Nov 14, 2024 02:38 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 14 Novemba, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 12 Jamadil Awwal 1446 Hijria sawa na 14 Novemba 2024.

Siku kama ya leo miaka 491 iliyopita, ardhi ya Ecuador inayopatikana huko Amerika ya Kusini iligunduliwa na wavumbuzi wa Kihispania na kuunganishwa na ardhi zilizokuwa zikidhibitiwa na Uhispania.

Ecuador ilikoloniwa na Uhispania kwa karne tatu. Hata hivyo mwaka 1822 wananchi wapigania ukombozi wa nchi hiyo chini ya uongozi wa Simon Bolivar walifanikiwa kurejesha uhuru wa nchi hiyo na Ecuador ikajiunga na Shirikisho la Colombia Kubwa. 

Miaka 308 iliyopita katika siku kama ya leo, Gottfried Wilhelm Leibnitz mwanahisabati na mwanafalsafa wa Kijerumani aliaga dunia mjini Hanover Ujerumani akiwa na umri wa miaka 70. Wilhelm Leibnitz alianza kuzisoma kwa bidii na juhudi elimu za falsafa na hisabati akiwa na umri wa miaka 15 alifanikiwa kupata shahada za juu kabisa katika masomo hayo.

Elimu na ufahamu mkubwa na mchango aliotoa katika elimu ya hisabati pamoja na vitabu alivyoandika kuhusiana na elimu hizo, ni mambo yaliyomfanya Gottfried Wilhelm Leibnitz awekwe katika faharasa ya wasomi maarufu wa falsafa na hisabati nchini Ujerumani. 

Gottfried Wilhelm Leibnitz

Katika siku kama ya leo miaka 227 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Novemba mwaka 1897, alizaliwa Charles Lyell mtaalamu wa masuala ya ardhi na mwanasayansi wa Scottland. Lyell alikuwa mtu wa kwanza kuweka misingi na kanuni sahihi za kielimu katika masuala ya geolojia.

Baada ya kufanya utafiti mkubwa hatimaye aliandika kitabu cha mijadala mitatu kuhusiana na misingi ya elimu ya utambuzi wa ardhi alichokipa jina la Principles of Geology.

Charles Lyell

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, Jawaharlal Nehru mmoja kati ya viongozi wakubwa wa harakati ya mapambano ya India dhidi ya mkoloni Mwingereza alizaliwa huko Allahabad kaskazini mwa India.

Nehru alianza mapambano dhidi ya mkoloni Mwingereza baada ya kujiunga na harakati ya kitaifa ya ukombozi wa India. Jawaharlal Nehru alitiwa mbaroni mara kadhaa na kufungwa jela kutokana na mchango na nafasi yake kubwa katika mapambano hayo. Baada ya Mahatma Ghandi kujiunga na harakati ya kitaifa ya India, wanaharakati hao wakiongoza mapambano ya kupigania uhuru ya wananchi wa India walitoa pigo kubwa kwa mkoloni Mwingereza. Hatimaye India ilipata uhuru Agosti 15 mwaka 1947.

Jawaharlal Nehru

Miaka 135 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Dakta Taha Hussein mwandishi na mwanafasihi mtajika wa Misri.

Msomi huyo mashuhuri alipofuka macho akiwa mtoto. Hata hivyo kipaji chake cha hali ya juu kilimuwezesha kuendelea na masomo na hadi kufikia mwaka 1918 alikuwa amekamilisha masomo yake ya shahada ya uzamivu katika vyuo vikuu vya Misri na Ufaransa.

Dakta Taha Hussein mbali na kuwa kipofu, aliweza pia kushika nyadhifa za juu ndani na nje ya Misri na kipindi fulani alikuwa Waziri wa Utamaduni wa Misri.

Dakta Taha Hussein

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, utungaji na upasishaji wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulikamilishwa na Baraza la Wataalamu.

Katiba hiyo ilianisha na kuupasisha mfumo wa Kiislamu uliojengeka juu ya misingi ya mafunzo na matukufu ya Kiislamu hasa uadilifu katika jamii na kuheshimiwa haki za binadamu.

Baada ya katiba hiyo kupasishwa kulifanyika kura ya maoni ya wananchi wote na katiba hiyo ikapasishwa kwa wingi wa kura.   

Tarehe 24 Aban miaka 45 iliyopita, siku chache baada ya kuvamiwa na kutekwa Pango la Ujasusi la uliokuwa ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran, serikali ya Marekani katika radiamali yake kali dhidi ya hatua hiyo ya kimapinduzi, ilizuia fedha za kigeni za Iran katika mabenki yake yote duniani.

Kufungwa kwa akaunti za Iran, kulipelekea mashinikizo ya kiuchumi ya serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuchukua mkondo mpana zaidi.

Siku chache kabla ya hatua hiyo, Iran ilikuwa imesimamisha uuzaji wa mafuta yake kwa Marekani kutokana na hatua na misimamo ya chuki ya Washington dhidi ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa, mfasiri mkubwa wa Qur'ani na msomi mashuhuri wa Kiislamu, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai akiwa na umri wa miaka 80.

Mwanazuoni huyo mkubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa hodari sana katika elimu za falsafa, irfani, tafsiri ya Qur’ani na vilevile katika masuala ya fasihi, hisabati na fiqhi. Allamah Tabatabai ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni tafsiri ya Qur'ani ya al-Mizan. 

Allamah Tabatabai

Leo tarehe 14 Novemba ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kisukari.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, kuanza na kustawi kwa miji, kubadilika muundo na mtindo wa chakula na kupungua harakati na mazoezi sahihi ya mwili kumetayarisha mazingira ya kuongeza kiwango cha sukari ya damu na ugonjwa wa kisukari. Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yanayoongezeka duniani kila mwaka.

Siku hii ya tarehe 14 Novemba, ni siku ya kuzaliwa "Sir Frederick Grant Banting", mgunduzi wa insulini, na ilipewa jina la Siku ya Kisukari Duniani kwa mara ya kwanza mnamo 1991 kwa ushirikiano na Shirikisho la Kimataifa la Kisukari (IDF) na Shirika la Afya Duniani (WHO). 

Madhumuni ya kupewa jina hilo ni kuongeza uelewa wa umma kuhusu sababu, matatizo, kinga na matibabu ya ugonjwa huo unaoongezeka kkila siku.