaliwa azimio nambari 598 na kukomeshwa vita vya kulazimisha vilivyoendelea kwa kipindi cha miaka minane. Vita hivyo vilimalizika baada ya jamii ya kimataifa kukiri rasmi kwamba Saddam Hussein ndiye aliyekuwa mchokozi dhidi ya Iran. Iran iliibuka mshindi katika vita hivyo ambavyo vilianzishwa kwa shabaha ya kusambaratisha mfumo mchanga wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini, lengo ambalo halikufikiwa. 

Ayatullah Rafsanjani

Suala la ujenzi na kukarabati wa uharibifu liosababishwa na vita lilipewa umuhimu na kipaumbele baada ya kumalizika vita hivyo. Katika medani hii pia Hashemi Rafsanjani alikuwa na mchango mkubwa. Hata hivyo kufariki dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini hapo mwaka 1989 kulisababisha ombwe mkubwa usioweza kufidika. 

Kwa kutilia maanani haiba kubwa aliyokuwa nayo hayati Imam Ruhullah Khomeini, maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu walidhani kwamba, kufariki dunia kwa shakhsia huyo ulikuwa mwisho wa uhai wa Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo kinyume kabisa na dhana hiyo, katika kipindi kifupi cha chini ya masaa 24 tu baada ya kufariki dunia Imam Khomeini, Baraza la Wataalamu lilimchagua Ayatulla Ali Khamenei kuwa Kiongozi Mkuu mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu, hatua ambayo uliwaacha bumbuazi watu wote. Rafsanjani kama kawaida alikuwa na mchango mkubwa katika uamuzi huo. Baada ya Ayatullah Khamenei kuchaguliwa kuwa kiongozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu, wananchi wa Iran walimchagua Ayatullah Hashemi Rafsanjani kuwa rais wa nchi katika vipindi viwili vya kati ya mwaka 1989 na 1997. Kipindi hiki cha miaka 8 kinajulikana hapa nchini kama kipindi cha ujenzi na ustawi. Ustawi wa pato ghafi la taifa katika kipindi hicho ulikuwa kwa asilimia 6.4. Nakisi ya asilimia 50 ya bajeti ya nchi mwaka 1988 ilitoweka na bajeti ya taifa ikaelekezwa zaidi katika masuala ya ujenzi. Sambamba na ustawi huo wa kiuchumi, kipato cha kila mwaka cha nchi kilipanda juu na hali ya bora ya kijamii ilionekana katika nyanja zote za afya, elimu na kadhalika.  

Ayatullah Ali Khamenei na Sheikh Rafsanjani

Mabwawa zaidi ya 60 ya kuhifadhi maji yalijengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi na ustawi wa mitandao wa kilimo cha umwagiliaji ulizidisha ustawi wa sekta ya kilimo na mazao ya sekta hiyo kwa asilimia karibu 6 kwa mwaka. Vilevile uzalishaji wa nishati wa vituo vya umeme nchini ambao ulikuwa chini ya megawati elfu 13 uliongezeka na kufikia megawati elfu 23, uzalishaji wa chuma, saruji na petrokemikali pia ulistawi kwa kiwango cha kuridhisha.

Baada ya kuongoza nchi kama rais kwa vipindi viwili mfululizo, Ayatullah Hashemi Rafsanjani aliteuliwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei kuwa Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran. Taasisi hii ni chombo kinachofanya kazi ya kutatua hitilafu zinazojitokeza kati ya Serikali na Bunge na kupanga sera na siasa kuu za nchi katika nyanja zote. Miongoni mwa kazi kubwa zilizofanywa na halmashauri hiyo katika kipindi cha uongozi wa Ayatullah Rafsanjani ni kubuni na kupasisha dira ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi mwaka 1404 Hijria Shamsia, jambo ambalo limepongezwa sana na wataalamu wa ndani na nje ya nchi.  

Kwa hakika jina la Hashemi Rafsanjani linaonekana katika matukio mbalimbali ya historia ya sasa ya Iran hususan katika kipindi cha miaka 50 uliyopita na alikuwa na mchango mkubwa katika kipindi hicho ambao unamuweka katika safu ya watu waliotengeneza historia mpya ya Iran kama Amir Kabiir.  

Katika kipindi chote cha harakati za mapambano ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rafsanjani alihudumia harakati hiyo kwa nguvu zake zote na alijisabilia kuhudumia wananchi na nchi yake baada ya ushindi Mapinduzi. Daima hakuondoka katika njia ya wastani na misimamo ya kati na kati katika vipindi vyote vya kutekeleza majukumu yake. Sifa hii ya kimaadili ndiyo iliyomfanya Hashemi Rafsanjani apewe heshima maalumu na wakosoaji na hata wapinzani wake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, ni wanasiasa wachache sana ambao huendelea kushikamana na maadili na mwenendo wa kiadilifu hata na wapinzani wake wakati anapokuwa katika kilele cha nguvu na madaraka makubwa. Kifo cha Rafsanjani pia kimeonesha kuwa ni mwanasiasa wa aina yake. Mahudhurio makubwa ya wananchi, watu mashuhuri na wanasiasa hata wapinzani na wakosoaji wa Rafsanjani katika mazishi yake ni kielelezo cha ushawishi wake mkubwa katika nyonyo za wananchi wa Iran. Zaidi ya watu milioni mbili na nusu wameshiriki katika mazishi ya mwanasiasa huyu. Mahudhurio haya makubwa katika kuaga mwili wa mwanamapinduzi huyu hayajawahi kushuhudiwa hapa nchini baada ya yale ya mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Ruhullah Khomeini. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.