Sep 28, 2023 03:03 UTC
  • Alkhamisi tarehe 28 Septemba, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1445 Hijria sawa na Septemba 28, 2023.

Siku kama ya leo miaka 1498 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW.

Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani.

Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu. 

Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina.

Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka na kuelekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume. 

Msikiti wa Quba

Siku kama ya leo miaka 1204 iliyopita, inayosadifiana na 12 Rabiul Awwal 241 Hijria, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo.

Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kujipatia elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal amesafiri katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW.

Ahmad bin Hanbal ni muasisi wa Madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na ameacha kitabu mashuhuri cha hadithi, kiitwacho Musnad.   

Miaka 128 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Louis Pasteur, tabibu na mwanakemia wa Kifaransa. Akiwa shuleni alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu. 

Louis Pasteur

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, alifariki dunia rais wa zamani wa Misri, Gamal Abdel Nasser.

Abdel Nasser alizaliwa mwaka 1916. Alishiriki katika vita vya kwanza vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel hapo mwaka 1948 na kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa kushirikiana na Jenerali Najib, dhidi ya Mfalme Faruq 1952 na kuung'oa utawala wa kisultani nchini humo. Miaka miwili baadaye Gamal Abdel Nasser alimuondoa madarakani mshirika wake Jenerali Najib na kuchukua jukumu la kuiongoza Misri sanjari na kufanya juhudi za marekebisho, kupambana na ukoloni na utawala ghasibu wa Israel. Mwaka 1956 aliutaifisha mfereji wa Suez na kuufanya kuwa mali ya Misri, hatua iliyozifanya nchi za Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuishambulia Misri.

Hatua ya viongozi wa Misri ya kujibu hujuma hiyo, iliongeza umaarufu wa Abdel Nasser nchini Misri na ulimwenguni kwa ujumla. 

Gamal Abdel Nasser

Katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio likiutaka utawala wa Kizayuni wa Israel kukomesha operesheni ya kuchimba mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Azimio hilo lililaani uchimbaji huo wa mashimo kinyume cha sheria chini ya eneo hilo takatifu. Hata hivyo upinzani wa Marekani ulipelekea kuondolewa kipengee hicho katika azimio hilo.

Uchimbaji huo wa mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa na utawala huo ghasibu, ulizusha machafuko ya umwagaji damu mkubwa hapo tarehe 23 Septemba 1996 kati ya askari wa Israel na Wapalestina ambapo askari hao waliua na kujeruhi mamia ya Wapalestina. 

Msikiti wa al Aqsa

Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita Intifadha ya wananchi wa Palestina kwa mara nyingine tena ilipamba moto.

Hatua ya Ariel Sharon kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha Likud na mhusika mkuu wa mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika kambi za Sabra na Shatila ya kuingia katika Msikiti wa al Aqswa na kuuvunjia heshima msikiti huo mtukufu, iliwatia hasira Wapalestina na kuwafanya waanzishe maandamano na mapambano makubwa dhidi ya utawala huo wa Israel. 

Intifadha ya Palestina

 

Tags