Aug 07, 2023 14:04 UTC
  • Sura ya Adh-dhaariyaat, aya ya 47-53 (Darsa ya 958)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 958 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 51 ya Adh-Dhaariyaat. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 47 hadi 49 ambazo zinasema:

وَالسَّمَاءَ بَنَيْنَاهَا بِأَيْدٍ وَإِنَّا لَمُوسِعُونَ

Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio wenye kuzitanua.

وَالْأَرْضَ فَرَشْنَاهَا فَنِعْمَ الْمَاهِدُونَ

Na ardhi tumeitandaza; basi bora ya watandazaji ni Sisi!

وَمِن كُلِّ شَيْءٍ خَلَقْنَا زَوْجَيْنِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ

Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie.

Aya hizi zinazungumzia kwa mara nyingine qudra na uwezo mutlaki wa Allah SWT katika kuumba mbingu, ardhi na viumbe vingine ili kuondoa shaka na utata walionao wakanushaji wa maadi yaani ufufuo na kurejea viumbe kwa Mola Mwenyezi. Na kwa mintaarafu hiyo, aya hizi kwanza zinaashiria adhama ya mbingu na kusema: nyota mzionazo juu mbinguni pamoja na sayari na galaksi kadha wa kadha zilizosambaa, ambazo nyinyi hamuwezi kuona zilikoanzia wala zinakoishia, vyote hivyo ni ushahidi dhahiri na wa wazi unaothibitisha qudra na uwezo usio na ukomo wa Mola Muumba wa ulimwengu. Aya hizi zinaeleza kwa uwazi kwamba, Mwenyezi Mungu Jalla Jalaalu ameziumba mbingu na anaendelea kuzitandaza na kuzitanua. Ugunduzi uliofanywa na wanasayansi, nao pia umedhihirisha kuwa dunia haiko katika hali thabiti ya kutobadilika, bali nayo pia inapanuka na kutandawaa kwa kasi. Kwa mujibu wa nadharia hii, nyota zilizoko kwenye galaksi moja zinasambaa kwa kasi kutoka katikati ya kilipo kitovu cha galaksi hiyo. Na tab’an wanasayansi wanaamini kwamba, kwa kuwepo mpanuko, lazima ulimwengu huu ulikuwa na mahali ulipoanzia ukiwa katika sura ya mfinyiko na kisha ukaanza kutanuka hadi ukafikia kwenye hali ya sasa. Aya zinasema, si mbingu pekee zilizoko juu yenu, bali hata ardhi iliyoko chini ya miguu yenu, Allah SWT ameiumba kwa namna hiyohiyo pia, kwa kuutanua uwanda wake ili ardhi hiyo iweze kutumika kwa ajili ya maskani na makazi yenu, shughuli za kilimo, ufugaji na mahitaji yenu mengine. Kwa maneno mengine, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametayarisha na kuwepesisha mazingira ya kuishi katika sayari ya dunia kwa ajili ya wanadamu ambao ni wageni wake Yeye Mola katika sayari hii. Ili kutoa ufafanuzi zaidi wa nukta hii tuangalie mfano ufuatao kuhusu nafasi ya hewa katika kuvifanya viumbe viendelee kubaki hai katika sayari hii ya dunia. Hewa, ambayo imesambaa katika ardhi yote, ndiyo inayobeba na kuhifadhi joto la jua. Kwa hivyo hewa hiyo ndiyo inayozuia ardhi isiwe baridi kupindukia wakati wa usiku au isiwe na joto la kupita kiasi wakati wa mchana. Lakini mbali na hayo, hewa iliyopo kwenye anga ya ardhi ni mithili ya ngao imara na madhubuti inayoikinga ardhi pamoja na wakazi wake na hujuma za mawe ya angani, kwa namna ambayo, mara tu mawe hayo yanapokumbana na hewa, huunguzwa na kuteketezwa. Baada ya kuzungumzia uumbaji wa mbingu na ardhi, aya tulizosoma zinawazungumzia viumbe mbalimbali. Mwenyezi Mungu SWT ameweka kanuni ya jozi katika uumbaji wa vitu vyote ili kila kiumbe kiendelee kuwepo na kukifanya kizazi cha mwanadamu na viumbe vinginevyo viendelee kuwepo kwa kufuata utaratibu wa kimaumbile. Kuyazingatia yote haya tuliyoyaeleza kunatosha kumfanya mwanadamu aache inadi na ukaidi wake na kuamini qudra na uwezo wa Allah TWT wa kusimamisha Kiyama. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ulimwengu haujatulia na kubaki katika hali moja tu, bali unapanuka na uko mwendoni muda wote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kanuni ya jozi haiwahusu wanadamu, wanyama na mimea peke yao, bali inajumuisha pia hata vitu visivyo na uhai. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Qur’ani si kitabu cha kutoa elimu ya vitu vya ulimwengu wa maumbile, lakini ili kuondoa ukungu wa ujinga na mghafala uliotanda kwenye macho ya mwanadamu, kinaashiria pia baadhi ya kanuni zinazotawala ulimwengu huo, ambazo ni ishara na alama za qudra na uwezo wa Muumba wake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 50 na 51 ambazo zinasema:

