Sep 30, 2023 12:23 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (81)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 81 ya mfululizo huu kitamzungumzia Ayatullah Muhammad Ali Shahabadi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Mnamo mwaka 1292 Hijria (1875 Miladia) katika nyumba ya Ayatullah Muhammad Javad Bidabadi, mmoja wa wanachuoni mashuhuri na wanamapambano wa Isfahan, Iran alizaliwa mtoto mwingine wa kiume ambaye alipewa jina la Muhammad Ali.

Hakuwa mtoto wa kwanza wa kiume katika nyumba hiyo, kwani alikuwa na kaka kadhaa wa kuzaliwa. Kutokana na kuwa, baba na kaka mkubwa wa Muhammad Ali wote walikuwa wanazuoni na mafaqihi, alijifunza elimu ya msingi na kama ambavyo alisoma kwao sehemu ya masomo ya awali ya dini. Huko Isfahan, Muhammad Ali alikuwa na walimu wengi wa elimu za akili na nakili, lakini mapambano ya baba yake dhidi ya wafalme wa Qajar yalimfanya Naser al-Din Shah kumpeleka uhamishoni Tehran yeye pamoja na familia yake. Mhammad Ali alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili alipoingia Tehran na kuendelea na masomo yake katika Hawza (vyuo vya kidini) na shule za Tehran. Alifikia daraja la Ijtihad akiwa na umri wa miaka kumi na minane na baada ya hapo pia alijishughulisha na kazi ya ualimu sambamba na kujiendeleza zaidi kielimu.

Alipofikisha umri wa miaka ishirini na minane, alikwenda kwenye Hawza (vyuo vya kidini) huko Samarra na Najaf Iraq na kuhudhuria darsa na masomo ya maustadhi wawili wakubwa katika zama hizo wa elimu za dini yaani Akhund Khorasani na Muhammad Taqi Shirazi (Mirzei Shirazi wa pili). Mirzai Shirazi wa Pili kutokana na umakini wake wa kimtazamo aliokuwa nao pamoja na unyeti wake maalumu katika masuala ya dini alikuwa mkali sana katika kutoa idhini ya Ijtihad kwa watu, lakini Muhammad Ali Bidabadi alikuwa mmoja wa watu sita waliofanikiwa kupata idhini ya Ijtihad kutoka kwa Mirzai II.

Ayatullah Mohammad Ali Bidabadi alirejea Tehran baada ya miaka minane kwa ombi la wananchi. Alikaa katika kitongoji kilichoitwa "Shah Abad" wakati huo, na kwa sababu hii watu wa Tehran walimwita Ayatullah Shahabadi. Ilikuwa katika kipindi hiki ambapo shughuli zake za kielimu, kidini na kisiasa ziliingia katika kipindi na duru mpya. Kuwasili kwa Ayatullah Shahabadi mjini Tehran kulisadifiana na mwisho wa kipindi cha utawala wa ukoo wa Qajar na kuibuka kwa nasaba ya Pahlavi nchini Iran.

Ayatullah Shahabadi alikuwa mmoja wa wapinzani wakubwa wa Reza Khan. Kwa ujasiri maalumu ambao haukuonekana kwa wengine, alitangaza upinzani wake katika hali yoyote na alikuwa akiwataka watu wengine kukabiliana na Reza Khan Pahlavi. Baada ya Reza Khan kushika hatamu za uongozi kwa usaidizi wa Uingereza, aliupinga hadharani Uislamu na madhihirisho yake. Alijaribu kuondoa alama na madhihirisho haya moja baada ya jingine kutoka katikak uso wa jamii.

Akiwa na nia ya kufikia lengo hili, aliamuru kupiga marufu hijabu. Aidha akitumia kisingizio cha kuweko vazi rasmi la watu wa Iran, pia alipiga marufuku uvaaji wa nguo za kidini yaani majoho na vilemba. Upinzani wa Reza Khan kwa Uislamu haukuishia hapo, kwani alikataza pia kufanyika kwa mikusanyiko ya maombolezo Imamu wa mashahidi, Imamu Hussein (a.s.). Aidha alikwenda mbali zaidi na kwa ujeuri kamili alianzisha vikundi vya unenguaji na furaha katika siku zote za mwezi wa Muharram. Si hayo tu, bali Reza Khan alipiga marufuku hata kuswali misikitini na alikuwa akiwakataza wanazuoni na Maulamaa kutoa hotuba. Katika mazingira haya ya ukandamizaji wa kisiasa nchini Iran, Ayatullah Shahabadi aliwaalika wanazuoni ili wafanye mgomo wa kuketi, lakini kutokana na mashinikizo ya utawala, ni wanachuoni wawili tu waliojiunga naye. Hata hivyo, Ayatullah Shahabadi akiwa na lengo la kutekeleza jukumu lake la kisheria alifanya mgomo wa kuketi katika haram ya Abdul Adhim al-Hassani katika mji wa Rey. Kila siku alitoa hotuba dhidi ya Shah na matendo yake ya kupinga dini. Sentensi yake mashuhuri ilikuwa: Reza Khan ni kibaraka wa Uingereza na lengo lake ni kuhakikisha Qur’ani na Uislamu vinatoweka nchini Iran.

