Alkhamisi, 18 Julai, 2024
Alkhamisi tarehe 12 Muharram 1446 Hijria sawa na Julai 18 mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na wanawake na watoto wa mashahidi wa Karbala, uliwasili katika mji wa Kufa, nchini Iraq. Kiongozi wa msafara huo alikuwa Bibi Zainab (as) dada wa Imam Hussein bin Ali (as) pamoja na Imam Ali bin Hussein Sajjad (as), mtoto wa Imam Hussein (as). Imam Sajjad na Bibi Zaynab (as) walitekeleza majukumu yao kwa kufikisha ujumbe wa Imam Hussein kwa jamii ya Waislamu.
Katika siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita sawa na tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria, miili ya mashahidi wa Karbala ukiwemo mwili mtukufu wa mjukuu wa Mtume (saw) Imam Hussein AS ilizikwa ikiwa ni siku mbili baada ya kuuawa shahidi na kuachwa jangwani.
Mashahidi wa Karbala walizikwa na watu wa kabila la Bani Asad. Mwili wa Imam Hussein na mashahidi wote wa Karbala ilibakia kwa siku mbili bila ya kuzikwa kwani hakuna mtu aliyekuwa na ujasiri wa kuzika miili hiyo kutokana na hofu ya utawala dhalimu wa Bani Umayyah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo wanawake wa kabila la Bani Asad waliwahamasisha wanaume wao kuzika miili hiyo mitakatifu ya wajukuu wa Mtume na masahaba wa Imam Hussein (as).
Siku kama ya leo miaka 1351 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Imam Ali Zainul Abidin maarufu kwa lakabu ya Sajjad mwana wa Imam Hussein (as) na mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW, aliuawa shahidi.
Imam Zainul Abidin alizaliwa mwaka 38 Hijria huko katika mji wa Madina. Mtukufu huyo aliishi katika zama ambapo watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu walikuwa wakikabiliwa na masaibu mengi. Imam Sajjad A.S ambaye alikuwa mgonjwa wakati wa tukio la Karbala, baada ya harakati adhimu ya Imam Hussein, alibeba jukumu kubwa la kueneza ujumbe wa mapambano hayo na kuendeleza njia ya baba yake.
Katika siku kama ya leo miaka 1153 iliyopita, kilianza kipindi cha vita vya miaka 25 kati ya Uingereza na Denmark katika karne ya 9.
Alfred The Great, mfalme kijana wa Uingereza alikuwa kamanda mashuhuri wakati wa kujiri vita hivyo katika kipindi hicho. Wadenmark katika siku hiyo waliivamia Uingereza na kuiteka ardhi kubwa ya nchi hiyo.
Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka 25 hatimaye vilifikia tamati kwa Waingereza kupata ushindi mnamo tarehe 9 Januari mwaka 896. ***
Miaka 243 iliyopita katika siku kama ya leo William Herschel, mtaalamu maarufu wa nujumu wa Uingereza alifanikiwa kugundua hakika ya kundi la nyota na sayari ikiwemo hii yetu ya dunia.
Alitumia darubini kubwa aliyokuwa ametengeneza kwa ajili ya kutazama nyota na kuthibitisha kwamba, kundi la nyota na sayari linaundwa na nyota nyingi ikiwemo sayari ya dunia ambayo ni sehemu ndogo sana ya kundi hilo. Herschel pia ndiye mvumbuzi wa sayari ya Uranus. Alifariki dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 84.
Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Kiislamu Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa.
Ayatullah Kashiful Ghitaa alizaliwa katika mji mtakatifu wa Najaf katika familia ya wasomi na wacha-Mungu na kuanza kutafuta elimu akiwa bado mtoto mdogo. Baada ya kukamilisha elimu ya msingi, Ayatullah Kashiful Ghitaa alihudhuria darsa za maulamaa wakubwa wa zama hizo na kukwea daraja za juu za elimu katika kipindi kifupi. Alifanikiwa kulea wasomi na maulamaa wakubwa na kufanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa.
Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu pia alikutambua kushiriki katika masuala ya kisiasa na kutilia maanani masuala ya serikali na utawala kuwa ni katika mambo ya wajibu na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha Harakati ya Kitaifa ya Iraq.
Ayatullah Kashiful Ghitaa alishiriki vilivyo katika mapigano ya jihadi ya wananchi wa Iraq wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya jeshi vamizi la Uingereza. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Zuheir Muhsein, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Harakati ya al Sa'iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa mashirika ya ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad) na lile la Misri huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa.
Maajenti wa tawala hizo mbili walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo. Zuheir Muhsin alikuwa mpinzani mkubwa wa mapatano ya kisaliti ya Camp David na aliwahi kutishia mara kadhaa kwamba harakati yake ya al Sa'iqa itamuua mtawala wa wakati huo wa Misri, Anwar Sadaat aliyetia saini makubaliano hayo na wazayuni.
Na tarehe 18 Julai, ni "Siku ya Kimataifa ya Mandela".
Mwaka wa 2009, Umoja wa Mataifa ulitangaza siku hii kuwa siku mahsusi kwa Nelson Mandela, mwasisi wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Umoja wa Mataifa uliitangaza siku ya kuzaliwa Mzee Nelson Mandela, yaani tarehe 18 Julai kuwa Siku ya Kimataifa ili kuenzi mchango wake mkubwa katika harakati ya kupigania uhuru nchini Afrika Kusini na juhudi zake kubwa za kutangaza amani, kutilia maanani utatuzi wa migogoro baina ya kaumu na nchi mbalimbali, kutetea haki za binadamu, na kuwepo usawa na maelewano baina ya wanadamu wa mbari na kaumu zote.
Mandela alifariki dunia tarehe 5 Disemba mwaka 2013.