فَفِرُّوا إِلَى اللَّهِ ۖ إِنِّي لَكُم مِّنْهُ نَذِيرٌ مُّبِينٌ

Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi kwenu ni mwonyaji waziwazi nitokae Kwake.

وَلَا تَجْعَلُوا مَعَ اللَّهِ إِلَٰهًا آخَرَ ۖ إِنِّي لَكُم مِّنْهُ نَذِيرٌ مُّبِينٌ

Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, hakika mimi kwenu ni mwonyaji waziwazi nitokae Kwake.

Aya hizi zinaendeleza yaliyozungumziwa katika aya zilizopita kwa kumtaka Bwana Mtume SAW awape onyo na indhari washirikina na makafiri ya kwamba: badala ya kuitakidi kuwepo kwa mshirika wa Allah katika mfumo wa uumbaji au uendeshaji wa masuala ya ulimwengu, achaneni na masanamu yenu ya mawe na vitu vingine mnavyojiwazia nafsini mwenu kuwa ni miungu na waabudiwa, na badala yake muelekeeni Allah SWT ili muifikie njia sahihi ya maisha na kuepukana na mwisho mbaya na wa kukhasirika kutokana na shirki na ukafiri. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, si mali na madaraka, wala jamaa na marafiki wanaoweza kwa namna yoyote ile kuwa egemeo la uhakika la kulitegemea mtu. Egemeo na kimbilio pekee na la uhakika kwa mwanadamu ni Allah SWT. Na ndio maana tuna kila sababu ya kutawakali na kumtegemea Yeye tu peke yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mbali ya Mitume kuwa na wajibu wa kuwalingania watu Tauhidi na kuwaongoza katika kufanya mema na ya kheri, wana jukumu pia la kuwapa indhari na kuwatahadharisha na mwisho mbaya wa fikra na imani potofu na matendo maovu na machafu wanayofanya.

Darsa yetu ya leo inaihitimishwa na aya ya 52 na 53 za sura yetu ya Adh-Dhaariyaat ambazo zinasema:

كَذَٰلِكَ مَا أَتَى الَّذِينَ مِن قَبْلِهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا قَالُوا سَاحِرٌ أَوْ مَجْنُونٌ

Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.

 أَتَوَاصَوْا بِهِ ۚ بَلْ هُمْ قَوْمٌ طَاغُونَ 

Je! Wameambizana kwa haya? (La!) Bali wao ni watu waovu.

Katika aya tulizosoma kwenye darsa iliyopita tuliona jinsi Firauni alivyotumia tuhuma za kumwita Nabii Musa AS mchawi na mwendawazimu ili kuwakimbiza na kuwafanya watu wajiweke mbali na Mtume huyo wa Allah. Aya hizi zinasema, si Musa AS peke yake aliyevurumiziwa tuhuma za aina hiyo, lakini katika zama zote za historia, Mitume wote wa Allah waliandamwa na tuhuma kama hizo. Mwenendo huo ulizoeleka na kuenea katika kaumu mbalimbali, utadhani kila kaumu moja na nyingine zilikuwa zimeambizana ziendeleze na wala zisiache kueneza tuhuma hizo. Kwa hakika, hulka ya inadi na ukaidi wa kuikataa haki ndiyo iliyopelekea watu hao kufanya mambo hayo kwa lengo la kuizima sauti ya watu wa haki. Na pale waliposhindwa kuwaondoa Mitume wenyewe na kuuzuia wito wao ndipo walipotumia mbinu hiyo ya kuwachafulia na kuwaharibia majina na heshima zao kwa kuwabambikizia tuhuma za uchawi na wendawazimu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tusihofu wala tusirudi nyuma kwa sababu ya matusi na kusemwa vibaya na wapinzani, kwani Mitume wa Mwenyezi Mungu nao pia walikuwa daima wakizushiwa kila uongo na kuandamwa na kila aina ya tuhuma. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa, uasi na kuchupa mipaka ya utu na ya udadisi wa kuijua haki na ukweli humfanya mtu asimame dhidi ya Mitume wa Allah mpaka kufika hadi ya kuwa tayari kuwaita waja hao wateule wachawi au wendawazimu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 958 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags