Sep 18, 2023 10:20 UTC
  • Uliwengu wa Michezo, Sep 18

Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia.

Futsal; Iran yasalimu amri

Timu ya taifa ya futsal ya Iran imeibuka mshindi wa pili kwenye Ligi ya Mataifa ya Futsal ya Brazil. Hii ni baada ya kukubali kichapo cha magoli 4-2 kwenye fainali ya mashindano hayo yanayofahamika kama Copa das Nacoes de Futsal iliyopigwa katika Ukumbi wa Sorocaba, mjini São Paulo. Mabao ya Iran kwenye mchuano huo yalifungwa na Mojtaba Parsapour na Saeid Ahmadabbasi kwenye fainali hiyo mbele ya mashabiki karibu 5,000.

Iran ilitinga fainali baada ya kuzibomoa Paraguay mabao 2-1, Colombia magoli 2-0 na Japan 2-0. Paraguay imemaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuichabanga Japan mabao 7-3.

Uzani mzito; Iran yaibuka ya 3 IWF

Timu ya taifa ya mchezo wa kunyanyua uzani mzito ya Iran imeibuka ya tatu katika mashindano ya mabingwa wa dunia wa mchezo huo ya IWF nchini Saudi Arabia. Iran imefunga orodha ya tatu bora kwenye mashindano hayo baada ya kuzoa alama 468. Mir-Mostafa Javadi aliipa Iran medali mbili za dhahabu katika katogoria ya kilo 89, huku Ali Davoudi akitunukiwa medali ya shaba katika safu ya uzani mzito kwenye mashindano hayo yaliyofunga pazia lake Jumapili.

Huku hayo yakiarifiwa, mwanamieleka wa Iran, Amir Hossein Zare ametwaa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya Mieleka huko Belgrade nchini Serbia. Zare wa mielkeka mtindo wa kujiachia (freestyle), aliibuka kidedea baada ya kumzidia nguvu na maarifa hasimu wake Geno Petriashvili kutoka Georgia, na kumzima kwa alama 11-0 katika fainali ya wanamieleka wenye kilo 125.

Soka; Iran yainyuka Angola

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliitandika Angola mabao 4 kwa sifuri katika mechi ya kirafiki iliyochezwa katika dimba la Azadi mjini Tehran. Mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa ilichezwa Jumanne iliyopita katika mlolongo wa mechi za kujipima nguvu katika kalenda ya FIFA (FIDA DAY). Vijana wa mkufunzi Amir Ghalenoei waliendeleza wimbi la ushindi katika mechi za kujipima nguvu, ambapo wiki iliyopita waliishinda timu ya Bulgaria bao 1 kwa yai. Katika mechi hiyo ya Jumanne dhidi ya timu ya Kiafrika ya Angola iliyochezwa bila ya kuhudhuriwa na mashabiki, timu ya taifa ya soka ya Iran al-Maarufu Team Melli ilitawala mchezo huo karibu katika sekta zote. Nyota wa mchezo huo alikuwa mshambuliaji Mehdi Taremi anayechezea Porto ya Ureno. Taremi alipachika mabao mawili huku mabao mengine ya timu ya soka ya taifa ya Iran yakitiwa wavuni na Sadeqi Muharrami na Shahriyry Moghalou.

Iran yainyuka Angola 4-0

Huku hayo ya yakiarifiwa, Rais wa Shirikisho la Soka la Iran (IRIFF) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia mjini Tehran, ambapo wamejadili njia za kupanua uhusiano wa kimichezo hasa kandanda baina ya mataifa haya mawili. Mehdi Taj, Rais wa Shirikisho la Soka la Iran Jumapili alikutana na Balozi Abdullah bin Saud al-Anzi wa Saudia hapa Tehran, kuelekea mchuano baina ya klabu ya soka ya Persepolis na Iran na Al-Nassr ya Saudia, utakaopigwa Jumanne hii katika Uwanja wa Azadi hapa mjini Tehran, ukiwa ni mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Asia ya AFC.

