Jun 20, 2024 22:43 UTC
  • Ijumaa, tarehe 21 Juni, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 14 Dhilhija 1445 Hijria sawa na Juni 21 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 497 iliyopita aliaga dunia Niccolò Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence.

Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo.

Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."   ***

Katika siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani, alimu mkubwa wa Waislamu. 

Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani alizaliwa mwaka 1285 Hijiria katika moja ya vijiji vya Zanjan nchini Iran. Awali alisoma kwa baba yake elimu ya dini na kidha akaelekea mjini Tehran kwa wasomi wakubwa wa zama hizo ambapo alifanikiwa kufikia daraja ya Ijtihad. Baada ya kupata elimu ya juu alianza kazi ya kufundisha.

Ameandika vitabu kadhaa kuhusu sheria za Kiislamu ikiwa ni pamoja na 'Kitaabul-Ijaarah' na 'Dhakhaairul-Ummah.' Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 75 huku akiwa ni marjaa wa Waislamu wa mji wa Zanjan.   ****

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Juni 1970, alifariki dunia Dakta Ahmed Sukarno mpigania uhuru wa Indonesia.

Sukarno alizaliwa mwaka 1901, na alikuwa mstari wa mbele katika mapambano yake dhidi ya mkoloni Mholanzi nchini humo. Kwa minajili hiyo, Sukarno aliwahi kukamatwa na kufungwa jela miaka minne na utawala wa kikoloni wa Uholanzi. Baada ya kifungo hicho alitiwa tena mbaroni na kubaidishwa.

Mnamo mwaka 1949 alichaguliwa kuwa rais wa Indonesia na ilipofika mwaka 1965 Ahmed Sukarno aliondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Janerali Suharto. ***

Na miaka 43 iliyopita sawa na tarehe Mosi Tir mwaka 1360 kwa mujibu wa Kalenda ya Kiirani, hayati Imam Ruhullah Khomeini alipasisha uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu wa kutokuwa na imani na rais wa wakati huo, Abul Hassan Bani Sadr, na kwa utaratibu huo kiongozi huyo akalazimika kung'atuka madarakani.

Bani Sadr ni miongoni mwa watu waliojidhihirisha kuwa wapenzi na watetezi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya Imam Khomeini kuhamia Paris, Ufaransa na alifanikiwa kushika madaraka ya nchi na kuwa rais katika uchaguzi wa kwanza wa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini kwa kutumia ujanja wa kipropaganda. Muda mfupi baadaye Imam Khomeini alimkabidhi ukamanda wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Hata hivyo Bani Sadr aliyekuwa mtu mwenye uchu wa madaraka, mwenye kiburi na msaliti alianza mara moja kushirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuangusha utawala wa Kiislamu nchini Iran.