Hadithi ya Uongofu (44)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Juma hili kipindi chetu hiki ambacho ni sehemu ya 44 ya mfululizo huu kitachajadili moja ya maudhui muhimu ya kijamii nalo ni suala la Swilat Rahm yaani kuunga udugu na kunukuu baadhi ya hadithi zinazoonesha umuhimu wa suala hili. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Moja ya vielelezo muhimu vya jamii salama na yenye saada ni kuweko mahusiano sahihi na miamala inayoambatana na mapenzi na huba baina ya wanajamii. Kwa hakika dini tukufu ya Kiislamu imezingatia engo zote za uwepo wa mwanadamu. Dini ya Kiislamu ikiwa na lengo la kuandaa uhusiano wa mwanadamu na wanadamu wenzake, imeweka sheria zenye thamani ambapo miongoni mwa sheria hizo ni Swilat Rahm yaani kuunga udugu au kuweko mawasiliano na mahusiano ya kifamilia au ya wanandugu.
Kwa hakika kujenga udugu na kuweko mawasiliano na maingiliano baina ya wanandugu ni jambo lenye nafasi maalumu na jambo hili limekokotezwa na kutiliwa mkazo mno.
Katika utamaduni wa Kiislamu kuunga udugu maana yake ni mtu kuwatendea wema na hisani ndugu zake ikiwa ni pamoja na kukutana nao na kuwatatulia matatizo yao. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, kila kazi au kitendo kinachopelekea kuunga udugu na wanandugu kinaitwa Swilat Rahm" hata kama itakuwa kazi ndogo sana kama kusalimia vizuri, kujibu salamu au kumpa mtu maji ya kunywa. Mkabala na hayo, kila kitendo cha kuwapuuza ndugu, kuwatelekeza na kutowatekelezea haki zao kinaitwa kuwa ni kukata udugu jambo ambalo hupelekea kutokea pengo baina ya wanandugu.
Ada na sunna ya kuunga udugu ni miongoni mwa ratiba bora kabisa za kidini katika mazingira ya maisha na kuamiliana na watu. Jambo hilo lina nafasi maalumu katika sira na mwenendo wa Mtume SAW na Ahlul Bayt zake AS.
Licha ya kuwa maisha ya kisasa na shughuli nyingi za kila siku pamoja na mazonge yake, wakati mwingine hulifanya jambo hili kukabiliwa na changamoto kadha wa kadha, lakini kulinda thamani na ada zenye faida na ambazo zina mizizi ya dini ni miongoni mwa mambo yanayoimarisha mahusiano na maingiliano ya kifamilia. Mtume SAW alitilia mkazo mno juu ya sunna na ada nzuri ya kuunga udugu. Hata mwanzoni mwa kazi yake ya kuwafikishia watu risala na ujumbe wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mtume SAW aliwazingatia ndugu zake wa karibu katika hilo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu akawaita na kuwalingania Uislamu.
Mtume SAW alikuwa akiutambua udugu kuwa ni mwanga wa rehma za Allah. Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa, "udugu ni mwanga na ishara za rehma za Mwenyezi Mungu."
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 36 ya Surat Nisaai:
Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri.
Tunaona katika aya hii kwamba, baada ya kuwafanyia wema na hisani wanachama wakuu wa familia, suala la uhusiano wa wanandugu limetiliwa mkazo na kukokotezwa. Kwa msingi huo katika hatua ya awali mtu anapaswa kumuonyesha huba na mapenzi baba na mama na kisha dada na kaka yake na katika hatua inayofuata awafanyie huba na mapenzi ndugu na jamaa zake na awe na mdakhala na maingiliano nao.
Mtume SAW anasema kuwa: Wafanyie wema kwa utaratibu yaani mama, kasha baba, dada, kaka na baada ya hapo jamaa wa karibu zaidi.
