Sep 07, 2024 02:29 UTC
  • Jumamosi, 7 Septemba, 2024

Leo ni Jumamosi 3 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria mwafaka na 7 Septemba 2024 Miladia.

Tarehe 3 Rabiul Awwal miaka 1005 iliyopita alifariki dunia mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu, Abul Alaa al Ma'arri. Alizaliwa mwaka 363 Hijria katika Syria ya sasa na baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."

Abul Alaa al Ma'arri

 

Katika siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, nchi ya Brazil ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Ureno ilianza kuikoloni Brazil mwaka 1494, na mbali na kuwatumikisha watu wa jamii ya Wahindi Wekundu wa nchi hiyo, ilichukua mamilioni ya Waafrika kwa ajili ya kuwatumikisha kama watumwa katika shughuli za kilimo. ***

 

Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita harakati ya kihistoria ya Wanamasumbwi nchini Uchina ilikandamizwa na kuzimwa. Wanamasumbwi lilikuwa jina walilopewa wanajeshi wa China waliosimama kupambana na ubeberu wa nchi za kigeni hususan za Magharibi ulioambatana na harakati za wamishonari wa Kikristo ndani ya China. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na wanamasumbwi hao ni kuteka balozi za nchi za Magharibi katika mji wa Beijing na kupambana vikali na shughuli za wahubiri wa Kikristo kutoka Ulaya. Harakati ya Wanamasumbwi wa Kichina ilikandamizwa na majeshi ya Ulaya, Marekani na Japan na serikali ya China ikalazimika kulipa gharama kubwa kwa nchi hizo. ***

Harakati ya Wanamasumbwi nchini Uchina

 

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi wa utawala wa kidikteta wa Pahlavi walishambulia maandamano makubwa ya wananchi wa mji wa Tehran na kuua raia wengi. Wananchi Waislamu wakazi wa Tehran siku hiyo walianza kuandamana tangu asubuhi, hayo yakiwa maandamano ya siku kadhaa mfululizo kuwahi kufanywa na wakazi wa mji wa Tehran dhidi ya utawala wa kibaraka wa Pahlavi. Wakati huo, utawala wa kijeshi ulikuwa umetangazwa katika mji wa Tehran, lakini wananchi Waislamu walipuuza hali hiyo na wakamiminika mitaani wakipiga nara dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo huo, walinzi maalumu wa Shah walifanya mashambulizi na katika muda mfupi wakawaua shahidi wananchi zaidi ya elfu nne wa Tehran waliokuwa wakipigania haki zao. ***

Harakati ya 17 Shahrivar

 

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita alifariki dunia dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji. ***

Mobutu Sese Seko

 

Tags