May 31, 2024 22:40 UTC
  • Jumamosi, 01 Juni, 2024

Leo ni Jumamosi tarehe 23 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1445 Hijria mwafaka na tarehe Mosi Juni 2024 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 364 iliyopita Mary Barrette Dyer, ambaye alikuwa mhubiri wa Quakerism huko Marekani, alinyongwa na mahakama ya Massachusetts kwa sababu za kidini. Wakati huo, sheria ya Massachusetts ilikataza Maquakers kuingia eneo hilo. Wafusi wa kundi hilo wanaojuulikana kama Quakers ni watu waliokuwa katika kundi la kihistoria la Kikristo la Kiprotestanti linalojulikana kama Jumuiya ya Kidini ya Marafiki. Quakerism iliibuka katika karne ya 16 na 17 kama jibu kwa hitilafu na vita vya kidini vilivyotokea huko Ulaya na vilevile uhasama na mizozo baina ya madhehebu ya Kikristo nchini Uingereza. George Fox alikuwa mmoja wa wahubiri mashuhuri wa kundi hilo. Kundi hili lilienea polepole katika ulimwengu wa Kikristo. Quakers waliamini katika kurahisisha shughuli za kidini na kwamba kanisa halipaswi kuwa na mchungaji maalumu na anayelipwa mshahara na kuwa kiunganishi na wasita kati ya Mungu na Mtume wake kwa upande mmoja, na watu wa kawaida kwa upande mwingine. Waliamini kuwa mahubiri na mafundisho ya Kikristo yanapaswa kufanywa kwa hiari na kila mtu mwenye ujuzi. ***

Siku kama ya leo tarehe Mosi Juni miaka 72 iliyopita, aliaga dunia John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Alihitimu falsafa katika Chuo Kikuu cha Vermont kabla ya kuwa na umri wa miaka ishirini, na baada ya kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya falsafa, alifundisha katika Chuo Kikuu cha Columbia. Dewey alibobea mno katika taaluma ya elimu na malezi. Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na elimu na malezi. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture." John Dewey alifariki dunia mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93. ***

Siku kama ya leo Miaka 54 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu. ***

Miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo,  sawa na tarehe 12 Khordad mwaka 1379 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi, mwanzuoni mwenye mwamko na mwanaharakati wa Iran katika ajali ya gari pamoja na baba yake Ayatullah Sayyid Abbas Abuturabi. Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi alizaliwa mwaka 1318, kwa mujibu wa kalenda ya Iran, katika mji wa kidini wa Qum. Alijifunza elimu ya dini kutoka kwa maulamama wakubwa akiwemo Imam Khomeini (M.A). Hujjatul Islam Abuturabi katika mapambano ya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu mara kadhaa alikamatwa na kuteswa na vibaraka wa Shah. Wakati vya vita vya Iran na Iraq mwaka 1359 alikamatwa mateka na askari wa utawala wa Baath wa Iraq na kufungwa kwa miaka 10 katika jela zenye mateso makali za Iraq. Lakini alivumilia kiasi cha kuwa mashuhuri miongoni mwa mateka wa Iran kwenye jela hizo. Alipoachiliwa huru aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya mateka na walioachiliwa huru. ***

Miaka 11 iliyopita katika siku kama ya leo, ya tarehe Pili Juni 2013 alifariki dunia Ayatullah Sayyid Jalaluddin Taheri Imam wa kwanza wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Esfahan. Mwanazuoni huyo alizaliwa mwaka 1926 katika moja ya maeneo ya kale ya mji wa Esfahan. Alisomea taaluma za Elimu Jamii na alihitimu masomo yake pia katika taasisi ya Jumuiya ya Iran na Ufaransa na alikuwa amebobea katika lugha za Kiarabu na Kifaransa. Ayatullah Taheri alikuwa mmoja wa wanaharakati wakubwa waliopinga na kupambana na utawala wa Shah, Reza Pahlavi katika vuguvugu la Mapinduzi. Alikuwa Imam wa kwanza wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Esfahan kwa maana kwamba, hata kabla ya Mapinduzi, na kwa sisitizo la Imam Khomeini alisalisha Sala ya Ijumaa katika msikiti mkuu wa Hussein Abad. Sayyid Jalaluddin Taheri alikuwa pia mwalikishi wa Faqihi Mtawala Esfahan na mwakilishi wa mkoa huo katika Baraza la Wataalamu wa Kutunga Katiba na pia kwenye Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ana vitabu kadhaa alivyoandika na kuchapishwa kwa lugha ya Kiarabu. ***