Nov 21, 2024 17:18 UTC
  • Alkhamisi, Novemba 21, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Jamadil Awwal 1446 Hijria sawa na Novemba 21 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 535 iliyopita Abulfadhl Abdulrahman Suyuti, mashuhuri kwa lakabu ya Jalaluddin, faqihi, mpokezi wa hadithi na mtaalamu maarufu wa lugha wa zama hizo alifariki dunia mjini Cairo.

Jalaluddin Suyuti alizaliwa mwaka 849 Hijria na alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana. Jalaluddin Suyuti kwa miaka kadhaa alijifunza masomo ya fiqih, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na lugha na kupata mafanikio makubwa.

Msomi huyo wa Cairo ameandika vitabu vingi vya thamani na miongoni mwavyo ni "Al Iqtirah", "Al Kitabul Kabir" na "Tarikhul Khulafaa".

Miaka 241 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Novemba mwaka 1783, kwa mara ya kwanza katika historia ya jitihada za mwanadamu za kupaa angani, puto lilitumwa angani.

Puto hilo lilikuwa limepandwa na watu wawili mmoja akiwa mwanafizikia wa Ufaransa aliyejulikana kwa jina la Pilatre De Rozier.

Tangu alipokuwa masomoni De Rozier alikuwa akifikiria kutengeneza wenzo wa kupaa angani na kwa kutengeneza puto hilo mwanafizikia huyo akawa amefanikiwa kuruka angani. 

De Rozier

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, Butros Butros Ghali alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa. Butros Ghali alizaliwa mwaka 1922 katika familia ya Kikristo katika mji mkuu wa Misri Cairo.

Baada ya kumaliza masomo yake Butros Butros Ghali alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Siasa cha Cairo. Mwanadiplomasia huyo ndiye aliyemshawishi na kumshajiisha Anwar Sadat, Rais wa zamani wa Misri, kutia saini mkataba wa Camp David mwaka 1978 na katika kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel. 

Butros Butros Ghali

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita inayosadifiana na 21 Novemba 1995, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Makubaliano ya Amani ya Dayton", yalitiwa saini.

Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na Waserbia.

Zaidi ya Waislamu laki moja waliuawa kwa umati katika vita vya Bosnia. 

Makubaliano ya Dayton

Na siku hii ya leo tarehe 22 Novemba imetangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Televisheni.

Lengo la Umoja wa Mataifa la kuianisha siku hii lilikuwa kuweko mabadilishano ya vipindi vya runinga hususan vipindi vinavyotayarishwa kwa lengo la kueneza amani, ustawi wa kijamii na kiuchumi na kuimarisha masuala ya kiutamaduni katika jamii.