Jumamosi, 28 Oktoba, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe 12 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria mwafaka na tarehe 28 Oktoba 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1313 iliyopita, yaani tarehe 12 Mfunguo Saba Rabiuthani mwaka 132 Hijria, Abul Abbas Abdullah bin Muhammad maarufu kwa jina la 'Saffah' alikalia kiti cha uongozi akiwa khalifa wa kwanza wa kizazi cha Bani Abbasi. Utawala huo wa Kiabbasi kwa kushirikiana na Abu Muslim Khorasani na majeshi yake, ulimuuwa Marwan wa Pili, mtawala wa mwisho wa ukoo wa Bani Umayyah na kuondoa madarakani utawa wao. Bani Abbas nao kama walivyokuwa watawala wa Bani Umayyah, waliwakandamiza raia na Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) na kufanya dhulma kubwa, na utawala wao uliendelea kushika madaraka katika ulimwengu wa Kiislamu hadi mwaka 656 Hijria. ***

Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo, wakati wa vita vya kwanza kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Waarabu, wanajeshi wa utawala huo waliwaua kwa umati wakazi wa kijiji cha al Dawayima huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wazayuni hao walivamia msikiti wa kijiji hicho na kuwauwa shahidi Waislamu 75 raia wa Palestina waliokuwa wakiswali. Vilevile waliwaua kwa umati watu wa familia 35 waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika pango moja nje ya kijiji hicho. Askari jeshi wa utawala haramu wa Israel walikisawazisha na ardhi kijiji hicho baada ya kuwaua kwa umati wakazi wake wote. ***

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, ulihitimishwa mgogoro wa makombora wa Cuba baada ya kiongozi wa wakati huo wa Urusi, Nikita Khrushchev kuamuru kurejeshwa nyumbani meli zilizokuwa na makombora ya nyuklia. Hatua ya Urusi ya kujenga vituo kadhaa vya makombora ya nyuklia nchini Cuba katika umbali wa kilomita 90 kutoka Marekani ilizusha mgogoro mkubwa wa makombora uliokaribia kuitumbukiza dunia katika vita vya nyuklia. Wakati huo Marekani na Russia zilitishia kushambuliana kwa makombora ya nyuklia na kuzusha hofu kubwa hususan kwa watu wa Marekani, Russia na nchi za Ulaya. Hatimaye tarehe 28 Oktoba mwaka 1962 Nikita Khrushchev alitoa amri ya kurejea nchini meli zote zilizokuwa na makombora ya nyuklia na kufungwa vituo vya makombora vya Urusi nchini Cuba. ***

Katika siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, alifariki dunia Taha Hussein mwandishi mahiri na stadi wa Kimisri. Alizaliwa mwaka 1889 katika moja ya vijiji vya Misri. Taha Hussein ambaye alikuwa mtoto wa saba katika familia yake, alipofuka na kupoteza uwezo wa kuona akiwa na umri wa miaka mitatu. Hata hivyo Mwenyezi Mungu alimjaalia kipaji cha hali ya juu. Taha Hussein alifanikiwa kuhafidhi Qur’ani yote katika kipindi kifupi. Akiwa na umri wa miaka 14 alifaulu mtihani wa watahaniwa wa kuingia Chuo Kikuu cha al-Azhar na akiwa pamoja na kaka yake, alijishughulisha na kusoma masomo ya dini pamoja na lugha ya kigeni. Mwaka 1914 Taha Hussein alihitimu kwa alama nzuri na kutunukiwa shahada ya uzamivu yaani PhD. Wakati huo Chuo Kikuu cha Taifa cha Misri kilichukua uamuzi wa kuipeleka timu ya wahadhiri nchini Ufaransa kwa ajili ya kufundisha historia ya Mashariki. Akiwa ahuko alijifunza histotia ya Ugiriki na Roma ya kale pamoja na lugha ya Kigiriki. Mwaka 1959 mwandishi huyo mahiri wa Kimsri alinutukiwa tuzo ya Nobel kutokana na mchango wake katika uga wa fasihi. Taha Husserin ameandika vitabu vingi katika taaluma za fasihi, sayansi ya siasa na historia. ***

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alipinga vikali mpango wa Fahd bin Abdulaziz kuhusu mapatano ya Palestina na Israel. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na baada ya kutiwa saini mkataba wa Camp David baina ya serikali ya Misri na utawala ghasibu wa Israel chini ya upatanishi wa Marekani, tawala vibara za Kiarabu zilifuata nyayo za utawala wa Misri katika suala hilo. Wakati huo Fahd bin Abdulaziz aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, alitoa pendekezo la kutambuliwa rasmi utawala vamizi wa Israel, suala ambalo lilikabiliwa na upinzani mkali wa Waislamu kote duniani. Kwa msingi huo katika siku kama hii ya leo Imam Ruhullah Khomeini alitoa hotuba akisema: "Ni wajibu kwetu sisi na kwa kila Mwislamu kupinga mipango kama ule uliopendekezwa na Fahd. Tunawajibika kulaani mipango kama hii isiyokuwa na faida kwa watu wanaodhulumiwa. Jambo hatari sana kwa sasa ni makubaliano ya Camp David na mpango wa Fahd ambayo inaimarisha zaidi Israel na kudumisha jiani zake." Upinzani huo wa wazi wa Imam Khomeini na uungaji mkono wa Waislamu kote dunia kwa misimamo hiyo ya Imam ilikuwa sababu ya kukataliwa na kupingwa pendekezo hilo katika nchi nyingine. ***

Na siku kama ya leo miaka 7 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Taqi Tabatabai Qumi mmoja wa Marajii Taqlidi wa Kishia. Ayatullah Taqi Tabatabai Qumi ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Haji Agha Taqi Qumi alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsia katika mji wa Mash’had. Baba yake ni Sayyid Hussein Tabatabai Qumi aliyekuwa mmoja wa Marajii wakubwa wa Taklidi ambaye kutokana na kupinga amri ya Reza Shah mfalme wa wakati huo wa Iran ya kuondolewa hijabu kwa nguvu, alilazimika kuhama Iran na kuelekea Iraq. Sayyid Taqi alisoma masomo ya awali na ya utangulizi kwa baba yake na alipoelekea Iraq alisoma kwa walimu mahiri wa zama hizo kama Sayyid Muhammad Hadi Milani, Sayyid Abdul-Hadi Shirazi, Hussein Hilli, Muhammad Kadhim Shirazi na wengineo. ***
