Oct 03, 2024 10:52 UTC
  • Ukoloni, tangu mwanzo hadi leo (4)

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika Episodi ya Nne ya Podikasti tuliyoipa jina la Ukoloni Tangu Mwanzo hadi Leo. Podikasti hii inazungumzia historia na jinsi ilivyojitokea fikra hii ya ukoloni katika nukta tofauti duniani, sababu na madhara yake makubwa. Podikasti hii inazungumzia pia aina mbalimbali za ukoloni.

Katika Episodi ya Nne ya podikasti hii, ambayo kimsingi inategemea yaliyoandikwa katika kitabu "Ujue Ukoloni" cha Mustafa Eskandari, itazungumzia na kuchambua sababu za msingi za kujitokeza ukoloni. Tafadhali endelea kuwa nasi hadi mwisho.

***********************

Katika episodi zilizopita yaani za kwanza, pili na tatu, tulitoa maana ya neno ukoloni na vipindi vyake vitatu tofauti, yaani kipindi cha ukoloni wa zamani, ukoloni mpya na ukoloni wa hivi leo. Vile vile tumechunguza sifa za kila moja ya vipindi hivi, kisha tukagundua kwamba mara zote ukoloni unahitajia kuandaa mazingira maalumuu ya kufikia malengo yake, na hatua ya kwanza katika kuweza kutambua shabaha ya ukoloni ni kuijua nchi inayolengwa katika masuala ya kidini, kiutamaduni kaumu na makabila na muundo wake wa kijamii. Baada ya kupata taarifa hizo ndipo wakoloni huwanza uporaji na kuanzisha na kuendeleza ukoloni.wao. Wanatumia wenyeji wa maeneo hayo, majeshi ya kigeni na vikundi mbalimbali kama vile wamishionari wa Kikristo, wataalamu wa masuala ya mashariki, washauri, wasomi, na watu wajinga kuweza kufanikisha malengo yao maovu. Katika episodi iliyopita tulizungumzia makundi ya mishionari wa Kikristo na wataalamu wa masuala ya mashariki mwa dunia walivyotumika kufanikisha malengo ya kikoloni. Katika episodi hii ya nne tutazungumzia makundi mengine tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho. 

**************************************

Washauri, watu wanaojifanya wasomi na watu wajinga ni makundi mengine ambayo ukoloni unayatumia kufikia malengo yake maovu.

Kundi la tatu linalochangia kutokea ukoloni ni la "washauri" ambao kwa ujumla huingia katika nchi nyingine kwa kujifanya ni washauri wa kiuchumi, kijeshi na kitamaduni na kuweka msingi wa ukoloni wao. Vikundi hivi huingia katika nchi kwa njia ya kisheria kama balozi na ujumbe wa kidiplomasia au hata kuchukua nafasi ya moja kwa moja ya ushauri kwa serikali za nchi nyingine lakini miongoni mwa kazi zao ni kukusanya taarifa muhimu na kuzipeleka kwa serikali za nchi zao. Jambo la ajabu kuhusu makundi haya ambalo huwarahisishia kazi zao, ni kinga yao ya kidiplomasia. Kinga hii ni kubwa kiasi kwamba kwa kawaida taarifa muhimu na za siri hutolewa nje ya nchi fulani na kupelekwa katika nchi nyingine bila ya kukaguliwa kwa namna yoyote ile na serikali kwa sababu siri hizo hufichwa chini ya hati miliki ya mizigo ya kidiplomasia mali ya ubalozi.

Mfano mzuri wa kazi za kikoloni za washauri hao, ni zile nyaraka za kijasusi zilizopatikana kwenye ubalozi wa Marekani uliokuwepo mjini Tehran ambao hivi sasa ni maarufu kwa jina la pango la kijasusi la Marekani. Baada ya kuingia katika ubalozi huo, hati hizi ziligunduliwa na kikundi cha wanafunzi Waislamu wa Iran walojulikana kwa jina la wanafunzi wanaofuata njia ya Imam Khomeini (RA) na kuchapishwa kwenye vyombo vya habari. Nyaraka hizo za siri zilionesha kwa uwazi vitendo vya kikoloni vya Marekani nchini Iran.

Kundi jingine linalofanikisha njama za kikolini ni za wasomi vibaraka wa Magharibi.

Makundi ambayo tumeyazungumzia huko nyuma kuwa ni sababu ya kutokea ukoloni, yote yalikuwa ni makundi ya kigeni. Lakini kuna hili kundi jingine ambalo ni hatari zaidi nalo ni la wenyeji wa nchi na jamii ambao lakini wametekwa na fikra za kikoloni na za Magharibi. Kundi hili la nne ni la watu wanaojiita wasomi. Ni wenyeji wa nchi zinazokoloniwa, lakini kazi yao si kutumikia nchi na mataifa yao, bali ni kutumikia madola ya kikoloni.

