Ijumaa, Juni 7, 2024
Leo ni Ijumaa tarehe 29 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1445 Hijria mwafaka na 7 Juni 2024 Miladia.
Katika siku kama ya leo mwaka 220 Hijria Imam Muhammad Taqi AS mmoja kati ya wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Mtukufu huyo alipewa jina la 'Jawad' likiwa na maana ya mtu mkarimu sana kutokana na ukarimu wake mkubwa. Imam Jawad alizaliwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka 195 Hijria na kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ridha (as). Kipindi cha maisha ya Imam Jawad kilikuwa kipindi cha kuchanua utamaduni wa Kiislamu na kuenea kwa fikra, itikadi na falsafa na kujitokeza mifumo ya fikra za Wagiriki na Warumi katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam alifanya juhudi kubwa kulea kizazi chenye maarifa na kueneza elimu na mafundisho sahihi ya Uislamu kama njia ya kukabiliana na fikra za kigeni sambamba na kufichua siri na maovu ya watawala wa Bani Abbas. Suala hilo liliwakasirisha mno watawala hao ambao hatimaye waliamua kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (SAW) katika siku kama hii ya leo. ***

Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita Paul Gauguin, mchoraji mashuhuri wa Kifaransa alizaliwa mjini Paris. Alipata hamu ya uchoraji kutoka kwa mke wake ambaye alikuwa mwalimu wa uchoraji. Hatimaye aliamua kusafiri hadi katika kisiwa cha Tahiti kilichoko katika bahari ya Pacific ili kuendeleza sanaa hiyo. Akiwa katika kisiwa hicho alichora picha za kuvutia kuhusiana na mazingira na pia maisha ya watu wa kisiwa hicho hadi alipofariki dunia mwaka 1903. ***
Siku kama hii ya leo miaka 145 iliyopita, yaani tarehe 7 Juni 1879 vilianza vita vilivyochukua muda wa miaka mitano kati ya nchi za Peru, Chile na Bolivia. Vita hivyo vilianza baada ya serikali ya Bolivia kutiliana saini na shirika moja la Chile na kisha kukiuka makubaliano ya mkataba huo, na suala hilo liliifanya Chile iishambulie kijeshi Bolivia. Hatimaye Chile ilijipatia ushindi kwenye vita hivyo na kutiliana saini makubaliano mapya na nchi za Bolivia na Peru. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ufukwe wote wa Bolivia na sehemu ndogo ya ardhi ya Peru ilichukuliwa na Chile. ***

Katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita na kufuatia kushindwa Waarabu katika vita na utawala haramu wa Israel, askari wa utawala huo waliingia katika mji wa kihistoria na kidini wa Baitul Muqaddas. Waislamu wanaupa utukufu maalumu mji huo kutokana na kuwa Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu unapatikana humo na pia kutokana na kuwa ni sehemu ambayo Mtume Mtukufu (saw) alipaa kuelekea mbinguni katika tukio la Mi'raaj kutokea hapo. Tangu utawala ghasibu wa Israel uzikalie kwa mabavu ardhi za Wapalestina, umekuwa ukitekeleza njama hatari za kuuharibu msikiti huo na badala yake kujenga hapo hekalu bandia la Nabii Suleiman (as). Utawala huo vilevile unatekeleza siasa hatari ya kuvuruga muundo wa jamii asili ya wakazi wa mji wa Baitul Muqaddas kwa kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao na kujenga hapo vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na Kizayuni. Walowezi hao wa Kizayuni wanafanya njama kubwa ya kufuta kabisa nembo na alama za Wapalestina na Waislamu katika mji huo mtukufu wa Baitul Muqaddas. ***
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1980, ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia na kukiharibu kituo cha nyuklia cha Tamouz kilichoko karibu na Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Licha ya shambulizi hilo kuharibu kikamilifu kituo hicho cha nyuklia na kuzikasirisha fikra za waliowengi duniani na vilevile kulaaniwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini hakuna hatua yoyote ya kivitendo ilizochukuliwa dhidi ya utawala wa Israel. Hivi sasa utawala huo ghasibu unamiliki zaidi ya vichwa 200 vya makombora ya nyuklia, na umekuwa ukikataa kuwaruhusu wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuikagua mitambo na vinu vyake vya nyuklia. ***