Apr 17, 2024 02:47 UTC
  • Jumatano, tarehe 17 Aprili, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 8 Shawwal 1445 Hijria sawa na Aprili 17 mwaka 2024.

Miaka 121 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 8 Shawwal mwaka 1324 Hijria toleo la kwanza la gazeti la 'Majlis' lilichapishwa nchini Iran. Gazeti hilo lilianzishwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Mirza Sayyid Muhammad Sadiq Tabatabai. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mijadala yote ya Majlisi ya Ushauri ya Iran yaani Bunge.

Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, sawa na tarehe 17 Aprili 1915, kwa mara ya kwanza kabisa duniani ilitumiwa gesi ya kubana pumzi ya wanadamu vitani. Hatua hiyo ya kinyama ilichukuliwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Ujerumani ilitumia gesi hiyo ya kubana pumzi dhidi ya askari wa Uingereza na Ufaransa na kuua askari wengi wa vikosi vya Waitifaki. Wajerumani walipata ushindi katika vita hivyo vilivyokuwa mashuhuri kwa jina la Vita vya Gesi.   ***

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, Mawahabi wa Saudi Arabia walibomoa makaburi ya Ahlul Bait wa Mtume (s.a.w) ambayo yako Baqii, katika mji mtakatifu wa Madina. Baada ya Muhammad Ibn Saud kutawala tena maeneo ya Hijaz, likiwemo eneo la Madina, sheikh Abdullah bin Bulaihad aliyekuwa mkuu wa makadhi wa Kiwahabi, alitoa fatwa ya kuhalalisha kuharibiwa makaburi matukufu na ya kihistoria ya mjini Madina. Mawahabi walikusanya watu kwa nguvu na kuwalazimisha kwenda katika makaburi hayo ya Baqii na kuanza kubomoa na kuharibu kila kitu kilichokuwa juu ya makaburi ya mji wa Madina na nje ya mji huo. Miongoni mwa makaburi yaliyobomolewa na kuharibiwa vibaya ni makaburi manne ya maimamu na wajukuu wa Mtume (s.a.w), makaburi ya Abdullah na Amina, wazazi wa mtukufu Mtume (s.a.w), kaburi la Ibrahim mtoto wa kiume wa Mtume (s.a.w) na kaburi la Ummul Banin mke mwema wa Imam Ali bin Abi Twalib na makaburi ya masahaba wa Mtume (saw). Kaburi pekee lililobakishwa na Mawahabi hao wenye mioyo ya kikatili ni la Mtume Muhammad (s.a.w), kwani walijua kuwa kubomoa kaburi la mtukufu huyo kungezua hasira kali ya Waislamu duniani.

Makaburi ya Baqii

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, raia wa Scotland kwa jina la John Logie Baird, alifanikiwa kuvumbua televisheni ambayo hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa katika upashaji habari duniani. Baird alikuwa mmoja wa wavumbuzi wakubwa wa enzi zake. Baada ya hapo mtu wa kwanza kutengeneza televisheni iliyoimarika zaidi alikuwa Giovanni Caselli, raia wa Italia ambaye mnamo mwaka 1862 alifanikiwa kutengeza chombo ambacho kwa kutumia mfumo wa telegrafi, kiliweza kutoa ramani na picha. Televisheni ya kwanza ambayo ilionyesha vizuri picha, ilianza kutumika tarehe 17 mwezi Aprili mwaka 1926 kwa ajili ya klabu ya kifalme nchini Uingereza. 

John Logie Baird

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika mji wa Mash'had huko kaskazini mashariki mwa Iran.  Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alikuwa mwana wa marhoum Hujjatul Islam wal Muslimin Hajj Sayyid Javad Husseini Khamenei na alikuwa mtoto wa pili katika familia. Maisha ya Sayyid Javad Khamanei, sawa na ya wanazuoni wengi yalikuwa sahali na ya kawaida kabisa. Ayatullah Khamenei alipata malezi bora katika familia ya kidini na kuanza kusoma akiwa na umri wa miaka minne. Akiwa na umri wa miaka 18, Ayatullah Khamenei alianza masomo  chini ya usimamizi wa mwanazuoni na marjaa maarufu Ayatullahil Udhma Milani. Sayyid Ali Khamenei alianza masomo ya dini chini ya usimamizi wa baba yake na kupiga hatua zaidi za maendeleo katika uwanja huo. Hatimaye alielekea katika mji mtakatifu wa Qum na kuendelea na masomo ya juu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kwa muda wa miaka saba. Wanazuoni kama Imam Khomein MA, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai ni miongoni mwa wasomi ambao Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alipata elimu kutoka kwao. Katika kipindi cha ujana wake Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei alijiunga na harakati za Imam Khomein MA za kuupinga utawala wa kidikteta wa Shah. Alieneza fikra za Imam Khomein na kufichua ufisadi wa viongozi waliokuwa katika utawala wa wakati huo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikamatwa na kutiwa gerezani mara kadhaa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa mwanachama wa Baraza la Mapinduzi na kisha baada ya hapo, aliwahi pia kuchaguliwa kuwa mbunge na pia mwanachama wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu. Aidha alikuwa Rais wa Iran katika duru mbili mfululizo na hatimaya mwaka 1989, baada ya kuaga dunia Imam Khomeini MA, alichaguliwa na Baraza la Wataalamu kuwa Kiongozi wa pili wa Iran. 

Sayyid Ali Khamenei

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Aprili 1946, Syria ilijipatia uhuru wake kutoka kwa askari wa kigeni waliokuwa wakiitawala nchi hiyo. Syria na baadhi ya ardhi zinazoizunguka awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Sham, na kabla ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu ilikuwa chini ya udhibiti wa Iran, Ugiriki, Misri na Rome. Ardhi hiyo ilikuwa makao ya utawala wa Ugiriki na baada ya kukaliwa kwa mabavu na Misri, baadaye ilichukuliwa na utawala wa Othmaniya. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya kuporomoka utawala wa Othmaniya, Syria ilikoloniwa na Ufaransa. Kufikia Juni 1941, wakati wa vita vya pili vya dunia, askari wa Uingereza na Ufaransa waliikalia kwa mabavu nchi hiyo, hadi kufikia mwaka 1946 wakati ilipojipatia uhuru wake.   

سوریه

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo yaani 29 Farvardin mwaka 1358 Hijria Shamsiya, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  lilitangaza utiifu kwa Imam Khomeini (MA) Hayati Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Siku hiyo Jeshi lilitangaza utiifu kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mnasaba huo likaandaa gwaride zisizo na kifani kote Iran.

Gwaride hizo zilipokelewa kwa vuraha na wananchi Waislamu wa Iran kwani zilikuwa ni dhihirisho la mshikamano wa wananchi na jeshi katika njia ya kulinda Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Kiislamu. Kwa msingi huyo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku hiyo hutambuliwa kama 'Siku ya Jeshi' na kila mwaka huandaliwa gwaride maalumu kwa mnasaba huo.

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, mwafaka na tarehe 17 Aprili 2004, vifaru vya utawala wa Kizayuni wa Israel vilishambulia gari lililokuwa limembeba Dakta Abdulaziz Rantisi, mwanaharakati wa Palestina na kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, na kumuuwa shahidi. Dakta Rantisi alichaguliwa kuiongoza harakati ya Hamas baada ya kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwasisi na kiongozi wa harakati hiyo. Rantisi alizaliwa mwaka 1964 katika mji wa Yafa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na alihitimu elimu ya tiba kama daktari katika chuo kikuu cha Alexandria nchini Misri. 

Dakta Abdulaziz Rantisi

 

Tags