Raga: Kenya yang'aa

Kenya ndiye bingwa wa Kombe la Afrika la raga ya wachezaji saba kila upande baada ya kuigaragaza Afrika Kusini kwa alama 17-12 kwenye fainali ya kukata na shoka siku ya Jumapili huko Harare, mji mkuu wa Zimbabwe. Patrick Odongo aliiweka Shujaa ya Kenya kifua mbele na pia kufanya mambo yawe suluhu bin suluhu, kabla ya miguso ya John Okoth kuipa timu hiyo ya Afrika Mashariki ubingwa.

Uganda imetunukiwa medali ya fedha, baada ya kuigaragaza Zimbabwe 24 kwa 12 kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu. Kwa ushindi huo, Shujaa ya Kenya imejikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Paris itakayofanyika nchini Ufaransa mwaka ujao 2024. Hata hivyo, wenzao wa kike, Kenya Lionesses walipokea kichapo kikali cha pointi 77-12 Jumamosi mikononi mwa wenyeji Afrika Kusini katika mechi ya kirafiki ya kujiandaa kwa mashindano ya dunia ya daraja la tatu (WXV3) yatakayofanyika mwezi ujao wa Oktoba.

Soka: Yanga yajongea makundi

Klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania imejongea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuigaraza Al-Merrikh ya Sudan mabao 2-0. Mabao ya Yanga yalifumwa wavuni na washambuliaji Kennedy Musonda na Clement Mzize kwenye mchuano huo wa wikendi dhidi ya Waarabu wa Sudan. Yanga imeanza ugenini kwenye raundi hii ya pili huku wenyeji wao, Al Merrikh ya Sudan ikiutumia Uwanja wa Pele, Kigali Rwanda kama uwanja wa nyumbani, kutokana na mchafuko yaliyopo nchini kwao. Mechi ya marudiano ya kuwania hatua ya makundi ya Ligi ya Mabigwa Afrika itapigwa Septemba 30 katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam. Huku hayo yakijiri, watani wao wa jadi, klabu ya Simba iliambulia sare ya mabao 2-2 ilipovaana na Power Dynamos ya Zambia kwenye mechi nyingine ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mabao ya Wekundu wa Msimbazi yalifungwa na Clatous Chama huku ya Dynamos yakifungwa na Joshua Mutale na Aaron Katebe. Simba imeanzia hatua ya pili ya mashindano hayo na hivyo inasubiri mchezo wa marudiano utakaopigwa Oktoba Mosi, ili kujihakikishia kutinga hatua ya makundi.

Riadha: Kenya yazoa medali Ligi ya Almasi

Wanariadha wa Kenya wameng'aa na kuzoa medali si haba katika mbio za Ligi ya Almasi. Nyota wa riadha, Faith Kipyegon amehifadhi taji lake kwenye mbio za mita 1500 kwenye mashindano hayo ya Diamond League, baada ya kuibuka kidedea kwenye fainali za mbio hizo Jumamosi huko Oregon nchini Marekani. Kipyegon ambaye katika miezi ya hivi karibuni amekuwa moto wa kuotea mbali kwenye mbio hizo, aliibuka mshindi wa Diamond League kwa kutumia dakika 3 sekunde 50.72.

Raia wa Ethiopia, Derive Welteji aliibuka wa pili, huku Laura Muir wa Uingereza akifunga orodha ya tatu bora. Mkenya Ferdinand Omanyala ameingia kwenye daftari ya kumbukumbu baada ya kuibuka mshindi wa tatu wa mashindano hayo kwenye mbio za mita 100. Omanyala ameitunukiwa medali ya fedha kwenye Ligi ya Almasi siku ya Jumamosi kwa kuibuka wa tatu, nyuma ya Mmarekani Noah Lyles na Christian Coleman. Wakati huohuo, Mkenya Simon Koech ametwaa ubingwa kwenye mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji, na kutunukiwa dola 30,000 za Marekani. Emmanuel Wanyonyi ameipa Kenya dhahabu nyingine siku ya Jumapili katika mbio za mita 800. Muethiopia Gudaf Tsegey siku ya Jumapili aliibuka mshindi na kuvunja rekodi ya Mkenya Faith Kipyegon kwa sekunde 5 kwenye mbio za mita 5000. Alimaliza mbio hizo za Ligi ya Almasi kwa kutumia dakika 14 na sekunde 00.21.

…………………TAMATI……………