Jumamosi, 6 Julai, 2024
Leo ni Jumamosi 29 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1445 Hijria mwafaka na 6 Julai 2024.
Katika siku kama ya leo miaka 170 iliyopita, alifariki dunia George Simon Ohm mwanahisabati na mwanafizikia wa Ujerumani akiwa na umri wa miaka 67. Simon Ohm alizaliwa mwaka 1789 na kuanza kupenda sana somo la fizikia na kufanikiwa kuvumbua kanuni katika uwanja wa umeme kutokana na utafiti mkubwa aliokuwa akiufanya katika uwanja huo. Alizipa kanuni hizo jina lake yaani "Ohm Laws". Kanuni ambazo zinatumiwa hadi leo hii. ***

Miaka 107 iliyopita katika siku kama hii ya leo inayosadifiana na tarehe 29 Dhulhija mwaka 1338 Hijria aliuawa shahidi Sheikh Muhammad Khiyabani, mwanamapambano na mpigania uhuru na kujitawala wa Iran. Alizaliwa mwaka 1297 Hijria Shamsia katika eneo la Khamene katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki. Sheikh Khiyabani alianzisha harakati za kupinga dhulma na ukandamizaji zilizokuwa zikifanywa na tawala za silsila ya Qajar hapa nchini. Baada ya kuusambaratisha udikteta wa Muhammad Ali Shah Qajar na kumlazimisha mtawala huyo kukimbia mwaka 1287 Hijria Shamsia, wananchi wa Tabriz walimchagua Sheikh Muhammad Khiyabani kuwa mwakilishi wao katika Bunge la Taifa. Hata hivyo katika siku kama ya leo Sheikh Khiyabani alikamatwa na kuuawa shahidi, wakati alipokuwa akipambana na askari wa serikali ya kifalme. ***

Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, tarehe 16 Tir 1301 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Zainul Abidin Marandi. Msomi huyo mkubwa alisoma elimu za awali katika mji aliozaliwa wa Marand, huko katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki nchini Iran. Baada ya hapo alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Ayatullah Sayyid Mohammed Hassan Husayni Nouri Shirazi na Habib Allah Rashti. Baada ya muda fulani Ayatullah Marandi alikuwa marjaa taqlidi katika maeneo ya Azerbaijan na hatimaye akafariki dunia siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 72 na kuzikwa katika makaburi ya Wadi-al Salaam mjini Najaf. ***

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Huda Karbasi, msomi mkubwa wa fiqhi na masomo mengine ya kidini. Baada ya kuhitimu masomo ya awali ya dini ya Kiislamu alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake ya kidini yapata mwaka 1281 Hijiria Shamsia, ambapo aliweza kusoma masomo ya ngazi ya juu ya usulu fiqhi na fiqhi kwa maulama wakubwa wa mji huo kama vile Ayatullah Akhund Mohammad Kazem Khorasani na Mohammed Kazem Yazdi. Aidha Ayatullah Mirza Abul-Huda Karbasi ameandika vitabu kadhaa kama vile 'Kifaayatul-Usul' 'al-Badrut-Tamaam' 'Zallatul-Aqdaam' na 'al-Fawaaidur-Rijaaliyah.' ***

Miaka 62 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. William alizaliwa mwaka 1897. Baada ya kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Faulkner alirejea tena nchini kwake. Alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake, Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili Wamarekani wenye asili ya Afrika. Hadithi za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa leo nchini Marekani. ***

Tarehe 6 Julai miaka 60 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Malawi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kabla ya Malawi kupata uhuru, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, makundi ya Wamishonari kutoka Scotland wakiwa pamoja na mvumbuzi David Livingstone waliwasili Nyasaland na kufuatiwa na Uingereza. Uingereza iliunga mkono uvamizi wa Ujerumani na Ureno huko Nyasaland na hatimaye mwaka 1891 nchi hiyo ikawekwa chini ya mamlaka yake. Kwa utaratibu huo Nyasaland ambayo ni Malawi ya leo ikawa miongoni mwa makoloni ya Uingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika. Kijiografia Malawi iko kusini mashariki mwa Afrika ikipakana na nchi za Tanzania, Zambia na Msumbiji. ***

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, visiwa vya Comoro vilipata uhuru. Raia wengi wa visiwa vya Comoro walianza kuingia katika dini ya Kiislamu na kueneza utamaduni wa dini hiyo visiwani humo, baada ya wafanya biashara wa Kiislamu kuwasili visiwani humo katika karne ya 12 Miladia. Tangu karne ya 16 visiwa vya Comoro vilikuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno na baadaye Sultan wa Oman alifanikiwa kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa visiwa hivyo. Hata hivyo mwaka 1842 sehemu kadhaa za visiwa hivyo ziliingia chini ya udhibiti wa Wafaransa na taratibu wakoloni hao wakaidhibiti ardhi yote ya nchi yote hiyo. Mapambano ya wananchi yalipelekea kutangazwa uhuru rasmi wa nchi ya Kiislamu ya Comoro mwaka 1975. Comoro ina ukubwa wa kilomita mraba 1862 na kijiografia inapatikana kusini mashariki mwa bara la Afrika katika bahari ya Hindi. ***
