Jun 04, 2024 23:14 UTC
  • Jumatano, 5 Juni, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 27 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1445 Hijria mwafaka na tarehe 5 Juni 2024 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 241 iliyopita baluni lilirushwa angani kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya jitihada za mwanadamu za kutaka kupaa angani. Baluni hilo lilikuwa na watu wawili, mmoja wao akiwa ni mwanafizikia wa Kifaransa aliyejulikana kwa jina la Jean-Francois Pilatre de Rozier. Tangu  alipokuwa shuleni de Rozier alikuwa akifikiria jinsi ya kutengeneza chombo cha kupaa angani na hatimaye baada ya r kutengeneza baluni, naye pia alitengeneza baluni lake na akapaa angani nalo katika siku kama hii ya leo. Mwanafizikia huyo alianguka chini na kufariki dunia katika moja ya safari zake za uhakiki angani. ***

 

Miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo yalianzishwa mapambano ya wapigania ukombozi Wairani yaliyoongozwa na Mirza Kuchak Khan Jangali dhidi ya utawala wa kiimla na uliokuwa dhalili wa Qajar na dhidi ya uporaji wa utajiri wa Iran uliokuwa ukifanywa na mkoloni Muingereza; ambapo siku iliyofuata yaani tarehe 6 Juni Mirza Kuchak Khan alitangaza "serikali ya muda ya Jamhuri". Kazi ya kuratibu harakati ya mapambano hayo ilitekelezwa na Kamati ya Umoja wa Uislamu iliyoundwa kwa ilhamu aliyopata katika fikra za wanafikra na warekebishaji umma kama Sayyid Jamaluddin Asad Abadi, Sayyid Abdurahman Kawakibi na Sheikh Muhammad Abdou; lengo likiwa ni kuleta umoja baina ya nchi za Kiislamu kwa madhumuni ya kupambana na watawala madikteta na ushawishi wa maajinabia. Kwa mtazamo wa Mirza Kuchak Khan hali ya Iran ilikuwa ya tafrani; na nchi ilikuwa imedhibitiwa na maajinabia. Kwa kufuata mielekeo ya umoja wa Uislamu alidhamiria kuunda vuguvugu la kijeshi kwa ajili ya kupambana na udikteta wa ndani na ukoloni wa nje ili kuiokoa Iran. Licha ya mapambano yaliyoendeshwa na Mirza Kuchak Khan na wafuasi wake, baadhi ya waungaji mkono wa utawala wa kikomunsti wa Urusi waliokuwemo kwenye safu za wafuasi wake waliifanyia uhaini na usaliti harakati yake. Hatimaye tofauti za baina ya viongozi na njama za wakoloni wa nje ziliivuruga harakati ya Mirza Kuchak Khan na pigo la mwisho lililoizima harakati hiyo lilikuwa ni la kuuliwa Mirza mwenyewe na utawala wa Reza Khan Pahlavi. ***

Mirza Kuchak Khan Jangali

 

Miaka 77 iliyopita, yaani tarehe Juni 1947 George Marshall, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Marekani alitangaza mpango wa utoaji mkopo wa dola bilioni tano wa kuzisaidia nchi kadhaa za Ulaya Magharibi zilizokuwa zimeathiriwa na vita. Lengo la mpango huo uliokuwa maarufu kama "Mpango wa Marshall" lilikuwa ni kuzikarabati na kuzijenga upya nchi wafuasi wa Marekani, kufutilia mbali uwezekano wa kujitokeza mielekeo ya Ukomunisti katika nchi hizo; na muhimu zaidi kuliko yote kupanua satua ya kiuchumi na kuhodhiwa Ulaya kisiasa na Marekani. Mkopo huo wa Marekani uliopambwa na nguvu za kijeshi na kipropaganda za serikali ya Washington, uliibadilisha nchi hiyo; na kwa muda mrefu baadaye ikaja ikawa moja ya madola mawili makuu yenye nguvu duniani sambamba na Urusi. ***

 

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita tarehe 16 Khordad 1368 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 6 Juni, mwaka 1989 mamilioni ya wananchi wa Iran waliokuwa na huzuni kubwa waliuzika mwili wa Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, karibu na makaburi ya mashahidi wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran ya Kiislamu, ya Behesht az-Zahra (as), pambizoni mwa mji wa Tehran. Zaidi ya wananchi na Waislamu milioni kumi kutoka miji mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi walishiriki kwenye mazishi hayo ya kihistoria. Kabla ya hapo wananchi wa Iran, waliuaga mwili wa Imam Khomeini, katika eneo la Musalla hapa mjini Tehran, na baadaye kuelekea eneo la Behesht az-Zahra kwa ajili ya mazishi. ***

Haram ya Imam Khomeini (RA)

 

Miaka 9 iliyopita katika siku kama ya leo yaani 27 Dhulqaada mwaka 1436 Hijria Qamaria winchi kubwa ya ujenzi ilianguka katika eneo moja la Msikiti Mtakatifu wa Makka na kuua idadi kubwa ya mahujaji wa Baitullah al-Haram yaani Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu. Tukio hilo lilijiri Ijumaa saa 17:10 alasiri  Septemba 11 mwaka 2015 ambapo winchi hiyo ilipelekea watu 107 kupoteza maisha na wengine 238 kujeruhiwa. Aghalabu ya waliopoteza maisha walikuwa ni mahujaji kutoka nchi za India, Pakistan, Indonesia na Iran. Wakuu wa Saudia walisema winchi hiyo ilianguka kutokana na upepo mkali. Tukio hilo la kusikitisha lilionyesha uzembe wa hali ya juu wa utawala wa Saudia. Tukio hilo la kuanguka winchi na maafa ya Mina wakati wa Sikukuu ya Idul Adha mwaka huo huo ni kati ya matukio machungu zaidi yaliyoshuhudiwa katika ibada ya Hija. ***