Feb 11, 2024 04:01 UTC
  • Jumapili, 11 Februari, 2024

Leo ni Jumapili Mosi Shaaban 1445 Hijria sawa na 11 Februari 2024 Miladia.

Mwezi wa Shaabani ulioanza leo ni mwezi wa ibada, kujipinda na kuomba maghufira. Mtume Muhammad (saw) aliutukuza mno mwezi huu na kuuita kuwa ni mwezi wake. Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake wamewausia mno Waislamu kufanya ibada hususan kufunga swaumu katika mwezi huu wa Shaabani kwa sababu ndio unaotayarisha uwanja mzuri wa kuingia kwenye mwezi wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na wenye baraka tele wa Ramadhan. Katika mwezi huu wa Shaabani kumetukia mambo mengi muhimu kama kuzaliwa Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw) na pia tukio la kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake. ***

 

Miaka 2684 iliyopita katika siku kama ya leo, mfalme wa kwanza wa Japan maarufu kwa jina la Jimmu alishika madaraka ya nchi. Kwa utaratibu huo mfumo wa kale zaidi na uliobakia kwa kipindi kirefu wa kifalme duniani ambao ungali unaendelea hadi sasa, ulianzishwa. Wafalme wa Japan huwa na cheo cha heshima tu na Waziri Mkuu ndiye anayeendesha masuala ya nchi. ***

Siku kama ya leo miaka 752 iliyopita Ghiathuddin Abu Madhaffar Abdul Karim bin Ahmad anayefahamika kwa lakabu ya Ibn Taus, alifariki dunia huko Kadhimain, moja kati ya miji ya Iraq. Ibn Taus alikuwa faqihi na mwandishi mashuhuri wa karne ya saba Hijria. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 11. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kiarabu na kupata elimu kwa wanazuoni wakubwa kama Khajah Nasiruddin Tusi. Ibn Taus ameandika vitabu kadhaa kwa lugha ya Kiarabu.  ***

Ibn Taus

 

Siku kama ya leo miaka 374 iliyopita alifariki dunia René Descartes, mwanafalsafa na mtaalamu wa hisabati wa nchini Ufaransa. Alizaliwa tarehe 31 Machi 1596 Miladia na baada ya masomo yake ya msingi alianza kusomea hisabati na tiba. Baadaye Descartes alibobea katika fani ya hisabati na uhandisi huku muda mfupi baadaye akianzisha utafiti pia katika uga wa falsafa. Aidha msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika fani nyinginezo za kielimu. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method. ***

René Descartes

 

Tarehe 22 Bahman miaka 45 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Iran ilikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote. Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi. Wananchi wanamapinduzi wa Iran, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee na watu wa matabaka yote walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran yalienea nchini kote huku wafuasi wa Imam Ruhullah Khomeini wakiwa katika juhudi za kumaliza kabisa mabaki ya utawala wa kidhalimu wa kifalme. Wakati ilipotangazwa habari kwamba vifaru vya majeshi ya Shah vilikuwa njiani kuelekea Tehran kwa ajili ya kukandamiza harakati za mapinduzi zilizokuwa zinaelekea kileleni, wananchi wa miji mbalimbali walijitokeza na kupambana na majeshi hayo huku wakifunga njia na kuzuia misafara ya vifaru hivyo. Baadhi ya makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Shah waliuawa na wananchi katika mapambano hayo na kulilazimisha jeshi kutopendelea upande wowote. Siku hiyo pia wananchi wanamapinduzi walitwaa Shirika la Redio na Televisheni la Iran kutoka kwenye udhibiti wa jeshi. Muda mfupi baadaye lilitolewa tangazo katika redio ya taifa likitangaza kwamba "Hii ni Sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu". Sauti hiyo ilitangaza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuporomoka utawala wa kidhalimu wa kifalme uliotawala Iran kwa kipindi cha miaka 2500. ***

 

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita sawa na tarehe 11 Februari 1990, Mzee Nelson Mandela kiongozi wa harakati ya kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini aliachiwa huru baada ya kufungwa jela kwa miaka 27. Mandela alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 1963 kwa sababu ya mapambano yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Lakini baada ya miaka kadhaa aliachiliwa huru kutokana na msimamo wake thabiti akiwa jela, mapambano ya wananchi wa nchi hiyo pamoja na mashinikizo yaliyotokana na fikra za waliowengi ulimwenguni. ***

Nelson Mandela

 

Tags