Apr 23, 2024 02:23 UTC
  • Jumanne, tarehe 23 Aprili, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 14 Shawwal 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 23 Aprili mwaka 2024.

Katika siku kama ya leo miaka 871 iliyopita alifariki dunia Qutbuddin Rawandi, faqihi wa karne ya sita Hijria ambaye pia alikuwa mtaalamu wa Hadithi na teolojia ya Kiislamu.

Kwa miaka mingi alipata elimu na maarifa kwa wasomi wakubwa wa zama zake na kubobea katika taaluma za fiq'hi, Hadithi na tafsiri ya Qur'ani.

Msomi huyu mkubwa wa Kiislamu ameandika karibu vitabu 80 vikiwemo vya "Tafsirul Qur'an", "Risaalatul-Fuqahaa", "Tahafutul Falasifa", "Aayaatul-Ahkaam" na "Asbaabun-Nuzul."

Qutbuddin Rawandi

Katika siku kama ya leo miaka 408 iliyopita, aliaga dunia William Shakespeare, mshairi na mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Uingereza. Shakespeare alianza kazi zake za usanii sambamba na kushiriki katika michezo ya kuigiza. Alipata umashuhuri mkubwa katika taaluma hiyo. Kazi zake za kisanii zilikuwa mchanganyiko wa sanaa iliyoakisi majonzi na vichekesho. Miongoni mwa kazi maarufu zaidi za Shakespeare ni Romeo and Juliet, Hamlet, King Lear na The Merchant of Venice.   

William Shakespeare

Miaka 166 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mwanafizikia Max Plank wa Ujerumani ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hisabati aliyebuni Nadharia ya Kwanta katika elimu ya fizikia.

Mwaka 1918 Max Plank alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel kwa kugundua nadharia ya kwanta. Plank ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler, alifanya utafiti mkubwa katika nyanja za mwendojoto (sayansi ya uhusiano wa joto na kazi za mitambo), fizikia nadharia, joto, mnururisho na nuru na kuandika vitabu kadhaa katika medani hiyo.

Max Plank

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, kwa mara ya kwanza kulianzishwa idara ya redio nchini Iran na kurushwa matangazo ya moja kwa moja. Awali kituo cha redio kilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Posta, Simu na Telegrafu. Miaka mitano baada ya kuanzishwa kituo cha redio mjini Tehran, hatua kwa hatua huduma hiyo ilipanuliwa katika miji mbalimbali hapa nchini.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu 1979, zilianzishwa redio na televisheni kadhaa, zikiwemo zile za matangazo ya ng'ambo, zinazotangaza kwa lugha mbalimbali za kigeni ikiwemo Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyoanzishwa mwaka 1994.

IRIB

Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Aprili 1992, alifariki dunia Satyajit Ray mwandishi na mtengeneza filamu mashuhuri wa India.

Satyajit Ray alizaliwa mwaka 1921, na filamu zake za kijamii ziligusa zaidi hisia za jamii ya wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kupendwa zaidi na wananchi wa India. 

Satyajit Ray

Na tarehe 23 Aprili miaka 29 iliyopita Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku hii ya kuwa Siku ya Kimataifa ya Kitabu na Haki za Mwandishi.

Lengo la kutangazwa siku hiyo ni kuonesha umuhimu wa kitabu na haki za waandishi wa vitabu, kuhamasisha watu kusoma vitabu, kuwapongeza watu wanaoandika vitabu kwa ajili ya kukuza na kustawisha utamaduni wa jamii ya mwanadamu na vilevile kuunga mkono na kusaidia ustawi wa sekta ya kusambaza vitabu.

Utamaduni wa kusoma vitabu umeshamiri zaidi katika dunia ya sasa hususan miongoni mwa tabaka la vijana kutokana na kusambaa zaidi vitabu vya elektroniki kupitia mitandao ya intaneti. 

 

Tags