Jumatano tarehe 06 Julai, 2016
Leo ni Jumatano tarehe Mosi Shawwal 1437 Hijria sawa na Julai 6 2016 inayosadifiana na sikukuu ya Idi al-Fitr.
Idul Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola Manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada huyo. Iddi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kujisafisha. Aidha katika siku kama hii ya leo ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kusali Sala ya Iddul Fitr. Kuhusiana na utukufu wa siku hii Mtukufu Mtume (saw) anasema: "Mtu yeyote atakayemuasi Mwenyezi Mungu katika siku ya Idi, basi ni kama mtu aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya miadi- yaani Siku ya Kiama." Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani.
Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita alifariki dunia George Simon Ohm mwanahisabati na mwanafizikia wa Ujerumani akiwa na umri wa miaka 67. Simon Ohm alizaliwa mwaka 1789 na alivutiwa sana somo la fizikia. Alifanikiwa kuvumbua kanuni katika uwanja wa umeme kutokana na utafiti mkubwa aliokuwa akiufanya katika uwanja huo. Alizipa kanuni hizo jina lake yaani "Ohm Laws". Kanuni ambazo zinatumiwa hadi leo hii.
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Malawi ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kabla ya Malawi kupata uhuru, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, makundi ya Wamishonari kutoka Scotland wakiwa pamoja na mvumbuzi David Livingstone waliwasili Nyasaland na kufuatiwa na Uingereza. Uingereza iliunga mkono uvamizi wa Ujerumani na Ureno huko Nyasaland na hatimaye mwaka 1891 nchi hiyo ikawekwa chini ya mamlaka yake. Kwa utaratibu huo Nyasaland ambayo ni Malawi ya leo ikawa miongoni mwa makoloni ya Uingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika. Malawi iko kusini mashariki mwa Afrika ikipakana na Tanzania, Zambia na Msumbiji.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, visiwa vya Comoro vilipata uhuru. Raia wengi wa visiwa vya Comoro walianza kuingia katika dini ya Kiislamu na kueneza utamaduni wa dini hiyo visiwani humo, baada ya wafanya biashara wa Kiislamu kuwasili visiwani humo katika karne ya 12 Miladia.
Tangu karne ya 16 visiwa vya Comoro vilikuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno na baadaye Sultan wa Oman alifanikiwa kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa visiwa hivyo. Hata hivyo mwaka 1842 sehemu kadhaa za visiwa hivyo ziliingia chini ya udhibiti wa Wafaransa na taratibu wakoloni hao wakaidhibiti ardhi yote ya nchi yote hiyo. Mapambano ya wananchi yalipelekea kutangazwa uhuru rasmi wa nchi ya Kiislamu ya Comoro mwaka 1975.
Comoro ina ukubwa wa kilomita mraba 1862 huku ikipatikana kusini mashariki mwa bara la Afrika katika bahari ya Hindi.