Ijumaa, tarehe 5 Julai, 2024
Leo ni Ijumaa tarehe 28 Dhulhija 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Julai mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, sawa na tarehe 28 Dhulhija mwaka 63 Hijiria, yaani miaka miwili baada ya harakati na mapambano ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) yaani Imam Hussein bin Ali (AS) katika ardhi ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria, kulijiri tukio la Harrah.
Mwaka huo watu wa mji mtukufu wa Madina waliokuwa wamechoshwa na dhulma na ukatili wa mtawala Yazid bin Muawiya, walimfukuza gavana wake mjini humo, Marwan bin al Hakam. Baada ya tukio hilo Yazid alituma jeshi likiongozwa na mtumishi wake mmwaga damu na mtenda dhulma, Muslim bin Uqbah, katika mji mtakatifu wa Madina na kuliamuru kufanya mauaji makubwa mjini humo na kupora mali. Mauaji kama hayo hayakuwahi kushuhudiwa katika historia ya zama za awali za Uislamu na wanahistoria wamesema kuwa Waislamu zaidi ya elfu kumi wakiwemo maswahaba wa Mtume, waliuawa katika shambulizi hilo.
Vitabu vya historia pia vinasema utawala wa Yazid bin Muawiya ulihalalisha mji wa Madina kwa askari wake kwa muda wa siku tatu, na kwamba wasichana na wanawake wa maswahaba walinajisiwa katika tukio hilo.
Siku kama ya leo miaka 213 iliyopita, nchi ya Venezuela ilijitangazia uhuru wake na kwa sababu hiyo, tarehe 5 Julai, hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo.
Tangu mwanzoni mwa karne ya 16, na kwa kipindi cha karne tatu Venezuela ilikuwa chini ya ukoloni wa Uhispania. Katika kipindi cha ukoloni huo, raia wa nchi hiyo walipatwa na matatizo mengi, kiasi kwamba makumi ya maelfu ya Wahindi Wekundu ambao ni raia asili wa taifa hilo waliuawa na mahala pao kuchukuliwa na Wahispania.
Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, mapambano ya wananchi yalianza chini ya uongozi wa Francisco Miranda na kuzaa matunda katika siku kama ya leo mwaka 1811.
Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, alifariki dunia Nicéphore Niépce, mvumbuzi wa kamera.
Niépce alifanikiwa kusajili kwa mara ya kwanza uvumbuzi huo, mnamo mwaka 1826, baada ya kufanya majaribio kadhaa ya kielimu katika uwanja huo.
Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, wananchi wa Algeria walipata uhuru dhidi ya wavamizi wa Ufaransa baada ya mapambano makali na ya muda mrefu na wavamizi hao.
Ufaransa iliikalia kwa mabavu Algeria kwa kutegemea jeshi lake kubwa mnamo mwaka 1830. Kwa kipindi cha miaka 130 ya kukoloniwa taifa hilo, raia wa Algeria waliasisi harakati kadhaa za kupigania uhuru zilizokuwa zikiongozwa na Amir Abdulqadir al Jazairi, ambazo hata hivyo zilikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa jeshi la Ufaransa.
Hata hivyo harakati hizo zilishika kasi zaidi na kuzaa matunda baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kujipatia uhuru wake miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Zulfiqar Ali Bhutto nchini Pakistan.
Muhammad Zia-ul-Haq alitwaa madaraka yote ya waziri mkuu na rais wa Jamhuri ya Pakistan na mbali na kuwanyonga Zulfiqar Bhutto na wapinzani wake wengine, alivunja mabunge ya nchi hiyo na kusimamisha shughuli zote za vyama vya siasa nchini Pakistan.
Zia-ul-Haq aliuawa katika ajali ya ndege akiwa na maafisa kadhaa wa jeshi la Pakistan, na utawala wake ukakomea hapo.