Jan 01, 2025 03:45 UTC
  • Jumatano, tarehe Mosi Januari, 2025

Leo ni Jumatano tarehe 30 Jamadil Awwal 1446 Hijria sawa na Januari mwaka 2025.

Leo ni tarehe Mosi Januari inayosadifiana na kuanza mwaka mpya wa 2025 Miladia.

Mpangilio wa miezi ya mwaka wa Kirumi unaoanza Januari hadi Disemba ulianza kutumiwa katika kipindi cha Mfalme Numa Pompilius wa Roma yapata miaka 700 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masih (as).

Kwa msingi huo tarehe 31 Disemba huwa siku ya mwisho ya mwaka wa Miladia na usiku wa kuamkia tarehe Mosi Januari huanza sherehe za kupokea mwaka mpya katika jamii za Wakristo na nchi nyingi za Afrika, America, Ulaya, Australia na hata Asia.

Tunawatakia heri ya mwaka mpya watu wote wanaoadhimisha mwaka huu.  ****

Miaka 221 iliyopita sawa na tarehe Mosi Januari mwaka 1804 nchi ya Haiti ilijitangazia uhuru ikiwa nchi ya kwanza kufanya hivyo katika eneo la Amerika ya Latini.

Uhuru wa Haiti ulipatikana kufuatia mapambano na harakati kubwa ya watumwa weusi wa nchi hiyo dhidi ya vitendo vya utumwa vya Ufaransa na kisha baadaye kuanzisha mapambano dhidi ya jeshi la Ufaransa. Ufaransa ilianza kuikoloni Haiti mwaka 1677.

Baada ya kujipatia uhuru, Haiti ilikumbwa na machafuko ya ndani.   ***

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita Heinrich Rudolf Hertz mwanafizikia  na mwanahisabati wa Ujerumani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 37. Alizaliwa mjini Hamburg Ujerumani mwaka 1857. Alikuwa na mapenzi makubwa na fizikia na umakenika tangu akiwa kijana mdogo. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akajiendeleza kimasomo katika uwanja huo.   ***

Heinrich Rudolf Hertz 

Miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo nchi ya Sudan ilipata uhuru kutoka kwa Misri na Uingereza. Mwaka 1899 Uingereza na Misri zilitiliana saini mkataba wa kuitawala kwa pamoja Sudan. Katikati mwa karne ya 20 lilianza vuguvugu la kutaka kujipatia uhuru nchini Sudan na mwaka 1956 Misri na Uingereza zikalazimika kuutambua uhuru wa nchi hiyo. Sudan inapakana na nchi za Sudan Kusini, Misri, Libya, Chad, Kenya, Uganda, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.   ***

Miaka 83 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ayatullah Fayyaz Zanjani fakihi na msomi mahiri wa elimu ya Usuul.

Awali alisoma masomo yake kwa Mujtahidi Akhund Mullah Muhammad. Baadaye akahudhuria masomo kwa walimu mahiri wa zama hizo mjini Tehran kama Mirza Muhammad Hassan Ashtiyani na kuwa mahiri katika taaluma za fikihi, Usuul, mantiki na tafsiri.

Mwanazuoni huyo alikuwa Marjaa Taqlidi wa Zanjani. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 30 alikuwa mmoja wa waeneza mafundisho ya Ahlul Bait na waalimu wakubwa wa Maktaba ya Ushia.  ***

Ayatullah Fayyaz Zanjani

Tarehe Mosi Januari mwaka 1959 miaka 66 iliyopita mapinduzi ya Cuba yalipata ushindi na dikteta Fulgencio Batista akaikimbia nchi hiyo.

Ushindi wa mapinduzi hayo yaliyoongozwa na Fidel Castro uliiweka Marekani katika mazingira magumu baada ya kushindwa vibaraka wake nchini Cuba. ***  

Miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani ambayo iliikalia kwa mabavu Cameroon kuanzia mwaka 1884.  Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Ufaransa na Uingereza ziligawana baina yao ardhi ya Cameroon. Hata hivyo haukupita muda kabla ya kuanza mapambano ya kupigania uhuru nchini humo.

Hatimaye mapambano ya kupigania uhuru nchini Cameroon yalizaa matunda katika siku kama ya leo baada ya nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika kujipatia uhuru. ***

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita nchi ya Brunei ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.

Nchi hiyo ndogo na yenye wakazi wachache kijiografia iko kusini mashariki mwa Asia. Tangu kale mfumo wa utawala nchini Brunei ulikuwa wa Kifalme ambao ulikuwa ukisimamiwa na Uingereza.

Brunei inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani kutokana na kuwa na akiba kubwa ya mafuta na gesi.   ***

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Januari 1993, yalianza kutekelezwa makubaliano ya Maastricht, eneo lililoko kusini mwa Uholanzi yaliyokuwa na lengo la kuondoa mipaka ya kiuchumi kati ya nchi 12 za Ulaya.

Mkataba wa muungano wa Ulaya ulitiwa saini tarehe 10 Disemba mwaka 1991 na viongozi wa nchi 12 wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya katika mji mashuhuri wa Maastricht. Baadaye Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya ilibadilishwa na kuwa Umoja wa Ulaya.

Utekelezwaji wa makubaliano ya Maastricht ulikuwa hatua kubwa katika mchakato wa kuungana zaidi wanachama wa Umoja wa Ulaya japo kuwa umoja huo ulikabiliwa na matatizo mengi katika miaka iliyofuatia.   ***

Na miaka minne iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Muhammad Taqi Mesbah Yazdi, faqihi, mfasiri wa Qur'ani na profesa wa chuo kikuu cha Qum nchini Iran.

Allamah Misbah Yazdi alianzisha Taasisi ya Utafiti wa Kisayansi ya Baqirul Uloom, na kisha Taasisi ya Utafiti ya Imam Khomeini huko Qum. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya kiislamu alishika nyadhifa nyingi ikiwa ni pamoja na mwakilishi wa watu wa Mkoa wa Khorasan katika Baraza la Wataalamu, mjumbe wa zamani wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni, mjumbe wa Jumuiya ya Maprofesa wa Semina ya Qum, na rais wa zamani wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt.

Miongoni mwa kazi zake, tunaweza kutaja kitabu cha maarifa ya Qur;ani chenye juzuu 9 na pia Mafundisho ya Falsafa katika juzuu mbili.