Kwa hakika Mtume SAW alikuwa akilipa umuhimu suala la mahusiano ya kidugu kiasi kwamba, kama itatokea hajamuona mmoja wa masahaba zake basi alikuwa akiulizia habari zake na kutaka kujua kilichomfanya asionekane. Akisikia kwamba, mmoja wa masahaba zake yu mgonjwa au ana tatizo, basi alikuwa akifunga safari na kwenda kumtembelea kwa shabaha ya kwenda kumjulia hali na akifika huko humliwaza na kumpa moyo. Ahlul Bayt wa Mtume SAW nao walikuwa namna hii na daima walikuwa wakitilia mkazo suala la mahusiano na kuimarisha uhusiano wa kidugu na kifamilia. Kwa kutumia aya za Qur'ani Tukufu na hadithi za Maimamu watoharifu tunaweza kuugawa mara mbili utekelezaji wa Swilat Rahm au kuunga udugu. Mambo kama kusalimia, kuwaombea dua nduguzo, kuwataja kwa wema na kujitenga mbali na kuwasengenya, kuwatuhumu, kuwatusi, kuwasema kwa ubaya na kuacha kufitinisha ni miongoni mwa mambo yanayohesabiwa kuwa ni ya kuunga udugu kwa njia ya ulimi. Aidha kuwatembelea, kwenda kufanya nao mazungumzo, kwenda katika nyumba zao na kuwaalika kwako, kuanzisha nao urafiki baada ya kununiana, na kujitokeza ugomvi baina yenu, kuwatembelea wakiwa wagonjwa, kushiriki katika mazishi, kurekebisha na kuondoa ufisadi baina ya wanandugu ni mambo ambayo yanaweza kuhesabiwa kuwa ni kuunga udugu kivitendo.
Kuna hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt zake watoharifu AS zinazobainisha faida nyingi zinazopatikana kutokana na kuunga udugu. Baadhi ya faida za kuunga udugu ni za kiroho na kisaikolojia na nyingine zinaashiria kuboreka maisha na kuleta marekebisho katika mahusiano ya watu sambamba na kuongeza huba, mapenzi na kuzikurubisha pamoja fuadi na nyoyo za watu katika jamii.
Inaelezwa katika hadithi nyingi kwamba, moja ya mambo yanayochangia kuongezeka umri wa mtu ni kuunga udugu. Kwani katika kivuli cha mawasiliano na ndugu, mivutano, madukuduku na wasi wasi usio na maana huondoka na kupelekea kupatikana nguvu, uchangamfu, utulivu na hata matumaini. Haya ni mambo ambayo yana taathira kubwa katika umri wa mtu. Imam Muhammad Baqir AS anasema: "Kuunga udugu huzifanya amali za mtu kuwa safi, huongeza mali, huondoa mabalaa, huifanya hesabu ya mtu Siku ya Kiyama kuwa nyepesi na huchelewesha kifo cha mtu."
Kufanya jambo jema ni kuzuri na kwenye faida na humridhisha Allah kiasi kwamba, wakati mwingine hubadilisha kadari na takdiri ya Allah ambapo Mwenyezi Mungu hutoa jaza na ujira wa kumuongeza mja huyo umri kutokana na kitendo hicho kizuri alichokifanya. Imam Ali AS anasema: "Kuweni na maingiliano na ndugu zenu, hata kama wao wamekata uhusiano na nyinyi."
Siku moja bwana mmoja alikwenda kwa Mtume SAW na kumwambia: Yaa Rasulallah! Mimi nina ndugu ambao nina mahusiano na maingiliano nao, lakini wamekuwa wakinifanyia maudhi. Hivyo nimekata shauri kuachana nao, yaani kukata mahusiano nao. Mtume SAW akasema: Ukifanya hivyo, basi naye Allah atakuacha. Bwana yule akauliza, basi nifanye nini ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Mtume SAW akamwambia, mtu ambaye amekunyima, wewe mpatie, mtu ambaye amekuacha wewe wasiliana naye, mtu ambaye amekufanyia dhulma, wewe msamehe. Ikiwa utafanya hivyo wakati wowote, basi Mwenyezi Mungu atakuwa ni mwenye kukuhami wewe.
Imenukuliwa kwamba, siku moja Bwana mmoja alimuuliza Imam Sadiq AS kwamba, baadhi ya ndugu zangu wana fikra na mitazamo inayopingana na fikra zangu. Je wana haki juu yangu? Imam Ja'afar Sadiq AS akasema: Ndio! Wana haki juu yako, haki ya kwanza ni haki ya udugu na familia, na haki ya pili ni haki ya Uislamu na Mwislamu.
Kama ambavyo kuunga udugu yaani Swilat Rahim kuna faida na taathira nyingi, pia kukata uhusiano na ndugu, kuwatelekeza na kutokuwa na mawasiliano na maingiliano nao, ni jambo ambalo linalokemewa mno na watu ambao wanakata udugu wamelaaniwa na Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 22 ya Surat Muhammad kwamba,
Basi yanayo tarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na mwatupe jamaa zenu? Hao ndio Mwenyezi Mungu alio walaani, na akawatia uziwi, na akawapofoa macho yao.
Kwa msingi huo ni jukumu la kila Mwislamu kutekeleza kuitekeleza Swilat Rahim yaani kuunga udugu
Kwa leo tunakomea hapa wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu.
Kwa leo muda wetu umefikia tamati hivyo sina budi kukomea hapa. Tukutane tena wiki ijayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…..