Alkhamisi, tarehe 19 Septemba, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na 19 Septemba mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, mafuta ya petroli ya makaa ya mawe yalizalishwa kwa mara ya kwanza katika historia ya juhudi za mwanadamu za kupata vyanzo au mada za kuzalisha nishati.
Mada hiyo mpya ya kuzalisha joto na nishati ilivumbuliwa na James Young, mwanakemia wa Scotland.
Young alikuwa mmiliki wa mgodi wa makaa ya mawe na alifanikiwa kutengeneza mafuta ya petroli kwa kutumia makaa hayo kupitia njia inayojulikana kitaalamu kama (distillation).
Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, serikali ya kwanza huru iliundwa na viongozi wa mapinduzi nchini Algeria. Harakati za wananchi wa Algeria dhidi ya mkoloni Mfaransa zilianza mwanzoni wa Novemba 1954 sambamba na kushika kasi harakati za kupigani uhuru za wananchi hao. Nalo Jeshi la Ukombozi wa Algeria likaundwa kwa shabaha ya kuratibu mapambano.
Tarehe 19 Septemba mwaka 1958 serikali ya muda ya Algeria ikatangaza uwepo wake. Hatimaye kushindwa jeshi la Ufaransa kusambaratisha harakati ya wananchi wa Algeria, kulipelekea Algeria ijitangazie uhuru mwaka 1962.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita Kuwait na Marekani zilisaini makubaliano ya kijeshi.
Makubaliano hayo yalisainiwa karibu miezi sita baada ya Iraq kuhitimisha kuikalia kwa mabavu Kuwait. Viongozi wa Kuwait walidai kwamba, lengo la makubaliano hayo, ni kuzuia kutokea tena uvamizi mwingine wa Iraq dhidi ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya kijeshi, Marekani iliruhusiwa kutumia bandari za Kuwait na kutuma wanajeshi na zana zake za kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo na nchi mbili hizo kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi.
Mwaka 1991, Kuwait ikatiliana saini makubaliano kama hayo na Uingereza na Ufaransa. Miaka iliyofuatia, Bahrain, Qatar, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu zilisaini makubaliano ya kijeshi na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo kinyume na matarajio ya viongozi wa nchi hizo za Ghuba ya Uajemi, makubaliano hayo badala ya kuwaletea amani, yalipelekea kutokea ushindani wa kumiliki silaha na kushadidi ukosefu wa amani katika Mashariki ya Kati.
Na miaka 30 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi elfu 20 wa Marekani walifanya mashambulizi ya anga na baharini na kuikalia kwa mabavu nchi ndogo ya Haiti inayopatikana katika bahari ya Caribean huko kusini mwa Marekani.
Washington ilidai kuwa imeishambulia Haiti ili imrejeshe madarakani Rais Jean Bertrand Aristide wa nchi hiyo. Mwezi Septemba mwaka 1991 Jenerali Raoul Cedras alimpindua Aristide ambaye ndio kwanza alikuwa uongozini kwa muda wa miezi minane.
Baada ya mapinduzi hayo Rais Jean Bertrand Aristide alikimbilia Marekani.
Na siku kama ya leo, miaka 13 iliyopita, tarehe 29 mwezi Shahrivar kwa mwaka wa Hijria Shamsia aliuawa Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama nchini Afghanistan, Burhanuddin Rabbani.
Alizaliwa tarehe 20 Septemba mwaka 1940. Alikuwa kiongozi wa chama cha Jumuiya ya Kiislamu nchini humo na rais rasmi wa kwanza wa utawala wa Mujahidina huko Afghanistan. Hadi mwisho wa maisha yake, Burhanuddin Rabbani alikuwa mkuu wa Baraza Kuu la Usalama lililoundwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Hamid Karzai. Baraza hilo lilikuwa na wadhifa wa kufanya mazungumzo na kundi la Taleban kwa lengo la kufikiwa suluhu na kumaliza mgogoro wa taifa hilo kwa njia ya amani.
Rabani aliuawa katika siku kama ya leo na gaidi aliyekuwa ameficha bomu katika kilemba chake, wakati alipoingia ofisini kwa mwanasiasa huyo kwa madai ya kufanya mazungumzo.