Sep 03, 2024 02:21 UTC
  • Jumanne, Septemba 3, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 29 Safar 1446 Hijria sawa na Septemba 3 mwaka 2024.

Tarehe 29 Safar miaka 1129 iliyopita aliaga dunia Abu Abdullah Muhammad bin Jabir bin Sinan ambaye alikuwa mwanahesabati mkubwa na mashuhuri wa Kiislamu. Muhammad bin Sinan alikuwa miongoni mwa wanafalsafa, wanajimu na wataalamu wakubwa na gwiji wa nyota wa Kiislamu. Hakuwa na mfano katika elimu ya hisabati katika zama hizo.

Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa nchini Misri na alitumia muda wa miaka 40 kufuatilia sayari na nyota. Abu Abdullah bin Sinan alifanikiwa kuainisha wakati halisi wa mwaka wa jua na ameandika vitabu kadhaa kama vile Taadilul Kawakib na Miqdarul Ittisalat.

Muhammad bin Sinan

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, Damascus mji mkongwe na wa kihistoria wa Kiislamu ulikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Uingereza.

Moja kati ya malengo makuu ya serikali za Ulaya wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia ilikuwa kuugawa utawala wa Othmania, lengo ambalo baadaye lilifanikiwa.

Wakati utawala wa Othmania ulipokuwa ukigawanywa, maeneo yaliyokuwa chini ya utawala huo, nayo moja baada ya jingine yalidhibitiwa na Ufaransa na Uingereza, ambapo mji wa Damascus katika Syria ya leo, pia ulishambuliwa na katika siku kama ya leo ukakaliwa kwa mabavu. Hata hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla kati ya London na Paris, Syria ukiwemo mji mkuu wake, Damascus, ilidhibitiwa na Ufaransa.

Damascus

Miaka 85 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufaransa na Uingereza ziliitangazia vita Ujerumani na kwa utaratibu huo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikaanza.

Baada ya jeshi la Ujerumani kuishambulia Poland, serikali ya Uingereza iliitumia Ujerumani ujumbe ikiitaka iondoke haraka katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Poland. Hata hivyo Ujerumani ilipuuza takwa hilo la Uingereza. Baadaye Uingereza iliipatia Ujerumani makataa ya kuhitimisha operesheni zake za kijeshi. Hata hivyo Adolph Hitler kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi alikataa kutekeleza takwa hilo.

Hatimaye katika siku kama ya leo, Uingereza na Ufaransa zikaitangazia vita Ujerumani. Sio Adolph Hitler pekee ambaye hakutaraji kama Ufaransa na Uingereza zingeingia vitani kwa ajili ya Poland bali hata Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti pia hakutarajia hilo.   

Katika siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, mkataba wa kusalimu amri Italia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ulitiwa saini baina ya wawakilishi wa Italia na nchi waitifaki.

Kwa mujibu wa mkataba huo, Waziri Mkuu wa Italia alikubali bila masharti kusalimu amri nchi yake na kwa utaratibu huo, mmoja wa waitifaki muhimu wa Ujerumani ya Kinazi katika vita hivyo, akawa ameondoka katika medani ya vita. 


Benito Mussolini

Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Qatar ilipata uhuru toka kwa mkoloni Mwingereza. Qatar iliwahi kudhibitiwa na Ufalme wa Othmania. Hata hivyo kufuatia kudhoofika utawala huo, Qatar ambayo kuanzia mwaka 1882 na kuendelea kivitendo ilikuwa ikiendeshwa na Uingereza, mwaka 1916 nchi hiyo ya Kiarabu ikawa imetambuliwa rasmi kuwa koloni la Muingereza. Hadi mwaka 1971 Qatar ilikuwa bado inakoloniwa na Uingereza ambapo mwaka huo huo, kwa ushirikiano wa viongozi wa eneo la pambizoni mwa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, likaundwa Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu.

Hata hivyo mnamo Septemba mwaka huo huo, yaani 1971, Qatar ilijiondoa katika Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu na kujitangazia uhuru.

Na tarehe 13 Shahrivar miaka 46 iliyopita kulifanyika maandamano ya kwanza ya mamilioni ya Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa Shah. Maandamano hayo yalianza baada ya Swala ya Eid-ul-Fitr kutoka sehemu nne za Tehran. Waandamanaji waliokuwa wamebeba picha kubwa ya Imam Ruhullah Khomeini (RA), kiongozi wa hayati wa Mapinduzi ya Kiislamu, walipaza sauti na nara za kudai uhuru, kujitawala na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Maandamano hayo makubwa ya mamilioni, ambayo yalikuwa msingi wa maandamano ya kihistoria ya tarehe 17 Shahrivar ya mwaka huo huo, yalimalizika baada ya Sala ya jamaa ya adhuhuri.

Maandamano ya Waislamu wa Iran dhidi ya Shah