Jumatatu, tarehe 20 Mei, 2024
leo ni Jumatatu tarehe 11 Dhulqaada 1445 Hijria sawa na Mei 20 mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1297 iliyopita, yaani tarehe 11 Dhilqaada mwaka 148 Hijiria, alizaliwa Imam Ali bin Musa al-Ridha (as), mmoja wa Ahlu Bayti watukufu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Madina.
Imam Ridha (as) alianza kuongoza Umma wa Kiislamu mwaka 183 Hijria baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu, yaani Imam Musa al-Kaadhim (as). Katika uhai wake alifahamika kama shakhsia wa pekee katika Ulimwengu wa Kiislamu kutokana na elimu yake kubwa na uchaji-Mungu. Ni kutokana na hali hiyo na katika kujaribu kudhibiti hali ya mambo na kuzuia taathira chanya za mtukufu huyo katika ulimwengu wa Kiislamu, ndipo khalifa wa utawala wa Bani Abbasi yaani Ma'amun, akamlazimisha kuwa mrithi wake wa kiti cha ufalme lengo kuu likiwa ni kumdhibiti Imam Ridha (as).
Hatua hiyo ilimlazimu mtukufu huyo kupelekwa mjini Mar'wu, kaskazini mashariki mwa Iran ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Bani Abbasi enzi hizo. Hata hivyo njama chafu hizo za mtawala Ma'amun ziligonga mwamba baada ya watu wengi kuvutiwa sana na Imam Ridha kutokana na elimu ya hali ya juu na mawaidha yake aliyokuwa akiyatoa kwa Waislamu suala ambalo lilipelekea mtawala huyo kupanga njama za kumuua. Hatimaye mwaka 203 Hijiria, Imam Ridha akauawa shahidi baada ya kulishwa sumu ndani ya chakula.
Siku kama ya leo miaka 1108 iliyopita, alizaliwa mjini Baghdad, Iraq, Muhammad Bin Muhammad, maarufu kwa lakabu ya 'Sheikh Mufid', msomi na faqihi mkubwa wa Kiislamu.
Sheikh Mufid alikulia katika familia ya watu wenye elimu na imani, na lipata elimu ya msingi katika familia yake na kisha kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baada ya hapo Muhammad, alitokea kuwa alimu mkubwa katika uga wa teolojia na sheria za Kiislamu wa zama hizo.
Miongoni mwa harakati za kifikra na kitamaduni za Sheikh Mufid ni pamoja na midahalo yake ya kielimu na wasomi wa sheria za Kiislamu na maulama wa madhehebu tofauti za Kiislamu, suala ambalo lilimfanya kuwa mwanazuoni hodari katika uga wa teolojia na fiqhi.
Sheikh Mufid ameacha athari nyingi za vitabu ambavyo vinafikia juzuu 200 baadhi yavyo ikiwa ni vitabu vya 'Al-Irshaad' 'Al-Arkaan' na 'Usulul-Fiqhi.'
Miaka 518 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 20 Mei mwaka 1506 aliaga dunia baharia mashuhuri wa Kiitalia Christopher Columbus.
Columbus alizaliwa Septemba 21 mwaka1 451 huko kusini mwa Italia. Mwezi Agosti mwaka 1492 Christopher Columbus alianza safari yake kuelekea Bahari ya Atlantiki. Watu wengi wanamtambua Columbus kuwa mtu wa kwanza kutoka Ulaya aliyevumbua bara la America. Tangu wakati huo historia ya bara hilo iliandikwa kwa mujibu wa matakwa ya wazungu na wahamiaji wapya.
Historia hiyo iliambatana na machungu ya ukoloni kutoka maeneo tofauti ya dunia dhidi ya wakazi asili wa ardhi hiyo, huku ubaguzi ukiwa mhimili wa siasa kuu iliyotekelezwa na wahamiaji wazungu. ***
Siku kama ya leo miaka 218 iliyopita alizaliwa John Stuart Mill mwanafalsafa na mwanauchumi wa Uingereza.
Stuart Mill alilelewa na kufunzwa na baba yake elimu za mantiki na uchumi na baadaye kuanza kuandika magazeti. Mill pia alichaguliwa kuwa mwakilishi wa bunge la Uingereza kwa duru moja.
Vitabu muhimu vya mwanauchumi huyo wa Kiingereza John Stuart Mill ni vile alivyoviita "Principals of Political Economy" na "Principals of Political Science". Mill aliaga dunia mwaka 1873. ***
Katika siku kama hii ya leo miaka 122 iliyopita Cuba ilitangazwa kama jamhuri huru na wanajeshi wote wa Marekani wakaondoka katika ardhi ya nchi hiyo.
Cuba ambayo iligunduliwa na Christopher Columbus tangu mwaka 1492, ilikuwa koloni la Uhispania hadi kufikia mwaka 1898 Miladia. Lakini Marekani iliingiza vikosi vyake nchini humo na kuchukua nafasi ya mkoloni Uhispania baada ya kutoa pigo na kuifukuza nchi hiyo huko Cuba, kwa kisingizio eti cha kuwaunga mkono wanamapambano wapigania uhuru wa Cuba. ***
Katika siku kama ya leo miaka 90 iliyopita Yemen ilishindwa mwishoni mwa vita vilivyojiri kati yake na Saudi Arabia baada ya nchi mbili hizo kuhitilafiana juu ya suala la mpaka na kupelekea kusainiwa makubaliano ya Ta'if kati ya Imam Yahya wa Yemen na Mfalme Abdulaziz wa Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Yemen iliikabidhi Saudia maeneo ya Najran, Jizan na Asir kwa muda wa miaka 40. Saudia ilianzisha vita vipya dhidi ya Yemen mwezi April 2015 kwa ajili ya kuyadhibiti zaidi maeneo hayo. ***
Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.
Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani ambayo iliikalia kwa mabavu Cameroon kuanzia mwaka 1884. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Ufaransa na Uingereza ziligawana ardhi ya Cameroon. Hata hivyo haukupita muda kabla ya kuanza mapambano ya kupigania uhuru nchini humo.
Hatimaye mapambano ya kupigania uhuru nchini Cameroon yalizaa matunda katika siku kama ya leo baada ya nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika kujipatia uhuru. ***
Siku kama ya leo, miaka 61 iliyopita, mwafaka na tarehe 20 Mei mwaka 1963, kongamano la kihistoria la nchi za Afrika lilifanyika huko Addis Ababa, Ethiopia.
Madola mengi ya Kiafrika yalijinyakulia uhuru katika miaka ya 60 na 70, na katika kipindi hicho hayakuwa na uhusiano baina yao. Ili kuunda jumuiya ya kwanza iliyokusudiwa kuzikurubisha pamoja nchi za Afrika, kongamano la kwanza la nchi hizo lilifanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa tarehe kama ya leo. Kongamano hilo ilikuwa hatua ya kwanza ya kuasisiwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU.
Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao uliundwa mwaka 1963 kwa shabaha ya kusimamia maslahi ya nchi wanachama, kuhamasisha maendeleo ya bara hilo na kutatua migogoro kati ya nchi Afrika.