Jun 08, 2024 02:46 UTC
  • Jumamosi, 8 Juni, 2024

Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1445 Hijria mwafaka na tarehe 8 Juni 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita Binti wa Mtume Muhammad (saw) Fatima al Zahraa (as) alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) Bibi Fatima alikuwa mwanamke mwema aliyejipamba kwa sifa zote nzuri ambaye alichumbiwa na shakhsia wakubwa na watu mashuhuri wa zama hizo. Hata hivyo Mtume (saw) alikuwa akiwaambia wachumbiaji hao kwamba suala la kuolewa Fatima liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Hatimaye Imam Ali bin Abi Twalib alikwenda kwa Mtume na kumchumbia Bibi Fatima na baada ya kushauriana na bintiye, Mtume alikubaliana na ombi la Ali na kuwafungisha ndoa. Baada ya kufunga ndoa, watukufu hao wawili waliishi maisha ya watu wa kawaida lakini yaliyojaa upendo, masuala ya kiroho na maadili ya Kiislamu. Watukufu hao wawili waliipa jamii ya mwanaadamu watu adhimu na kamili kama Imam Hassan, Imam Hussein na Bibi Zainab (as). Ali na Fatima (as) walikuwa kigezo bora cha mwanaadamu kamili.***

 

Miaka 859 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Ibn Abi al-Hadid alimuu na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Abu Haamid Abdul-Hamid bin Muhammad Madayani maarufu kwa jina la Ibn Abil-Hadid Mu'tazili, ni mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Muu'tazila, fakihi, mshairi, mwanafalsafa na mwandishi. Kitabu chake cha Sharh ya Nahajul-Balagha ambacho kimempatia umashuhuri zaidi kinadhihirisha mapenzi yake makubwa aliyokuwa nayo kwa Amirul-Muuminina (as) na familia ya Mtume (saw). ***

 

Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita inayosadiafiana na tarehe 8 Juni 1830, Camberz mbunifu wa Kijerumani alivumbua utengenezaji wa kiberiti. Tofauti kubwa ya kiberiti hicho cha awali na hiki kinachotumiwa hivi sasa, ni uwakaji wake uliokuwa wa taratibu. Baada ya Camberz walijitokeza watafiti wengine kadhaa waliofanya utafiti wao kuhusiana na kiberiti, na hatimaye Phillips raia wa Kimarekani alifanikiwa kutengeneza kiberiti kama hiki ambacho kinatumika leo hii. ***

 

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita kwa mujibuu wa kalenda ya Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai, mmoja wa maulamaa na wataalamu wa elimu ya irfani. Sayyid Muhammad Tabatabai alizaliwa Tabrizi huko kaskazini mwa Iran mwaka 1325 Hijiria. Akiwa na miaka 19 alielekea  Najaf, Iraq akiwa na kaka yake mkubwa, Allamah Muhammad Hassein Tabatabai na kupata elimu ya dini katika mji huo. Baada ya kutabahari katika taaluma za Kiislamu alirejea eneo alikozaliwa la Tabriz na kujishughulisha na malezi na kueneza elimu na maarifa yya Kiislamu. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha Uhusiano wa Kimaanawi Baina ya Roho na Sauti. ***

Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai

 

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, shirika la kijasusi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni. Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso mmoja wa viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO huko Paris, Ufaransa.  Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel Mossad ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo. ***

Atef Bseiso