Apr 29, 2024 04:26 UTC
  • Tuujue Uislamu (12)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 

Katika kipindi chetu cha juma hili tutaendelea kubainisha kumtambua Mwenyezi Mungu kupitia kuangazia  mimea na maajabu yanayopatikana katika mimea hiyo. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki, hii ikiwa ni sehemu ya 12 ya mfululizo huu.

 

Kutembelea na kuvinjari katika asili na mandhari ya kijani kibichi nzuri na yenye kupendeza kuna athari kubwa juu ya upanuzi wa nafsi ya mwanadamu. Bila shaka wewe pia mpenzi msikilizaji umewahi kutumia masaa kadhaa ukiwa katika mandhari kama hii ili kujadidisha na kukusanya upya nguvu zako na hivyo kupunguza uchovu? Je umewahi kufikiria ni kwa jinsi rangi ya kijani kibichi inaleta furaha na nishati? Kwa hakika, mimea ina nafasi muhimu katika maisha ya binadamu na wanyama na afya na hata uzima wa mazingira.

Bila shaka umewahi kuona muundo na mandhari ya maua mazuri pamoja na rangi zake tofauti tofauti. Sisi sote tumewahi kunusa mara chungu nzima harufu nzuri ya uturi wa maua na kutambua jinsi harufu ya maua hayo ilivyokuwa nzuri na ya kuvutia. Je, kuna mchoraji yeyote stadi aliyewahi kuchora picha nzuri kama zile tunazoziona katika mandhari ya bustani ya maua? Kwa hakika mandhari hizi na muonekano huu wa kushangaza na wenye mpangilio wa ajabu ni uthibitisho wa kuwepo kwa Muumba ambaye ana ujuzi na uwezo usio na kikomo.

Jambo hili limeashiriwa katika Qur’an ambapo Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 141 ya Surat al-An’am:

 Na Yeye ndiye aliyeziumba bustani zenye kutambaa juu ya chanja, na zisiotambaa, na mitende, na mimea yenye matunda mbalimbali, na mizaituni na mikomamanga inayofanana na isiyofanana. Kuleni matunda yake inapozaa, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo. Hakika Yeye hawapendi watumiayo kwa fujo.

 

Wapenzi wasikilizaji, jambo la kuvutia ni kwamba maua ya rangi kwa rangi, matunda mbalimbali, nafaka za chakula, na hatimaye mandhari haya yote mazuri na ya kupendeza ambayo yanapamba dunia na kuyafanya mazingira tunayoishi kutawaliwa na mandhari nzuri, yote hayo yanatoka kwenye udongo. Yanatoka katika udongo huu wa giza ulio chini ya miguu yetu. Hakika, udongo ni kama maabara ya hali ya juu sana, hutokeza aina mbalimbali za bidhaa na kuzifanya zipatikane kwa wanadamu. Zawadi hizi zote za uhai hutokaje katika udongo usio na roho wala uhai?

Mwenyezi Mungu anapasua mbegu na kokwa katika moyo wa udongo wenye giza ili kutoa njia ya uumbaji wa mandhari haya yote mazuri na yaliyopanuka. Fikiria na kujaalia bustani au shamba katika taswira yako. Bustani hii yote au shamba hutiwa maji kwa sura sawa, udongo ni wake takribani uko sawa. Mwanga wa jua pia huangaza kwenye udongo huu kwa sifa na hali sawa. Licha ya kuweko hali hizi sawa, lakini tunaona kuwa, kila aina ya maua na matunda yenye rangi mbalimbali yenye maumbo na ladha tofauti huibuka na kuota katika bustani au shamba lile. Hii ni ishara ya mpango wa ubunifu na utaratibu Muumba wa ulimwengu huu.

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 4 ya Surat Raad:

Na katika ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isio chipua kwenye shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yao bora kuliko mengine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanaotia mambo akilini.

Jambo lingine kuhusu mimea ni faida na mchango wa majani ya mimea. Mmea hupumua kupitia majani. Moja ya shughuli muhimu zaidi za majani ni kukabonisha yaani kuigeuza kuwa kaboni. Mimea ya kijani kibichi inapoangaziwa na jua, huchukua kaboni dioksidi kutoka kwa mazingira, kuibadilisha kuwa kaboni na oksijeni, kisha huiacha oksijeni hewani na kubakisha kaboni. Hivyo, mimea ina jukumu muhimu katika kudhibiti oksijeni na kaboni dioksidi katika hewa. Kama unavyojua, wanadamu na viumbe vingine hai wanavuta oksijeni na kutoa nje hewa chafu ya kaboni dioksidi.

 

Chakula kinachohitajika na mimea hutolewa kwenye majani yao. Majani yana rangi inayoitwa klorofili. Klorofili husababisha majani kugeuka kijani. Klorofili huzalisha chakula kwa kutumia kaboni dioksidi, maji, virutubisho na nishati ya jua. Kwa hakika michakato yote hii ambayo ina mpangalio wa kushangaza haiwezekani kuwa inatokea hivi hivi bila ya kuweko mwenye kusimamia na kuendesha yote haya ambaye si mwingine bali ni Muumba wa ulimwengu huu.

Moja ya maajabu ya ulimwengu wa mimea ni kwamba, sheria ya urithi inatawala baina yao. Katika kiini cha seli za jinsia za mimea, kuna sababu ambayo inalinda sifa za kila aina ya mmea kwa karne nyingi na katika mazingira na hali tofauti. Moja ya ishara za hekima ya Mungu katika mimea ni kwamba, kila aina yao ina shina maalumu, majani na maua ambayo yanaweza kutambuliwa kati ya maelfu ya aina nyingine.

Moja ya maajabu mengine ya uumbaji ni ukuaji wa mimea maalumu katika maeneo ya jangwa. Muundo wa mimea hii unaendana kabisa na hali ya hewa ya eneo kavu na la moto ambapo hukua. Dungusi kakati ambayo ni aina ya mmea kama mpungate ni moja ya mimea hii. Mimea ya jangwani huhifadhi maji wanayohitaji katika mizizi yao mikubwa, shina nene au majani yenye nyama. Baadhi ya mimea hii ina uso wa nywele ambao hunasa unyevu hewani na kuizuia kukauka.

Katika Aya kadhaa za Qur'ani, imetajwa kuhusu mimea na manufaa na umuhimu wake. Makusudio ya Qur’ani ni kuwafahamisha watu kwamba matunda na mimea yote hii tofauti imeundwa kwa sababu zipi? Qur’ani inawahimiza watu kutumia matunda ya rangi na ladha na baraka nyinginezo za Mwenyezi Mungu, lakini inakumbusha kwamba watu hawapaswi kuridhika na kutosheka na hili.

Badala yake, mtu anapaswa kufikiria ni mkono gani wa msanii umeunda uzuri mwingi. Tunapoingia kwenye bustani, tuangalie miti, maua na matunda kwa macho ya hekima. Kumbuka matunda haya yalikuwa hayajaiva, lakini sasa kutokana na maji, udongo na jua yamepakwa rangi nzuri na yamepata uchangamfu maalumu ili tuyale kwa raha na buraha. Bila shaka, watu wenye hekima na wanaofikiri wanaona katika mabadiliko haya na mabadiliko ya maua, mimea na matunda, kwamba, kuna ishara za nguvu na mipango ya ulimwengu wa uumbaji na kwa hakika yote haya ni ishara za kuweko Muumba.

 

 Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijao.

Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh