Sep 20, 2024 07:48 UTC
  • Ijumaa, tarehe 20 Septemba, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 16 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na Septemba 20 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1445 kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Swala ya kwanza ya Ijumaa iliswaliwa na Mtume Muhammad (saw) baada ya mtukufu huyo kuhama mji wa Makka.

Baada ya kuwasili katika eneo la Bani Salim bin Auf kwa jina la Quba karibu na Madina wakati wa adhuhuri, Mtume (saw) alitoa hotuba na kusimamisha Swala ya Ijumaa mahala hapo. Wanahistoria wanasema hiyo ilikuwa Swala ya kwanza ya Ijumaa katika Uislamu.

Hatua hiyo pia inaonesha umuhimu wa ibada hiyo ya kiroho na kisiasa ambayo Bwana Mtume aliamua kuitekeleza mara tu baada ya kuwasili karibu na mji wa Madina. Baadaye Waislamu walijenga msikiti katika eneo hilo palipofanyika Swala ya Ijumaa ya kwanza katika Uislamu. 

Msikiti wa Quba

Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, lilitengenezwa basi la kwanza lililokuwa likitumia nishati ya mvuke.

Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 30 na kwenda kwa kasi ndogo na lilitengenezwa na Gordon Branz, raia wa Uingereza.

Hii leo mabasi bora na ya kisasa ni miongoni mwa vyombo muhimu vya usafiri kote duniani. 

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, nchi ya Hungary iliungana na ardhi ya Austria, na Francois Joseph akawa mtawala wa kifalme wa nchini mbili hizo.

Hungary ambayo kwa mara kadhaa katika historia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na nchi zenye nguvu za Ulaya kama vile Austria na utawala wa Othmania, baadaye ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka 1918 mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia. 

Francois Joseph

Tarehe 20 Septemba miaka 45 iliyopita, Jean-Bedel Bokasa, dikteta wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Bokasa alizaliwa mwaka 1922 na kusomea nchini Ufaransa. Alikuwa shabiki mkubwa wa Napoleon Bonaparte na Charles de Gaulle, viongozi wawili wa zamani wa Ufaransa.

Bokasa alichukua madaraka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 1966 baada ya kufanya mapinduzi dhidi ya binamu yake, David Dacko, wakati Bokasa alipokuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo. 

Jean-Bedel Bokasa alitawala nchi hiyo kwa mfumo wa kiimla na kwa kipindi cha miaka 13 na kusimamia moja kwa moja wizara 14 kati ya wizara 16 za nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.   

Jean-Bedel Bokasa

 

Tags