Mar 05, 2024 02:35 UTC
  • Jumanne, 5 Machi, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 24 ya mwezi Sha'ban 1445 Hijria sawa na tarehe 5 Machi 2024.

Katika siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, sawa na tarehe 5 Machi 1827 alifariki dunia Alessandro Volta, mtaalamu wa fizikia wa Italia akiwa na umri wa miaka 83.

Sambamba na kufundisha katika chuo kikuu, Volta alikuwa akifanya  uhakiki na alifanikiwa kutengeneza chombo cha kupimia kiwango cha umeme Electrometre.

Alessandro Volta

Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, alifariki dunia Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mar'ja' mashuhuri wa Kiislamu.  Alizaliwa mwaka 1230 katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini na kupata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari.

Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa ikihodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni. 

Mirza Muhammad Hassan Shirazi

Tarehe 5 Machi miaka 71 iliyopita alifariki dunia Joseph Stalin, kiongozi na dikteta wa Urusi ya zamani.

Stalin alizaliwa mwaka 1879 nchini Georgia na alijiunga na mrengo wa kikomunisti baada ya kusoma fikra za mrengo huo. Joseph Stalin alipelekwa uhamishoni huko Siberia mwaka 1913 kutokana na harakati zake za kisiasa dhidi ya serikali ya wakati huo ya Urusi.

Stalin alibakia huko hadi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Urusi mwaka 1917. Alipata vyeo vya ngazi za juu wakati wa uongozi wa Lenin na alishika uongozi wa nchi hiyo akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri baada ya kufariki dunia Lenin. Mwaka 1927 Stalin aliwafutilia mbali wapinzani wake ndani ya chama na kuwa kiongozi asiye na mpinzani katika Chama cha Kikomunisti. Joseph Stalin aliendelea kuwafuta na kuwaangamiza bila ya huruma wapinzani wake ndani na nje ya chama hicho.

Joseph Stalin

Tarehe 5 Machi miaka 11 iliyopita alifariki dunia rais wa zamani wa Venezuela, Hugo Chavez. Chavez aliyezaliwa tarehe 28 Julai mwaka 1954 alikuwa rais wa 64 wa nchi ya Venezuela. Alitambulika kama kinara wa "Mapinduzi ya Kibolivari" na alipata umashuhuri kwa siasa zake za demokrasia ya kisoshalisti, kupinga utandawazi wa kileberali na sera za nje za Marekani na kuziunga mkono Iran na Palestina. Hugo Chavez aliaga dunia mwezi Machi mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 58 kutokana na maradhi ya saratani.

Hugo Chavez

Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita alifariki dunia mbunifu wa E-mail yaani baruapepe, Ray Tomlinson. Tomlinson ambaye mwaka 1971 alikuwa akifanya kazi katika kampuni moja ya uhakiki kama mhandisi huko Boston nchini Marekani alianzisha mfumo wa awali wa E-mail katika mtandao wa Arpanet yaani nakala ya kwanza na intaneti. Mtaalamu huyo kwa hakika alituma baruapepe ya kwanza kabisa kwa mtindo wa kisasa. Ray Tomlinson alifariki dunia katika tarehe aliyozaliwa akiwa na umri wa miaka 75 kutokana na ugonjwa wa kiharusi.

Ray Tomlinson

 

Tags