… Ninaitangazia dunia kwamba, kama hamtachukua hatua, khabithi huyu atautokomeza Uislamu.

Mgomo huu wa kuketi ulidumu kwa muda wa miezi kumi na tano na hatimaye kumalizika kwa upatanishi wa wanazuoni wengine, lakini huu haukuwa mwisho wa mapambano ya shakhsia huyu mkubwa. Katika kipindi ambacho Maulamaa wengi walilazimika kuacha mavazi ya wanazuoni kutokana na mashinikizo ya utawala wa Reza Khan, Ayatullah Shahabadi aliwavisha wanawe saba mavazi haya ya kidini na ya wanazuoni. Kamwe hakuheshimu marufuku ya kusimamisha Sala msikitini, kutoa hotuba, pamoja na marufuku ya kufanya maombolezo katika siku za Muharram, na alikuwa akifanya mikutano hii kila mara nyumbani kwake au katika Msikiti Mkuu wa Tehran.

Siku moja maajenti wa serikali waliiba mimbari ya Msikiti wa Jamia ili kuvuruga mkusanyiko wake wa hotuba. Kuanzia hapo Ayatullah Shahabadi alitoa hotuba akiwa amesimama na kusema: "Ninasema nikiwa nimesimama ili wajue kwamba mimbari haisemi, ikiwa wanataka majlisi hii isifanyike basi, waniibe mimi, sio mimbari." Makabiliano ya mwanafaqihi huyu mwanamapambano na makachero wa Reza Shah yalikuwa ya ushujaa sana, lakini ujasiri na ushujaa wote huu ulitoka wapi na vipi ulikuweko katika uwepo wa Ayatullah Shahabadi?!! Ujasiri huo unaweza tu kuwa ni matokeo ya jambo moja; "Hofu ya Mungu". Yule anayemchukulia Muumba Mmoja kuwa ndiye mwenye uwezo pekee wa dunia na kuona mwisho wa mambo yote mikononi Mwake, kamwe hatamuogopa yeyote au kitu chochote isipokuwa Yeye. Mtu wa namna hii humtumainia Mungu katika kufanya mambo na atasimama na kutekeleza shaari za kimungu bila hofu wala woga wowote.

Ili tusiwaogope wenye nguvu duniani haitoshi kuwa na ufahamu tu juu ya nguvu isiyo na kikomo ya Mwenyezi Mungu, bali kabla ya kuingia katika medani ya mapambano haya, tunapaswa kuwa tumepata ushindi katika jihadi kubwa yaani vita vya nafsi. Kila ambaye ataweza kukabiliana vyema na nafsi ya kihayawani na matakwa ya nafsi ya kimaada, basi ndivyo atakavyofanikiwa zaidi katika kutekeleza majukumu ya Mwenyezi Mungu. Kwa upande wake Ayatullah Shahabadi kwa mujibu wa ushuhuda wa waalimu na wanafunzi wake wengi alifanikiwa kushinda vita na mapambano dhidi ya nafsi. Ayatullah Shahabadi alikuwa na wanafunzi wengi katika elimu za Usul, fiqhi, tafsiri, irfan, mantiki na falsafa. Miongoni mwa wanafunzi wake mashuhuri zaidi ni Imam Khomeini (RA), Ayatullah Seyyid Shahabuddin Mar’ashi Najafi na Ayatullah Muhammad Thaqafi Tehrani.

Pia ameandika vitabu vingi katika nyanja mbambali. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Shadharat al-Maarif na Rashahat al-Maarif. Reza Shah ambaye alikuwa akiogopa hata kufanyika shughuli ya kuusindika mwili wa mwanazuoni huyu, wakati Ayatullah Shahabadi alipoaga dunia baada ya kuishi kwa miaka 77, aliamuru mwili wake usafirishwe kwa gari hadi katika Haram ya Shah Abdul-Adhim baada ya kufanyika usindikizaji wa mukhtasari katika soko la Tehran.

Lakini umati wa watu ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba haikubaki nafasi ya kutekeleza amri ya Reza Shah na hivyo usindikuizaji na shughuli ya kumuaga alimu huyo iliendelea hadi mahali pa kuzikwa kwake na waombolezaji wa Tehran, kana kwamba ujasiri wa mtu huyu mkuu ulikuwa umefufuka katika nyoyo zao. Tarehe 3 Safar mwaka 1369 Hijria mwafaka na 1949 ilikuwa siku ya huzuni mno kwa wapenzi wa Ayatullah Shahabadi.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki. Ninakuageni nikikutakieni kila la kheri. Wassalaam Aalykum Warahmatullah Wabarakaatuh.