Jul 26, 2024 02:36 UTC
  • Ijumaa, tarehe 26 Julai, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 20 Muharram 1446 Hijria, sawa na 26 Julai mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 177 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Liberia ilipata uhuru.

Liberia iko katika mwambao wa bahari ya Atlantic na inapakana na nchi za Guinea, Sierra Leone na Ivory Coast. Idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo yenye jumla ya watu milioni tatu wanafuata dini za kijadi na kimila na asilimia 16 ya raia wake inaundwa na Waislamu. Lugha rasmi ya raia wa Liberia ni Kingereza.

Liberia iliundwa mwaka 1822 kwa ajili ya Waafrika waliokuwa watumwa huko Marekani. Mwaka 1841 nchi hiyo iliandika katiba na kupewa jina la Liberia lenye maana ya ardhi ya watu huru.   

Miaka 168 iliyopita katika siku kama ya leo George Bernard Shaw mwandishi, muigizaji wa michezo ya kuchekesha na mkosoaji wa Ki-Ireland alizaliwa katika mji wa Dublin.

Baba yake alikuwa mtumishi wa serikali. Akiwa katika rika la kuinukia George Bernard alianza kuandika visa na tamthiliya. Alijitihidi kutoa taswira ya matatizo ya kijamii katika visa vyake. 1925 Shaw alitunukiwa tuzo ya nobel ya fasihi.     

George Bernard Shaw

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, Gamal Abdul-Nasser rais wa wakati huo wa Misri alitangaza kuutaifisha Mfereji wa Suez.

Mfereji huo ulianzishwa mwaka 1896 baada ya Misri kukaliwa kwa mabavu na Uingereza na kwa utaratibu huo, njia ya baharini baina ya Ulaya na Asia ikawa imefupishwa. Udhibiti wa Uingereza na Ufaransa kwa Mfereji wa Suez uliendelea hadi serikali ya Abdu l-Nasser ilipokuja kuutaifisha na kuutangaza kuwa mali ya taifa. Hatua hiyo ilifuatiwa na mashambulio ya kijeshi ya Uingereza, Ufaransa na utawala dhalimu wa Israel.

Hata hivyo mashinikizo ya kimataifa dhidi ya madola vamizi na mapambano ya wananchi Waislamu wa Misri, yalivifanya vikosi vamizi viondoke katika mfereji huo muhimu na ukawa katika miliki ya serikali na taifa la Misri. 

Gamal Abdul-Nasser

Katika siku kama ya leo miaka 59 iliyopita visiwa vya Maldives huko kusini mwa bara Asia vilipata uhuru.

Visiwa vya Maldives vilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Wareno mwanzoni mwa karne ya 16. Visiwa hivyo baadaye vilidhibitiwa na Waholanzi na Wafaransa na hatimaye mwishoni mwa karne ya 19, vikakaliwa na Waingereza.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, yaani tarehe 26 Julai mwaka 1979,  Zuheir Mohsen, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Harakati ya as-Sa'iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni (Mossad) huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa.

Magaidi wa Kizayuni walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo na polisi wa Ufaransa walidai kuwa hawakupata uthibitisho kwamba Mossad ilihusika na mauaji hayo.   

Zuheir Mohsen

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 5 Mordad mwaka 1358 Hijria Shamsiya, iliswaliwa rasmi Swala ya kwanza ya Ijumaa katika mji wa Tehran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Tehran ikiongozwa na marehemu Ayatullah Talaqani, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu, kufuatia agizo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Swala ya Ijumaa haikuwa ikifanyika kutokana na kuweko anga ya udhibiti na ukandamizaji wa serikali ya Shah. 

Ayatullah Talaqani akiongoza Swala ya Ijumaa, Tehran

Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi mfalme wa mwisho wa Iran aliaga dunia huko Cairo, Misri.

Aliingia madarakani baada ya baba yake yaani Rezakhan kuondolewa kwenye uongozi na kubaidishwa na Waingereza. Kama alivyokuwa baba yake, Muhammad Reza Pahlavi alikuwa na uhusiano mkubwa na Uingereza na ndio maana akafanya jitihada za kulinda maslahi haramu ya nchi hiyo nchini Iran. Hata hivyo baada ya harakati za wananchi na kushinda harakati ya kuitaifisha sekta ya mafuta, maslahi ya Waingereza nchini Iran yalifikia tamati.

Shah aliwakandamiza wananchi wa Iran kwa ngumi ya chuma na alikuwa kibaraka mkubwa wa Marekani. Suala hilo lilizidisha kasi ya harakati za Mapinduzi ya Kiislamu zilizoongozwa na hayati Imam Khomeini na mwaka 1357 Mapinduzi ya Kiislamu yalihitimisha utawala dhalimu wa Shah ambaye alikimbilia nje ya nchi na kufia Misri katika siku kama hii ya leo.   

Reza Pahlavi

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, ilianza operesheni kubwa ya kijeshi iliyopewa jina la "Mirsad" huko magharibi mwa Iran kwa lengo la kuwasambaratisha vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqin (MKO).

Kundi la Munafiqin ambalo lilikuwa limekusanya magaidi katika mpaka wa Iran na Iraq wakiwa na silaha nzito kutoka kwa utawala wa zamani wa Baghdad lilianza kuishambulia ardhi ya Iran siku mbili kabla ya kuanza operesheni hiyo. Kiongozi wa Munafiqin alidhani kuwa magaidi hao wangeweza kuvuka barabara kuu za Iran bila ya kizuizi na tabu yoyote na kufika haraka mjini Tehran.

Hata hivyo wanajeshi wa Iran wakishirikiana na wananchi waliojitolea katika operesheni hiyo ya Mirsad waliwazingira vibaraka hao wa Munafiqin huko magharibi mwa nchi na kuwasambaratisha magaidi hao walio na uhusiano mkubwa na nchi za kigeni.

Operesheni ya Mirsad

 

 

Tags