Ili kupanua udhibiti wao wa kiutamaduni na fikra za watu wa nchi iliyokoloniwa, wakoloni wanatumia mbinu hiyo ya kuwarubuni baadhi ya watu wa nchi hizo na kuwapa majina makubwa kama wasomi na wanafikra na baadaye kuwatumia kwa malengo yao ya kikoloni. Wakoloni wameamua kwamba mbali na kutumia washauri, wanahitaji pia vibaraka wa ndani wawafanikishie malengo yao maovu na ili kupitia vitimbakwiri hivyo, waweze kuzidhibiti zaidi kiutamaduni nchi hizo. 

Wasomi hao ni wale watu ambao kawaida wanapinga dini, wana mitazamo finyu na hasi kuhusu dunia na fikra zao kimsingi ni za kupinga mila na desturi za kaumu na jamii zao. Ni watu ambao wanapinga jadi zao, wanapinga masuala ya dini na masuala ya kiroho na kimaanawi na shabaha yao kuu ni kupandikiza na kueneza fikra za kilahidi na kumkataa Mwenyezi Mungu Muumba. 

Wasomi wa namna hiyo katika Ulimwengu wa Kiislamu walianza kujitokea kwa mara ya kwanza katika nchi za Iran, Uturuki, Misri, Syria na Lebanon na kushiriki katika propaganda za kikoloni. Mfano mzuri na mkubwa wa vitimbakwiri hivyo vya wakoloni, ni Mustafa Kamal Pasha, anayejulikana kama Atatürk. Ataturk alitoka kwenye familia ambayo, kwa mujibu wa mwanahistoria Muingereza, Arnold Joseph Toynbee, ilikuwa na damu ya Kiyahudi kwenye mishipa yake. Baada ya kuingia madarakani nchini Uturuki, Kemal Mustafa Pasha au Ataturk alileta uzushi mwingi katika miundo ya kidini ya jamii ya Waturuki. Miongoni mwa uzushi huo ni kama ifuatavyo: 

Alibadilisha herufi za Kiarabu za lugha ya Kituruki na kuzifanya za Kilatini
Alipiga marufuku ya Hija kwa miaka kadhaa
Alifunga skuli za kidini
Aliwafukuza wasomi wenye misimamo imara
Alipiga marufuku ya mavazi ya staha ya Kiislamu (hijab)
Alifuta suala kwamba Uislamu ndiyo dini rasmi nchini Uturuki.

Ni kwa sababu hiyoi ndio maana wakati wabunge wa Uingereza walipompinga Lord Curzon, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa nchi hiyo na kumuuliza kwa nini ameuamua kuipa Uturuki uhuru wake, aliwajibu kwa kuwaambia: :

"Kuanzia sasa (yaani baada ya madaraka kuhodhiwa na Ataturk), Uturuki haitabakia kuwa Uturuki mnayoijua kwa sababu nguvu ya Uturuki iliyotokana na Uislamu na ukhalifa, tumeimaliza."

Wabunge wa Uingereza walimpigia makofi na kuunga mkono hotuba yake. 

******************************************

Watu wajinga na wasio na ufahamu wa kutosha ni mawakala wengine wakuu wa kuendeleza na kufanikisha malengo ya kikoloni. Watu hao bila ya kujua wanaingia katika mitego ya kutumikia malengo ya wakoloni na kuwasaidia kufikia shabaha zao.

Kundi hili limegawanyika katika mafungu mawili makuu ya waovu.

Kundi la kwanza ni la watu wajinga ambao wana fikra mgando na ambao wana welewa wa juu juu sana tu wa dini. Hao ni wale watu ambao hawathamini kabisa mafundisho ya dini. Hili ndilo kundi la kwanza la watu hao wajinga ambao wanajifanya kuwa ni watu wa dini lakini wana fikra mgando bali hawathamini mafundisho ya dini. Watu hao wanajifanya kujua kila kitu, lakini kwa hakika ni sawa na sehemu za makali za mkasi ambazo kila sehemu inakuwenda upande wake lakini mwisho hukata kitu kilichopo katikati ya makali hayo. Watu hao mwisho wake huishia kwenye kutumikia malengo ya wakoloni. 

Wasomi hao wenye fikra mgando kama za jiwe ambao ni wapinzani wa dini, katika muda wote wa historia na kwenye vita baina ya hahki na batili, wao wako kwenye upande wa kupiga vita haki na kupigania badili. Ni kwa sababu hiyo ndio maana kuna baadhi ya mambo ambayo Maimamu maasumu waliwaonya watu kuhusu watu hao kwa kutumia minasaba na nyakati tofauti. 

Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib AS ambaye ni Imam wa Kwanza wa Waislamu wa Kishia anasema haya kuhusu wasomi wa aina hiyo: 

"Makundi mawili yamenivunja mgongo, wasomi wasio na dini na watu wenye dini lakini wasio na elimu wala muono wa mbali. Amma mtu mwenye dini lakini akawa mjinga na asiyeona mbali, anawazuia watu kuipenda dini kutokana na ibada na matendo yake ya songombingo na yule msomi asiye na dini anawapotosha watu kwa kukosa kwake taqwa na kumuogopa Mwenyezi Mungu. 

