Jul 11, 2016 07:44 UTC
  • Ureno yaisasambua Ufaransa na kutwaa Kombe la Yuro 2016

Ahlan wasahlan wamarhaba mpenzi msikilizaji wa Radio Tehran na hususan ashiki wa spoti natumai huna neno. Baada ya kupezana kwa muda wa mwezi mmoja kutokana na kupumzishwa kipindi hiki cha Ulimwengu wa Michezo ili kupisha vipindi na mawaidha ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani, nakukaribisha kwa moyo mkunjufu nikupashe yaliyojiri viwanjani ndani ya siku saba zilizopita. Nakusihi tuandamane sote hadi tamati ya kipindi.

Wanamieleka wa Iran wazoa medali za dhahabu Taiwan

Wanamieleka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walioshiriki mashindano ya Mabingwa wa Mieleka barani Asia mwaka huu 2016 mjini Taichung katika kisiwa cha Taiwan, mashariki mwa China, wameshinda jumla ya medali 11, zikiwemo 8 za dhahabu. Mohammad Reza Mokhtari aliipa Iran medali ya dhahabu katika siku ya mwisho ya mashindano hayo siku ya Ijumaa, katika kitengo cha Greco-Roman, safu ya kilo 58, baada ya kumsasambua hasimu wake raia wa Uzbekistan, Mukhammadkodir Yusupov. Mabingwa wengine wa Iran waliong'ara katika safu ya Greco-Roman ni Omid Arami, kategoria ya kilo 42, Mohammad Mehrabi wa kategoria ya kilo 48 na Mohammad Hosseinvand wa kitengo cha kilo 50. Wanamieleka mahiri wa Iran waliyoiletea nchi hii dhahabu katika kitengo cha Freestyle ni Seyyed Abolfazl Hashemi, upande wa kilo 85 baada ya kuwalemea Mjapani, raia wa India na Mongolia. Mwigine ni Seyyed Mehdi Hashemi, aliyefanya vyema katika kitengo cha kilo 100 baada ya kuwabwaga chini raia wa India, Mongolia na Kyrgyzstan. Mashindano hayo yajulikanayo kama Asian Cadet Wrestling Championship yalifunga pazia lake Ijumaa iliyopita.

Voliboli: Iran yaibamiza Turkmenistan huko Taiwan

Timu ya taifa ya voliboli ya vijana ya Iran imeanza vyema duru ya 18 ya mashindano ya Mabingwa wa Voliboli Asia Wenye chini ya Miaka 20, baada ya kuitandika Turkmenistan seti 3-0 katika kitimutimu cha ufunguzi Jumamosi. Katika mchezo huo uliopigwa katika ukumbi wa Kaohsiung, kusini magharibi mwa mji wa Kaohsiung huko Taiwan, mabarobaro wa Iran ya Kiislamu waliwapelekea mbio viajana wa Turkmenistan, ikiwa ni mchuano wa kwanza wa Kundi B katika mashindano hayo ya kieneo.

Mkufunzi mkuu wa timu hiyo, Behrouz Ataei amewapongeza vijana wake kwa kuanza vyema na kusema kuwa: "Katika mashindano yoyote ile, mchuano wa kwanza huwa na ugumu Fulani, nimefurahi kikosi change kimejitahidi na kujituma na kuonyesha ugwiji wao."

Iran, Turknenistan, Qatar na Hong Kong zipo katika Kundi B huku Kundi A likizileta pamoja mwenyeji Taiwan, Thailand, Kazakhstan na Myanmar. Kundi C lina China, Japan na India huku Korea Kusini, Bahrain, Sri Lanka na Australia zikiorodheshwa katika Kundi D. Mashindano hayo ya kieneo yanayojulikana kama Asian Men's U20 Volleyball Championship yalianza Julai 9 na yanatazamiwa kumalizika Julai 17.

Ureno yaibamiza Ufaransa na kutwaa Kombe la Yuro 2016

Timu ya taifa ya Ureno imefuta uteja wa takriban miongo 4 dhidi ya Ufaransa kwa kuisasambua bao 1-0 katika mchuano wa fainali ya Kombe la Yuro mwaka huu 2016 mjini Paris. Ufaransa ambayo mara ya mwisho kufungwa na Ureno ilikuwa April 26 mwaka 1975 ilikubali kichapo cha bao 1-0 licha ya kwamba ilikua inaupiga nyumbani katika uwanja wa Stade de France katika kitongoji cha Saint-Denis, kaskazini mwa mji mkuu Paris. Fainali hiyo ya Jumapili ilichezwa katika hali ambayo, wengi walikuwa wamebashiri kuwa mwenyeji Ufaransa ingeshinda kutokana na rekodi yake ya miaka 40 kutofungwa na Ureno. Nusra vijana wa Ureno wapoteze matumaini baada ya nahodha wao Cristiano Ronaldo kushindwa kuendelea na mchezo kutokana na jeraha la goti. Mchezo huo ulionekana kuwa mgumu licha ya Ufaransa kuongoza kwa kumiliki mpira kwa asilimia 54 kwa 46. Dakika 90 za ada zilimalizika kwa suluhu ya mtungi kwa mtungi, hivyo refa akalazimika kuongeza dakika 30 za ziada na hapo ndipo kitumbua cha Wafaransa kikaingia mchanga, kupitia goli la pekee la mtoka benchi Eder Antonio la dakika ya 109.

Hii ni mara ya kwanza kwa vijana wa mkufunzi Fernando Santos kutwaa taji hilo na iwapo Ufaransa wangeshinda, wangekuwa tu wanaendeleza ubabe wao katika soka.

Dondoo: Messi ajipata pabaya baada ya kukwepa kodi

Lionel Messi, mshambuliaji nyota wa timu ya taifa ya Argentina na ambaye anakipiga pia katika klabu ya Barcelona ya Hispania, amejikuta akiandamwa na mkono wa sheria kwa kukwepa kulipa kodi. Messi amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela kwa makosa ya ukwepaji kodi. Baba yake, Jorge Messi, pia alihukumiwa kutumikia kifungo jela kwa makosa ya ubadhilifu wa yuro milioni 3.5 na milioni 4.5 kati ya mwaka 2007 na 2009. Mwanasoka huyo pamoja na baba yake, pia wametakiwa kulipa fidia ya mamilioni ya yuro kwa ukwepaji kodi na kuficha fedha kwenye nchi za Belize na Uruguay, fedha ambazo walizipata kutokana na haki za kutumia picha yake. Hata hivyo, wataalamu wa sheria nchini Hispania, wanasema kuwa huenda wasitumikie kifungo gerezani, kwakuwa sheria za Hispania, zinasema wazi kuwa, mtu akihukumiwa kifungo cha chini ya miaka miwili, anaweza asitumikie kifungo hicho jela na badala yake kuwa chini ya uangalizi maalumu. Lionel Messi na baba yake walipatikana na hatia ya makosa matatu ya ukwepaji kodi, katika uamuzi uliosomwa kwenye mahakama ya mjini Barcelona. Wakati wa kesi hiyo, Lionel Messi aliiambia mahakama kuwa, hakufahamu chochote kuhusu fedha zilizopatikana kupitia njia ya matangazo na usajili wake, na kwamba masuala yote yaliyokuwa yakihusu matumizi ya fedha zake, baba yake ndiye alikuwa muhusika mkuu.

......................................TAMATI.............................

 

Tags