Oct 03, 2023 15:32 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (30)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 30 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine ya Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 30.

الْحَذَرَ الْحَذَرَ فَوَاللَّهِ لَقَدْ سَتَرَ حَتَّى کَأَنَّهُ قَدْ غَفَرَ 

Tahadhar! Tahadhar! Naapa kwa Mwenyezi Mungu, anasitiri mno Allah mpaka ikadhaniwa amesamehe!

Moja ya sifa za kipekee za Mwenyezi Mungu ni kusitiri aibu za waja Wake. Sifa ya Allah ya Sattar al 'Uyub, maana yake ni kusitiri na kuweka kifuniko kwenye aibu na makosa ya viumbe wa Allah. Na sifa hii ina faida mbili: Kwanza, utu na heshima ya watu huhifadhiwa. Kuchunga shakhsia za watu ni sehemu ya kinga ya kuwazuia watu hao kuanguka katika madhambi. Sababu yake ni kwamba kama mtu atakuwa maarufu kwenye jamii kwa madhambi na mabaya yake, huwa haoni tena haja ya kufanya juhudi za kufuta madhambi yake bali huzidi kutumbukia kwenye dimbwi la madhambi na makosa yake. Lakini mara tu anapogundua kuwa madhambi yake yamesitiriwa na aibu zake zimehifadhiwa, hupata nguvu ya kuepuka kufanya tena madhambi hayo.

Faida ya pili ni kwamba, ni kuhifadhiwa asli ya uhuru na ikhtiyari ya mtu. Kwa maneno mengine, ikiwa mtu atafedheheshwa kwa kutenda kosa moja mara inayofuata hatofanya kosa hilo kwa kuona haya na kujificha. Lakini kama atastiriwa kuteleza kwake, huwa ni kama aliyepewa fursa nyingine ya kuacha madhambi, na kuna uwezekano mkubwa wa kuacha kabisa madhambi. Aidha mtu anapoacha kutenda madhambi kwa sababu ya kuogopa tu asikashifiwe na si kwa kumuogopa Allah, Muumba, ni kuacha madhambi kusikoweza kumfaidisha lolote mtu zaidi ya hivyo kuogopa watu wasimuone. 

Mwenyezi Mungu, kwa rehema Zake nyingi, humsitiri mja Wake na huwa hamkashifu kwa makosa anayofanya faraghani. Humpa fursa ya kujirudi na kutubu na humlindia heshima yake. Katika hikma hii ya 30 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anawaonya watenda madhambi wasijighururishwe na subira ya Mwenyezi Mungu mbele ya madhambi yao. Anasema:

الْحَذَرَ الْحَذَرَ فَوَاللَّهِ لَقَدْ سَتَرَ حَتَّى کَأَنَّهُ قَدْ غَفَرَ 

Tahadhar! Tahadhar! Naapa kwa Mwenyezi Mungu, anasitiri mno Allah mpaka ikadhaniwa amesamehe!

Katika hikma zake hizi zilizojaa busara, Imam Ali AS anatuonya kwamba tusijipumbaze kwa neema na rehema hiyo ya Mwenyezi Mungu ya kutusitiria madhambi yetu. Tuwe macho isije ikawa huko ni mtu kupuruziwa ili atumbukie zaidi na mwisho aadhibiwe kwa adhabu kali. Milango ya toba kwa wanaotenda madhambi iko wazi lakini vile vile hakuna yeyote mwenye yakini na mwisho wa maisha yake, hivyo cha busara ni mtu kufanya haraka sana kutubu na kurejea kwa Mola wake kila anapoteleza na kufanya makosa. Ni wajibu wa kila mtu kushukuru neema anazopewa na Mwenyezi Mungu. Mtu anapofanya kiburi cha kutoshukuru neema huwa pole pole anaelekea kwenye shimo la ghururi lisilo na kurudi nyuma na mwisho wake ni adhabu kali. Tab'an si kila kuwa na neema ni aina fulani ya kupuruziwa ingawa kila kitu ni mtihani lakini neema inapotumiwa vizuri huwa njia ya kumwokoa mwanadamu duniani na Akhera. 

Vilevile tunaweza kupata somo kutoka kwa maneno hayo ya hikma ya Imam Ali ASla kwamba tunapaswa kuwasitiria watu aibu zao. Isiwe mtu ukisikia tu mtu fulani amefanya kosa, uwe kiranja wa kumchafulia jina na kumkashifu mbele ya wengine na kumfungia kabisa njia zote za kutubu. Tunapaswa kujipamba kwa sifa hiyo ya Allah ya kuwa wingi wa kusitiriana aibu zetu. 

Tags