Jul 14, 2024 03:49 UTC
  • Jumapili, 14 Julai, 2024

Leo ni Jumapili 8 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria mwafaka na 14 Julai 2024 Miladia.

Tarehe 8 Muharram mwaka 61 Hijria maji yaliadimika kabisa katika mahema ya mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia yake katika jangwa lenye joto kali la Karbala. Kharazmi katika kitabu cha Maqtalul Hussein na Khiyabani katika Waqaiul Ayyam wameandika kwamba: Katika siku ya nane ya Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Imam Hussein na masahaba zake walikuwa wakisumbuliwa na kiu kali, kwa msingi huo Imam Hussein alichukua sururu na akapiga hatua kama 19 nyuma ya mahema kisha akaelekea kibla na kuanza kuchimba ardhi. Maji matamu ya kunywa yalianza kutoka na watu wote waliokuwa pamoja naye walikunywa na kujaza vyombo vyao kisha maji yakatoweka na hayakuonekana tena. Habari hiyo ilipofika kwa Ubaidullah bin Ziad alimtumia ujumbe kamanda wa jeshi la Yazid mal'uuni, Umar bin Sa'd akimwambia: Nimepata habari kwamba Hussein anachimba kisima na kupata maji ya kutumia, hivyo baada ya kupata risala hii kuwa macho zaidi ili maji yasiwafikie na zidisha mbinyo na mashaka dhidi ya Hussein na masahaba zake."  ***

 

Siku kama ya leo miaka 235 iliyopita, gereza la kihistoria la Bastille lilitekwa na wakazi wa Paris katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa na sehemu kubwa ya gereza hilo ikaharibiwa. Jela hiyo ilijengwa mwaka 1369 kwa lengo la matumizi ya kijeshi. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa iligeuka na kuwa gereza la kutisha ambapo ndani yake walizuiliwa wafungwa wengi wa kisiasa hususan watu waliokuwa wakiendesha harakati za kudai jamhuri nchini humo. Gereza la Bastille lilidhihirisha udikteta wa wafalme wa Ufaransa.   ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 163 iliyopita ilitengenezwa bunduki ya kwanza ya rashasha. Bunduki hiyo ilitengenezwa na msomi wa Kimarekani Dr. Richard J. Gatling kwa kutumia uzoefu wa wavumbuzi wa kabla yake wa silaha. Bunduki iliyotengezwa na Gatling haikuwa ya utomatiki lakini baadaye teknolojia ya kutengeneza silaha hiyo ilikamilishwa zaidi na hii leo bunduki ya rashasha inatambuliwa kuwa silaha muhimu sana katika medani za vita.  ***

Moja ya bunduki za leo aina ya rashasha

 

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1318 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo katika shule ya sekondari, alijikita zaidi katika masomo ya kidini kutoka kwa baba yake, na kupiga hatua kubwa ya kielimu katika kipindi kifupi. Ayatullah Khamenei alielekea Qum kwa masomo ya juu ya kidini na kupata fursa ya kunufaika na elimu kutoka kwa maulamaa wakubwa katika mji huo, kama vile Imam Ruhullah Khomeini, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai katika masomo ya fiqh, usululi na falsafa. Akiwa bado kijana, Sayyid Khamenei alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi dhidi ya utawala kibaraka wa Shah hapa nchini, na mara kadhaa alitiwa mbaroni, kutumikia vifungo na hata kupelekwa uhamishoni. Baada ya kufariki dunia Imam Khomeini MA mwaka 1368 Hijria Shamsia, Baraza la Wanachuoni linalomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran, lilimchagua Ayatullah Khamenei, wakati huo akiwa rais wa nchi, kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. ***

Ayatullah Khamenei

 

Miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Abdul Karim Qassim alifanya mapinduzi nchini Iraq na kuuondoa madarakani utawala wa Kifalme na kisha kuanzisha mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri. Faisal II mwana wa mfalme na Waziri Mkuu wa Iraq waliuawa katika tukio hilo la mapinduzi. Aidha wafuasi wa utawala wa Kifalme walikandamizwa na kusambaratishwa kabisa. Baada ya mapinduzi hayo, Abdul Karim Qassim aliyekuwa na mirengo ya utaifa alishika hatamu za uongozi nchini Iraq hadi mwaka 1963, wakati alipokuja kuondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi pia na Abdul Salam Arif aliyekuwa muitifaki wake mkubwa na wa karibu.  ***

Jenerali Abdul Karim Qassim

 

Katika siku kama ya leo miaka 56 iliyopita yaani tarehe 24 Tir mwaka 1347 Hijria Shamsia, Ismail Balkhi mwanamapambano na mwanafikra wa Kiafghani aliuawa shahidi mjini Kabul. Alizaliwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Afghanistan. Alianza kusoma kwa bidii masomo ya dini tangu akiwa mdogo na kipindi fulani alifanya safari nchini Iran na Iraq, lengo likiwa ni kujiendeleza zaidi kielimu. Ismail Balkhi alikuwa akiendesha mapambano dhidi ya udikteta na daima alikuwa akiwashajiisha wananchi Waislamu wa Afghanistan kupambana na tawala dhalimu. Kutokana na harakati hizo, shahidi Balkhi alikuwa chini ya mashinikizo ya watawala wa wakati huo wa Afghanistan, na kwa miaka kadhaa alifungwa jela. ***

Ismail Balkhi

 

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1389 Hijria Shamsia, kwa akali watu 27 waliuawa na wengine 169 kujeruhiwa kwenye milipuko miwili ya mabomu iliyotokea katika mji wa Zahedan, ulioko kusini mashariki mwa Iran. Milipuko hiyo ilitokea mkabala na Msikiti Mkuu wa Zahedan, wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib (as) mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Kikundi cha kigaidi kilichojiita Jundullah, ndicho kilichotekeleza shambulio hilo la kigaidi. ***

 

Tags