Kwa upande wake Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema:

“Fikra za kipumbavu za namna hii ambazo wanazo baadhi ya watu zinawasaidia wakoloni na serikali za kidhalimu kuzidi kuzikandamiza nchi za Kiislamu na kupambana na harakati za Kiislamu. Hizo ni fikra za kundi la watu ambao wanajifanya watu bora kuliko wengine wakati hawana ubora wowote. Inabidi fikra za watu hao tuzirekebishe. Ni wajibu wetu kutangaza kutoridhiana nao kwani fikra hizo ni kikwazo kwa mabadiliko na mapambano yetu.

Kundi la pili la watu duni na dhalili linaundwa na wapumbavu. 

Watu duni au kwa maneno mengine majambazi ni wale wasio na elimu sahihi ambao ni viranja wa kutumikia malengo ya kikoloni.

Sifa kuu ya watu duni hawa ni kwamba yumkini wakati panapojitokeza hali ya kupambanishwa haki na batili, kheri na shari, jambo sahihi na ghalati, wakapatia baadhi ya wakati kujua haki, jambo sahihi na la kheri ni lipi lakini sehemu ambayo pana shari mbili, mambo yanapochanganyika yasiyo ya sawa, yaliyo ghalati na batili, hapo watu hao wanakuwa hawana nguvu za kubainisha na kugundua kuwa yote hayo ni shari na yote hayo mawili ni ghalati na batili na akachagua ambalo shari yake ni ndogo zaidi.

Kuhusiana na suala hili imenukuliwa kutoka kwa Imam Ali AS akisema:

"لیسَ الْعاقِلُ مَنْ یَعرِفُ الْخَیرَ مِنَ الشَرَّ ـ وَلکِنُّ العاقِلَ مَن یَعْرِفُ خَیْرَ الشَّرَّینِ"

"Mwenye akili si yule awezaye tu kupambanua kheri na shari, bali mwenye akili hasa ni yule awezaye kupambanua iliyo afadhali kati ya shari mbili."

Katika dunia ya leo ambapo mfumo unaotawala sehemu nyingi duniani ni wa demokrasia ya kutegemea kura za wananchi, makundi haya yanaona yamepata fursa nzuri ya kutumikia malengo haramu ya wakoloni. Watu wa makundi hayo wananaathiriwa mapema mno na propaganda za kihadaa za wakoloni kuliko watu wengine na wako tayari kuliangamiza hata taifa zima kwa kutegemea propaganda hizo na kudai wanalalamikia matokeo ya uchaguzi hata kama ushahidi wote utaonesha kuwa wameshindwa. 

Tunaweza kutolea mfano wakati wa kusambaratika vuguvugu la kuyafanya mafuta kuwa ni mali ya taifa nchini Iran yaani mwanzoni mwa miaka ya 1950. Wakati huo kundi moja lililoongozwa na mtu aitwaye Shaaban Jafari, aliyejulikana kwa jina maarufu la Shaaban Bei Mokh, lilifanya fujo na kuandaa mazingira ya kufanyika mapinduzi ya aibu yaliyoiondoa madarakani serikali ya wananchi ya Dk Mohammad Mossadegh. Matokeo yake yalikuwa ni Iran kuwekwa chini ya udikteta wa mfalme Mohammad Reza Pahlavi aliyekuwa kibaraka wa pande zote wa Marekani. 

Mfano mwengine wa njama kama hizo ulitokea baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaani tarehe 29 Agosti 1981. Wakati huo makundi yasiyo na ghera wala uchungu na taifa lao waliwaua shahidi makumi ya shakhsia bora wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran akiwemo Ayatullah Dk Beheshti aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mahakama, Rais wa wakati huo wa Iran, Mohammad. Ali Rajaee na Mohammad Javad Bahonar waliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran wakati huo. 

**********************************************

Naam wasikilizaji wapendwa, episodi nyingine ya Podikasti hii ya Ukoloni Tangu Mwanzo hadi Leo (Sehemu ya Nne) imefikia tamati. Katika episodi hii tumezungumzia mambo ya msingi na kuchambua sababu na makundi yanayosaidia kufanikisha malengo haramu ya madola ya kikoloni. Tumezungumzia nafasi ya wamishionari wa Kikristo, makundi ya washauri, makundi ya wasomi wajinga n.k na kuonesha ni jinsi gani makundi hayo yanachangia ufanikishaji wa malengo ya kikoloni katika mataifa tofauti duniani. Tunakaribisha maoni yenu kupitia WhatsApp na Telegram yetu ya +989035065487 na b-pepe yetu ya [email protected].

Tuna hamu ya kusikia maoni yako kuhusu podikasti hii na kama una mapendekezo kuhusu maudhui nyingine, usiache kutuandikia ili tuiandikie podikasti mpya kwa manufaa ya watu wengi zaidi. 

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags