Sep 17, 2023 16:22 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (80)

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu. Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Ayatullah Seyyid Hussein Qadhi.

 

Tulisema kuwa, tangu akiwa mdogo, alianza safari ya kulea nafsi kwa mujibu wa elimu ya irfani (kumtambua Mwenyezi Mungu) alipokuwa akisoma kwa baba yake Aidha tulibainisha kwamba, mwanazuoni huyo alijifunga mno na suala la kusali Sala za usiku. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alikuwa akiwanasihi na kuwasisitizia sana wanafunzi wake juu ya suala la kushikamana na Sala za usiku. Alikuwa akiwaambia: Kama mnataka dunia salini Sala za usiku, kama mnataka akhera basi salini pia Sala za usiku.  Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 80 ya mfululizo huu kitatupia jicho kwa mukhtasari historia, maisha na harakati za Agha Bozorg Tehran. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

 

Katika mwaka wa 1293 Hijria, wiki moja kabla ya kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume (saww), alizaliwa mtoto katika familia ya mfanyabiashara wa Tehran. Baba yake ni Haj Molla Ali, ambaye alikuwa miongoni mwa wahisani na watu wenye kusaidia watu wengine katika mji wa Tehran. Mama yake anatokana na masharifu Kialavi. Babu yake ni Molla Mohsen, ambaye alikuwa mmiliki wa kituo cha kwanza cha uchapishaji nchini Iran. Mullah Ali alikusudia kumpa mtoto wake jina la baba yake yaani "Mohsen", lakini siku ya kuzaliwa kwake iliposadifiana na kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Mtume (saww), alikata shauri kumpa jina la "Muhammad Mohsin".

Ilikuwa ni ada na mazoea miongoni mwa watu wa Tehran katika zama hizo kumwita kwa jina la Agha Bozorg, mtoto wa kiume ambaye jina lake linafanana na jina la babu mkubwa wa familia. Ni kutokana na ada hiyo ndio maana Muhammad Muhsin pia akapewa lakabu ya Agha Begorz, (yenye maana ya Bwana Mkubwa) ingawa kwa hakika baadaye aliondokea kuwa Bwana mkubwa kwa maana halisi ya neno.

Mohammad Mohsin alianza kujifunza Quran nyumbani alipokuwa na umri wa miaka minne au mitano tu hivi. Alijifunza alfabeti na sura ndogo ndogo za Qur'ani kabla ya kuanza rasmi masomo yake. Akiwa na umri wa miaka 7 Muhammad Muhsin akaenda shule ambazo wakati huo zikifahamika kama Maktabkhaneh. Hata hivyo, hakuwa na shauku sana ya kuendelea na masomo yake. Alipenda kufuatilia kazi na taaluma ya mababu zake ya kushughulika na biashara. Mohammad Mohsin baadaye aliandika katika kumbukumbu zake:

"Nilikuwa nikicheza nyumbani hadi nilipokuwa na umri wa miaka sita. Nakumbuka nilitengeneza duka moja na niliikuwa nikiweka humo bidhaa za dukani, manukato, mizani ... sikuwa na hamu kabisa ya kusoma. Nilitaka kuwa mfanyabiashara."

 

Muhammad Muhsin alijishughulisha na kazi ya biashara kwa muda fulani akiwa na kaka yake, lakini haukupita muda akagundua kuwa hakuwa mwafaka kwa kazi hii, hivyo akaachana nayo na kuanza kwenda shule tena. Baba yake alifurahishwa na uamuzi wake na alimtia moyo sana. Msaada wa baba yake ulimfanya ajivunie kuvaa nguo za wanazuoni wa kidini na kilemba akiwa na umri wa miaka kumi. Ni katika miaka hii ambapo alifahamika kwa jina la Sheikh Agha Bozorg.

Sheikh huyu aliyekuwa na umri wa miaka 10 aliendelea kusoma katika shule za Tehran kwa muda wa miaka 12 mingine na kufanikiwa kuwa mahiri katika elimu mbalimbali kama fasihi ya lugha, mantiki, fiq'h, Usul na kadhalika.

Wakati wa masomo yake, Agha Bozorg alikuwa akipenda sana kuwa katika mazingira ya maktaba na moja ya mambo mazuri aliyofanya katika miaka hiyo ilikuwa kunakili baadhi ya vitabu muhimu na vyenye itibari. Hii leo, baadhi ya miswada ya Sheikh huyu kijana inapamba maktaba na hazina za kielimu za Uislamu, nakala ambazo zinaonyesha vizuri juhudi zisizokoma za Agha Bozorg katika njia ya elimu na kujifunza, na bila shaka, zinaonyesha pia dhuku, shauku na mwandiko wake mzuri na maridadi.

Mnamo mwaka 1313 Hijria Agha Bozorg alikwenda Iraq pamoja na kaka yake kwa ajili ya kufanya ziara na akaamua kubakia huko milele katika mji wa Najaf. Hata hivyo sisitizo la wale waliokuwa karibu naye la kumtaka kurejea Tehran lilisababisha utekelezaji wa uamuzi huo auakhirishe kwa miaka mingine miwili. Hatimaye, mwaka 1315 Hijria, Sheikh Agha Bozorg aliingia Najaf akiwa na umri wa miaka ishirini na mbili kwa minajili ya kuendelea na elimu yake ya juu. Akiwa katika mji wa Najaf Muhammad Muhsin alishiriki darsa na masomo ya shakhsia wengi wakubwa akiwemo Mirzaei Shirazi wa pili (Ayatullah Muhammad Taqi Shirazi), Akhund Khorasani na Muhaddith Nuri.

 

Muhaddith Nouri, ambaye yeye mwenyewe anahesabiwa kuwa mmoja wa wasomi wakubwa na mashuhuri zaidi wa Kishia katika elimu ya hadithi, alikuwa mtu wa kwanza kutoa ruhusa na idhini kwa Sheikh Agha Bezorg Tehrani ya kunukuu hadithi, na hii ni katika hali ambayo Agha Bezorg alikuwa angali katika rika la ujana. Ukweli ni kwamba, baada ya Muhaddith Nouri, msomi maarufu wa Kishia katika uga wa elimu ya hadithi ni Sheikh Agha Bozorg Tehrani.

 Juhudi zake zisizokoma zilisababisha baadhi ya wanavyuoni wakubwa wa Kisunni pamoja na wanavyuoni wa Shia kumpa ruhusa ya kunukuuu hadithi. Sheikh Mohammad Ali Azhari Makki, mmoja wa wanazuoni wa madhehebu ya Maliki, Sheikh Abdul Wahab Shafi'i na Sheikh Abdul Rahman Alish Hanafi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar nchini Misri, ni miongoni mwa wanazuoni waliompa idhini Agha Bozorg Tehrani ya kunukuu hadithi.

 

Mwanazuoni huyu hakuwa nyuma pia katika uga wa uandishi wa vitabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha Agha Bozorg ni al-Dharia ila Tasanif al-Shia". Katika kuandika kitabu hiki alilazimika kufanya safari ndefu na kutembelea maktaba mbalimbali za Iraq, Iran, Syria, Palestina, Misri na Hijaz.

Hatimaye mnamo mwaka 1354 Hijria (1935 Miladia), juzuu ya kwanza ya kitabu cha Sheikh Agha Bozor Tehrani ilikuwa tayari kuchapishwa, na alijaribu kuanzisha kituo cha uchapaji huko Najaf, lakini serikali ya Iraq wakati huo ilizuia hilo kwa sababu mbalimbali. Miezi sita baada ya tukio hili, juzuu ya kwanza ya kitabu "Al-Dhariyah ilaa al-Tsanif al-Shi'a" ilichapishwa huko Iraq.

Sheikh Agha Bozorg Tehrani aliaga dunia siku ya Ijumaa, tarehe 13 Dhu al-Hijja, 1389 Hijria akiwa na umri wa miaka 96. Mmoja wa wanazuoni wa Najaf aliyeitwa "Ayatullah Madani", ambaye baadaye alijulikana kwa jina la "Shahidi wa Mihrab", aliukosha na kuukafini mwili wake na kisha kuzikwa huko Najaf Iraq.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati hivyo sina budi kukomea hapa kwa juma hili. Hata hivyo kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi kama ambavyo pia kumalizika kwa muda wa kipindi hiki sio mwisho wa mfululizo huu bali ndio mwanzo wa harakati za kukuandalieni kipindi kingine, basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh