Jumanne, Mei 7, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 28 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria sawa na tarehe 7 Mei 2024.
Siku kama ya leo miaka 972 iliyopita alizaliwa Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran katika eneo la Ghaznin, moja ya miji ya kale ya Iran na ulioko katika Afghanistan ya sasa.
Akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi.
Sanā'ī Ghaznavi alianzisha mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi ambapo pia ndani yake ameweka wazi fikra za kiakhlaqi na irfani za malenga.
Vitabu vya 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi.
Miaka 216 iliyopita katika siku kama ya leo wananchi wa Uhispania walianzisha harakati dhidi ya vikosi vya jeshi la Mfalme Napoleon wa Ufaransa, vilivyokuwa vinakalia kwa mabavu nchi yao.
Wakati huo Uhispania pia ilikuwa ikihesabiwa kuwa moja ya makoloni makubwa ya Ulaya na ilikuwa ikikalia kwa mabavu ardhi nyingi nje ya bara hilo. Lakini wananchi wa Uhispania walikuwa wameonja uchungu wa nchi yao kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya kigeni.
Baada ya miaka mitano ya mapambano dhidi ya vikosi vamizi vya Ufaransa, walifanikiwa kuvifukuza vikosi hivyo mwezi Disemba mwaka 1813 kutoka nchini kwao. Wakati huo huo kutokana na kushindwa katika Amerika ya Kusini, Uhispania ililazimika kuziacha huru nchi kadhaa ilizokuwa ikizikoloni.
Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, alizaliwa Robert Browning, malenga na mwanafikra wa nchini Uingereza.
Akiwa kijana mdogo Browning alikuwa na maandalizi ya kuwa malenga ambapo alitoa shairi lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 12. Taratibu akaanza kupata umashuhuri katika jamii ya Uingereza kama malenga mkubwa.
Robert Browning alikuwa akiwasilisha itikadi yake juu ya umoja wa Mungu duniani kupitia mashairi yake. Ameacha athari nyingi katika uwanja huo. Robert Browning alifariki dunia mwaka 1889.
Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mei 1888, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilianzisha uvamizi katika ardhi ya Zimbabwe ya sasa.
Mipango ya kuikalia kwa mabavu Zimbabwe ilibuniwa na mwanasiasa na mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina la Cecile Rhodes, ambaye aliasisi shirika la Afrika Kusini la Kiingereza nchini humo.
Kwa kusaidiwa na jeshi la Uingereza, Rhodes aliuwa kwa umati maelfu ya raia wazalendo na kuwakamata mateka wengine wengi, na hivyo kuweza kuidhibiti ardhi yote ya Zimbabwe na kuipachika jina lake la Rhodesia.
Na siku kama hii ya leo miaka 42 iliyopita mji wa Huweize ulioko kusini mwa Iran ulikombolewa katika operesheni kubwa iliyopewa jina la Baitul Muqaddas ya wanajeshi supavu wa Iran kutoka kwenye makucha ya jeshi vamizi la Saddam Hussein wa Iraq.
Mji huo wa Huweize unatambuliwa kuwa moja kati ya nembo za ushujaa na ujasiri wa vijana wa Iran. Operesheni hiyo iliongozwa na Shahidi Alamul Huda na wenzake kadhaa waliopambana na maadui hadi tone la mwisho la damu zao katika miezi ya mwanzoni mwa uvamizi wa jeshi la Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ukombozi wa Huweize ulikuwa utangulizi wa ushindi mkubwa zaidi wa jeshi la Iran ya Kiislamu wa kukomboa mji wa Khorram-Shahr.