Aug 08, 2024 02:24 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 8 Agosti, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 2024.

Siku kama ya leo miaka 2357 iliyopita sawa na tarehe 8 Agosti 333 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, ilianza kazi ya ujenzi wa mji wa Alexandria nchini Misri, ambao leo hii unahesabiwa kuwa moja kati ya bandari muhimu kusini mwa Bahari ya Mediterranean.

Ujenzi huo ulifanyika kwa amri ya Alexander Macedon huko kaskazini mwa Misri. 

Miaka 1389 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Mwezi 3 Safar mwaka 57 Hijria Qamaria, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, alizaliwa katika mji wa Madina, Imam Muhammad Baqir (AS), mjukuu kipenzi wa Bwana Mtume SAW na Imamu wa Tano wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. 

Ukamilifu wa kimaanawi na kielimu ambayo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu waliyotunukiwa Ahlubayti wa Mtume SAW, ulidhihirika kwa uwazi katika shakhsia ya Imam Muhammad Baqir (AS) pia. Katika kipindi cha miaka 19 ya Uimamu wa mtukufu huyo, ambacho kilisadifiana na miaka ya mwishoni ya utawala wa Bani Umayyah, yalipatikana mazingira mwafaka katika jamii kwa yeye kuweza kuimarisha misingi ya kifikra na kiutamaduni ya Waislamu. Taaluma nyingi zilistawishwa na kuenea katika jamii ya Waislamu kupitia chuo cha fikra cha mtukufu huyo pamoja na mwanawe, yaani Imam Jaafar Sadiq (AS); na hata wanafunzi wake walikuja kuwa wavumbuzi wa fani mbalimbali mpya za elimu.

Lakini sambamba na hayo, Imam Baqir hakughafilika na kupambana na dhulma na uonevu wa utawala wa kijabari wa Bani Umayyah na ndiyo maana katika mwaka 114 Hijria Qamaria aliuliwa shahidi na mtawala wa zama hizo. Tunachukua fursa hii pia kukupeni mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa kwa mjukuu huyo kipenzi wa Mtume SAW.      

Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 1998, wanamgambo wa kundi la Taliban nchini Afghanistan waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Mazar Sharif ulioko kaskazini mwa nchi hiyo.

Baada ya kukaliwa kwa mabavu mji huo, wanamgambo wa Taleban waliushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji huo na kuwauwa shahidi wanadiplomasia 8 wa Kiirani na mwandishi mmoja wa habari.

Kundi la Taliban liliasisiwa mwaka 1994 kwa ufadhili na usaidizi wa Marekani na Pakistan na kufanikiwa kuikalia sehemu kubwa ya ardhi ya Afghanistan.     

 

Tags