Oct 22, 2023 13:15 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (84)

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Ayatullah Seyyid Hussein Qadhi. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 84 ya mfululizo huu kitamzungumzia Sayyid Hussein Borujerdi, alimu na mwanazuoni mashuhuri. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Mnamo mwaka 1874 katika mji wa kihistoria wa Borujerd, alizaliwa katika familia ambayo ukoo wake unarudi kwa Imam Hassan (AS), mtoto ambaye alipewa jina la ni Hussein. Jina la baba yake Hussein ni Seyed Ali na alikuwa akijishughulisha na kilimo, lakini alipendelea sana mtoto wake mpendwa kusoma dini. Seyyed Hussein alienda shule akiwa na umri wa miaka saba, na ilikuwa wakati huu kwamba kipaji chake katika kujifunza elimu kilichanua na kudhihirika.

Haikuwa ajabu kwake kuwa na fikra za namna hiyo kwa sababu alikuwa mrithi wa familia ambayo ilikuwa na wasomi na waheshimiwa wengi. Babu yake wa tano alikuwa Seyyed Mohammad Tabatabai, mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa kidini na katika ndugu na jamaa wa Mohammad Bagher Majlisi. Seyyed Mehdi Bahrul Ulum ni mtu mwingine mashuhuri wa familia yake. Baba yake alimpeleka Seyed Hussein katika mji wa Boroujerd na alisoma katika Shule ya Noorbakhsh, shule ambayo iliachwa kama kumbukumbu na mababu zake wa upande wa mama.

 

Alikuwa na umri wa miaka kumi na minane wakati alipoenda Isfahan na kuendelea na masomo yake ya kidini na falsafa na kuhudhuria masomo na darsa za walimu mahiri wa zama hizo kama vile mwanafalsafa Qashqaei na Mohammad Bagher Durchei.

Seyyed Hossein Tabatabai Borujerdi alikaa Isfahan kwa muda wa miaka minne na baada ya hapo akaenda kwenye Hawza ya Najaf na punde si punde akazingatiwa mno Akhund Khorasani, Marjaa mkubwa wa Mashia. Upepo wa sifa ya kipaji chake ulivuma na kuenea katika mji huo hadi kufikia hatua ambayo kila mtu alimwonyesha mwenzake na kusema: "Huyu ni Seyyid Hossein." Akhund Khorasani alikuwa akizingatia sana maoni yake kiasi kwamba, ikiwa hakutoa maoni juu ya jambo fulani, alikuwa akimtaka atoe maoni yake.

Miaka ya maisha ya Seyyid Hussein Tabatabai Borujerdi iliambatana na matukio mengi ya kisiasa na kijamii. Wakati Ayatollah Seyyid Hossein Borujerdi aliporejea Iran kutoka Najaf, takribani miaka minne ilikuwa imepita tangu kutokea kwa mapinduzi ya katiba nchini Iran.

 

Wananchi wa Iran walikuwa wamefanya hima na bidii kubwa, walivumilia matatizo mengi na vijana wengi walikuwa wamejitolea mhanga ili mapinduzi haya yatimie. Matokeo ya mapinduzi haya yalipaswa kuwa ni masharti na kubanwa mamlaka ya Shah kwenye sheria za Uislamu, lakini uingiliaji kati wa wasomi waliokuwa wameathirika na fikra za Kimagharibi na bila njama za Waingereza kulisababisha matokeo muhimu zaidi kuwa ni kuibuka kwa ukandamizaji na dhulma mpya ya ukoo wa Pahlavi.

 

Reza Shah Pahlavi kidhahiri alikuwa ameipata serikali yake kwa kura za wawakilishi wa wananchi Waislamu na kwa mujibu wa sheria alipaswa kutekeleza Uislamu. Lakini baada ya kushika hatamu za uongozi alianza haraka kupinga nembo na madhihirisho ya Uislamu na viongozi wa dini. Ili kugeuza sura ya jamii ya Wairani kuwa ya Kimagharibi, hakuepuka kufanya vurugu zozote, aliwapeleka uhamishoni au kuwapa sumu wanazuoni wanaompinga, na alijibu upinzani wowote wa umma kwa risasi na mtutu wa bunduki.

Ilikuwa ni wakati wa matukio haya ambapo kulitokea vita viwili katika eneo, vita ambavyo havikuwa na natija yoyote kwa Wairani isipokuwa uvamizi, uporaji, ukame, njaa, njaa na maradhi. Katika mazingira haya, Hawza ya Qom ilikuwa chini ya mashinikizo makubwa kutoka kwa serikali ya Pahlavi ambayo ilikuwa ikifanya kila iwezalo kuharibu mamlaka na heshima ya wanachuoni, na kwa upande mwingine, watu walikuwa katika hali ngumu sana kijamii na kiuchumi, na kinyume na ilivyokuwa huko nyuma hawakuwa tena na uwezo wa kuwaunga mkono wanachuoni.

