Jul 25, 2016 06:03 UTC
  • Jumapili Julai 24, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 19 Shawwal mwaka 1437 Hijria, inayosadifiana na tarehe 24 Julai 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1172 iliyopita, alifariki dunia mjini Gundeshapur, moja ya miji ya zamani ya Iran, Ya'qub al-Layth al-Saffar, mwasisi wa silsila ya wafalme wa ukoo wa Safari nchini Iran. Sifa njema za Ya'qub al-Layth al-Saffari  ziliwafanya watu kuvutiwa naye huku akichaguliwa kwa muda fulani na wananchi wa Sistan, kusini mashariki mwa nchi hii kuwa kiongozi wao. Baada ya muda punde Ya'qub al-Layth al-Saffari na kwa uungaji mkubwa wa wananchi alifanikiwa kutawala miji kadhaa ya Iran na hivyo kumfanya kuweza kuunda utawala mmoja katika mji wa Sistan na miji mingine ya jirani. Mwaka 261 Hijiria, kiongozi huyo akiongoza jeshi kubwa, alielekea Iraq kwa lengo la kuudhibiti mji wa Baghdad ambao wakati huo ulikuwa ukitawaliwa na watawala wa Bani Abbas. Hata hivyo al-Layth al-Saffari alishindwa na jeshi la watawala hao wa Bani Abbasi na kulazimika kurudi nyuma.

Siku kama ya leo miaka 1003 iliyopita alizaliwa Abu Zakariya Yahya Bin Abdul-Wahhabi, maarufu kwa jina la Ibn Mandah, mtaalamu wa hadithi, sheria za Kiislamu na mwanahistoria mkubwa wa Iran. Abu Zakariya Yahya Bin Abdul-Wahhabi alikuwa mtu wa mwisho miongoni mwa kizazi cha Ibn Mandah ambapo baada ya kuhitimu masomo ya enzi hizo kutoka kwa wasomi wakubwa, alijikita katika ufundishaji na kuandika vitabu. Kuna athari nyingi kutoka kwa mwanahistoria na mtaalamu huyo wa hadithi, moja ya athari hizo kikiwa ni kitabu kinachoitwa 'Zendegi Nameh Tabaran.' 

Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita Simón Bolívar mwanasiasa na mwanamapinduzi maarufu wa Amerika ya Kusini alizaliwa huko Caracas mji mkuu wa Venezuela. Simon Bolivar alikomboa ardhi kubwa ya Amerika ya Kusini kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kihispania. Vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Caracas na kufanikiwa kuiteka Bogota huko katikati mwa Colombia.Simon Bolivar aliteuliwa kuwa Rais na Congress iliyokuwa imeundwa kwa shabaha ya kuasisi Colombia Kubwa na alifanikiwa kuzikomboa ardhi za Colombia, Venezuela na Panama. Mwaka 1822, mapambano ya ukombozi yaliyokuwa yakiongozwa na Bolivar yalienea hadi Ecuador na nchi hiyo ikajiunga na Colombia Kubwa, baada ya kupata uhuru.

Miaka 214 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas. Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa.

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita Jumuiya ya Mataifa iliipatia mamlaka rasmi serikali ya Uingereza ya kuzidhibiti Palestina, Iraq na eneo la mashariki mwa Jordan huku usimamizi wa Syria na Lebanon ukipewa serikali ya Ufaransa. Hata hivyo Paris na London ziliafikiana katika Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya hapo juu ya kugawana utawala wa kifalme wa Othmania na uamuzi huo wa Jumuiya ya Mataifa kuhusu mgao ilioutoa kwa nchi mbili hizo ukahalalisha suala hilo.

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita sawa na tarehe 24 Julai 1944, wanajeshi wa kikosi cha anga cha Uingereza walifanya mashambulizi makali dhidi ya bandari muhimu ya Hamburg huko kaskazini mwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Uingereza na Ujerumani zilianza kushambuliana mwanzoni mwa vita hivyo. Mashambulizi ya nchi mbili hizo yalishadidi baadaye na kuua raia wengi wasio na hatia wa nchi mbili hizo. 

Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, alifariki dunia Bi, Ismat Setarezadeh, mtafiti na mfasiri mashuhuri wa Iran. Bi Ismat alizaliwa mwaka 1290 Hijiria katika mji wa Tabriz, kaskazini mashariki mwa Iran. Na baada ya kuhitimu masomo ya msingi alijishughulisha na kazi ya ualimu. Baada ya kufiwa na mume wake huku akiendelea na jukumu la kulea watoto, aliamua kuendelea na masomo yake na kufikia daraja ya PHD katika fani ya lugha na fasihi ya Kifarsi. Mbali na lugha ya Kifursi alizungumza lugha ya Kiturki ambapo alifasiri vitabu kadhaa kutoka lugha moja kwenda nyingine.

 

Image Caption

 

Tags