Baya zaidi ya yote haya ni kwamba, kulikuwa kumetokea mpasuko kati ya wanazuoni wa Hawza ya Qom. Kila mmoja wao alitoa mpango na wazo tofauti wa kutoka katika hali hii isiyo ya kuridhisha. Mmoja alilingania kunyamaza kimya na mwingine aliwatakka watu waanzishe vuguvugu na mapambano. Hatimaye, ili kutatua hitilafu hizo, wanazuoni waliamua kuukabidhi uongozi na usimamizi wa Hawza kwa mmoja wa wanafunzi wa Akhund Khorasani, yaani Ayatollah Seyyed Hossein Tabatabai Borujerdi.

Reza Shah na mwanawe Muhammad Reza Pahlavi

 

 

Ayatullah Borujerdi alikuwa kiongozi wa Chuo cha kidini (Hawza) cha Qom kwa muda wa miaka 17 kuanzia mwaka 1944, yaani kuanzia alipokuwa na umri wa miaka sabini hadi mwisho wa maisha yake. Fauka ya hayo, tangu 1946, alikuwa pia Marjaa mkubwa na mashuhuri zaidi wa Mashia katika zama hizo.

Katika kipindi chote hiki alifanya hima na juhudi kubwa za kuhifadhi uwepo wa Hawza kuliko kitu kingine chochote na kwa ajili ya kufikia lengo hilo alijaribu kuzuia kupenya kwa vyama tofauti vya kisiasa na maoni yao kwenye Hawza. Aliwakataza wanafunzi na wanazuoni kujihusisha na siasa, kwa sababu kwa maoni yake ni kwamba, siasa zinazotawala katika eneo na Iran zilifanana zaidi na mchezo ambao mwisho wake haukuwa ukitabirika.

Ayatullah Borujerdi aliamini kwamba, katika hali ambayo Hawza imedhoofika sana na watu wako katika matatizo, hatuwezi na hatupaswi kutarajia mapinduzi. Kwa hiyo, alikuwa na nia zaidi ya kuweka msingi wa mapinduzi ya baadaye na alifanya kazi nyingi kwa ajili ya suala hili.

Moja ya kazi hizi ilikuwa ni kueleza na kubainisha nadharia ya Wilayat al-Faqih wakati wa kufundisha masomo yake. Nadharia ambayo ilikuwa ya kisiasa kikamilifu na ilikuwa ikichora ramani ya njia ya kuundwa utawala wa kidini ambao utakuwa chini ya Walii Faqih ambaye ametimiza masharti.

Katika zama za Umarjaa wa Ayatullah Borujerdi, kulichukuliwa hatua nyingi za kiutamaduni. Mbali na kuboresha masomo na masuala yanayohusiana na Hawza na wanafunzi, alitumia ushawishi wake ndani ya Baraza la Mawaziri la Shah na kuongeza masomo ya dini katika mtaala wa masomo wa wanafunzi mashuleni.

 Kwa mara ya kwanza Ayatullah Borujerdi aliwatumja nje ya nje kwa ajili ya masomo wanafunzi wa masomo ya dini (matalaba) ili wakasome elimu mpya. Akiwa na lengo la kuwafikishia walimwengu Uislamu halisi, aliwatuma wawakilishi huko Ulaya, Marekani, Afrika, India, Pakistan na Saudi Arabia. Aidha alijenga msikiti mkubwa katika mji wa Hamburg nchini Ujerumani, msikiti ambao hadi leo ni moja ya vituo vikubwa vya Tablighi ya Uislamu katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Msikiti wa Imam Ali Hamburg, Ujerumani

 

 

Katika zama za Umarjaa wa Ayatullah Borujerdi, Hawza ya Qom iligeuka na kuwa moja ya vituo muhimu zaidi vya dini katika Ulimwengu wa Kishia na kwa mara ya kwanza, Hawza ya Najaf ikashika nafasi ya pili. Miaka mingi baadaye, Hawza ya Qom ilikuwa sehemu ya kuanza vuguvugu na kuharakisha kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyopata ushindi mwaka 1979 kwa uongozi wa Imamu Ruhullah Khomeini.

Ayatullah Borujerdi alikuwa akizingatia sana suala la kuweko umoja baina yaa Mashia na Masuni. Moja ya hatua zake za kihistoria na muhimu katika uga huu, ni kuandaa kongamano la kukurubisha pamoja madhehebu huko nchini Misri.  Kongamano hili lilifanyika kwa kuhudhuriwa na Maulamaa mashuhuri 50 wa Kisuni na hatimaye Sheikh Shaltut, muasisi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar alitoa fatuwa ya kuruhusu kufanyiwa kazi fiq'h ya Kishia.  

Mwishoni mwa umri wake, Ayatullah Borujerdi alipatwa na maradhi ya moyo na akaaga dunia kwa maradhi haya haya. Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kishia aliaga dunia 1961 na mwili wake ukazikwa katika Haram ya Bibi Fatima Maasuma (as).

Waumini wakisindikiza mwili wa Ayatullah Borujerdi

 

Kwa leo muda wa kipindi chetu umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo saa na wakati kaama wa leo.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuuh